Yanga haihofii timu yoyote

BAADA ya kufanikiwa kutinga nusu fainali ya michuano ya Kombe la Mapinduzi, kocha msaidizi wa Yanga, Shedrack Nsajigwa amesema kamwe hawaihofi i timu yoyote katika michuano hiyo.

Yanga katika michuano hiyo inatumia idadi kubwa ya wachezaji chipukizi na kuchanganya na wazoefu na katika mechi ya nusu fainali huenda ikakutana na timu zenye wachezaji wazoefu, ambazo ni Azam au URA kwa kuwa Simba imetolewa jana.

Akizungumza katika mchezo dhidi ya Zimamoto ambayo Yanga ilishinda bao 1-0, na kufikisha pointi 12 sawa na Singida United, Nsajigwa alisema wamekwenda kwenye michuano hiyo wakiitumia kama mazoezi na hawaihofii timu yoyote hata kama ina uwezo kiasi gani.

Kocha huyo ambaye anamsaidia George Lwandamina aliyepo kwao Zambia alikokwenda baada ya kufiwa na mwanawe, alisema wanachotaka kuona ni uwajibikaji wa wachezaji wao na kupata uzoefu wa kutosha kutokana na malengo waliyokuwa nayo kwenye michuano ya kimataifa.

Alisema kutokuwepo kwa Donald Ngoma na Obrey Chirwa siyo tatizo kubwa kwao kwa sababu wachezaji waliopo wanafanya vizuri na timu inapata ushindi, kwa hiyo amewataka mashabiki wa timu hiyo kuondoa wasiwasi kwani ana imani timu yao itafanya vile wanavyotarajia.