Ubingwa wawapagawisha Kenyatta na Ruto

RAIS wa Kenya Uhuru Kenyatta na makamu wake William Ruto wamepagawa na ushindi wa kombe la Chalenji kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati na tangu juzi wamekuwa akitamba kwenye mitandao ya kijamii wakiwapongeza wachezaji wao.

Timu ya soka ya Taifa ya Kenya, Harambee Stars juzi ilitwaa ubingwa wa kombe la Chalenji michuano inayoandaliwa na Baraza la vyama vya soka Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) kwa kuifunga Zanzibar Heroes kwa mikwaju ya penalti 3-2.

Timu hizo zililazimika kupigiana mikwaju ya penalti baada ya kutoka sare ya mabao 2-2 katika dakika 120. Mwingine aliyeipongeza Harembee Stars alikuwa rais wa Shirikisho la soka la Kenya, Nick Mwendwa aliyemshukuru Gavana Alfred Mutua (Machakos), Wycliffe Oparanya (Kakamega) na Anyang’ Nyongo (Kisumu) kwa majimbo yao kuwa wenyeji wa michuano hiyo.

“Kwa niaba ya serikali, naipongeza timu yetu ya taifa, Harambee kwa kufanya vizuri kuanzia hatua ya awali mpaka kutwaa ubingwa wa Cecafa,” Kenyatta aliandika kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Facebook.

“Hongera, mmetufanya tujivunie”. Ruto, ambaye aliongoza Wakenya kwenye Uwanja wa Machakos kushuhudia fainali hizo, alimpongeza kipa wa Harambee Stars, Patrick Matasi, kwa kuokoa mikwaju mitatu ya penalti ya Zanzibar na kuipa timu yake ubingwa wa saba wa michuano hiyo.

Ruto ameahidi kuwapa wachezaji Sh milioni 5 za Kenya. “Shujaa kipa Patrick Matasi amewaongoza mashabiki wa Harambee Stars kuifunga Zanzibar 3-2 kwa mikwaju ya penalti na kutwaa taji la Chalenji la Cecafa 2017,” aliandika Ruto kwenye ukurasa wake wa Facebook.

Mwendwa pia alitumia nafasi hiyo kuwashukuru mashabiki kwa kujitokeza kwa wingi uwanjani. “Shukran kwa mashabiki wote mliokuja uwanjani leo (juzi) na kwa siku 20 nyingine zilizopita, Mungu awabariki, Mungu aibariki Kenya,” alisema Mwendwa. Mwandishi wa habari za michezo Collins Okinyo aliipongeza Stars kwa ushindi na Zanzibar kwa kuonesha soka safi.