Simba haipoi

MSHAMBULIAJI John Bocco amevunja mwiko wa maafande wa Mbeya, Prisons na kuwafunga bao pekee katika mechi ya Ligi Kuu Bara iliyochezwa kwenye Uwanja wa Sokoine na Simba kuibuka na ushindi wa bao 1-0.

Ushindi huo wa Simba ni baada ya kushindwa kushinda kwa miaka mitatu iliyopita kwenye uwanja huo wa Sokoine. Bao hilo lilifungwa dakika ya 84 baada ya mabeki wanne wa Prisons kushindwa kuokoa mpira uliokuwa miguuni mwa Bocco.

Kutokana na ushindi huo Simba itaendelea kubaki kileleni mwa msimamo wa ligi kwa pointi 22, ikiendelea kusubiri matokeo ya mechi ya Azam na Njombe Mji leo ambapo kama Azam itashinda italingana pointi na Simba.

Katika mechi ya jana, Simba ilitawala mpira kipindi cha kwanza huku wapinzani wao wakionekana kucheza kwa kujihami zaidi na kuruhusu mashambulizi. Kipindi hicho cha kwanza Simba ilitengeneza nafasi mbili kupitia kwa Shiza Kichuya na Mwinyi Kazimoto na kushindwa kuzitumia ipasavyo.

Kadhalika, Prisons walitengeneza nafasi moja hawakuitumia ipasavyo. Kipindi cha pili Kocha Joseph Omog alifanya mabadiliko ya kikosi chake kwa kuwatoa Haruna Niyonzima, Kazimoto na Mzamiru Yassin na kuingia Mohamed ‘Mo’ Ibrahim, Laudit Mavugo na Ally Shomari ambapo kuingia kwao kulibadili mchezo kwa asilimia kubwa.

Mabadiliko hayo yalichangia Simba kushambulia na kuwasumbua mabeki wa Prisons mara kwa mara ambapo Mo, Mavugo na Bocco walionekana kusumbua kwenye lango la wapinzani na kuwalazimisha mabeki pinzani kurudi nyuma kulinda zaidi badala ya kushambulia.

Mbali na mchezo huo uliochezwa Mbeya, Ruvu Shooting ikiwa nyumbani Mabatini, Mlandizi ilipata ushindi wa kwanza wa bao 1-0 dhidi ya Ndanda FC. Ushindi huo umeondoa gundu lililowapata msimu huu na pengine sasa watapata nguvu ya kupambana katika michezo inayofuata.

Aidha, Majimaji ilipata ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Mbao FC kwenye Uwanja wa Majimaji Songea huku Stand United ikipata sare ya bila kufungana 0-0 dhidi ya ndugu zao wa Shinyanga, Mwadui FC.