Simba kufumua kikosi

KUFUATIA sare ya bao 1-1 dhidi ya Lipuli FC juzi, kocha msaidizi wa Simba, Masud Djuma amekiri kikosi chake kina mapungufu na wanalazimika kufanya usajili kwenye dirisha dogo ili kubaki kwenye mbio za kuwania ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu huu.

Simba pamoja na kutangulia kupata bao la mapema na kuutawala mchezo kwa asilimia kubwa katika mechi hiyo iliyochezwa uwanja wa Uhuru mwishoni mwa wiki iliyopita, ilijikuta ikimaliza dakika 90, kwa sare hiyo hali iliyowachukiza mashabiki wake kwani walikuwa na nafasi ya kuongeza wingi wa pointi kileleni.

Sare hiyo imeifanya Simba kufikisha pointi 23, lakini kuongoza kwake kileleni mwa msimamo kulitarajia matokeo ya mechi ya jana usiku kati ya Azam na Mtibwa Sugar.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya mchezo huo, Djuma, alisema kilichosababisha washindwe kupata ushindi ni mapungufu yaliyopo kwenye kikosi chao ambacho hakikusajiliwa vizuri kulingana na ushindani uliopo kwenye ligi.

“Tulicheza vizuri na kutengeneza n dwa kuzitumia nafasi tulizozipata tatizo kubwa timu yetu inayo mapungufu na nilazima tusajili kipindi hiki cha usajili tunahitaji kuongeza wachezaji watatu hadi wanne ili kukiimarisha kikosi na kuanza kufikiria ubingwa,” alisema.

Kocha huyo aliyetua Simba hivi karibuni akirithi mikoba ya Mganda Jackson Mayanja alisema, nafasi ambazo wanatarajia kuongeza wachezaji ni kipa, beki wa kati na pembeni na mshambuliaji mmoja.

Djuma alisema kama wakifanikiwa kuzijaza nafasi hizo anaamini Simba itakuwa na uhakika wa ushindi katika kila mchezo watakaocheza na kuwa miongoni mwa timu ambazo zinapigania taji la ubingwa linaloshikiliwa na Yanga.

Kwa upande wake kocha wa Lipuli, Selemani Matola aliwapongeza wachezaji wake kwa kazi nzuri waliyoifanya hadi kupata sare hiyo lakini akasema siri kubwa ya matokeo hayo ni kucheza kwa nidhamu na kuwaheshimu Simba kutokana na uzoefu waliokuwa nao.

“Tulicheza kwa nidhamu kubwa sana kwa sababu Simba ni timu kubwa inawachezaji wazoefu hivyo nilazima tucheze kwa tahadhari lakini wakati huo tukifanya mashambulizi ya kustukiza ili kupata bao nashukuru mbinu zetu zilifanikiwa,” alisema Matola