Azam kuendeleza vichapo Ligi Kuu

KOCHA Mkuu wa mabingwa wa Kombe la Mapinduzi mwaka 2018, Azam FC, Aristica Cioaba amesema kuwa na kipa bora kumechangia timu yake iweze kutwaa taji hilo.

Azam imetwaa taji hilo kwa changamoto ya mikwaju ya penalti 4-3, dhidi ya URA ya Uganda baada ya kwenda suluhu katika muda wa kawaida huku kocha wao akitamba sasa kuelekeza nguvu katika Ligi Kuu Bara.

Akizungumza na gazeti hili mara baada ya mchezo kumalimalizia Cioaba, alisema ilikuwa ni fainali ngumu na yenye ushindani, lakini ubora wa kipa wake, Razak Abalora ndiyo imewapa heshima na kufanikiwa kutetea taji hilo.

“Lazima niwapongeze wachezaji wote kwa kazi nzuri waliyoifanya, lakini hasa kipa wangu Abalora ni kijana mdogo, ameonesha uwezo mkubwa tangu amejiunga na sisi msimu huu,” alisema Cioaba.

Kocha huyo raia wa Romania alisema, pamoja na matumaini aliyokuwa nayo ya kutetea ubingwa huo mapema, lakini kazi haikuwa rahisi. Alisema taji hilo litawaongezea ari watakaporudi kwenye mechi za Ligi Kuu, wakianzia na mchezo wao wa ugenini dhidi ya Majimaji ya Songea utakaofanyika wiki hii.

Katika michuano hiyo Azam FC, walizawadiwa medali za dhahabu na Kombe pamoja na kitita cha Sh milioni 10 wakati washindi wa pili URA ya Uganda walipata medali za fedha na Sh milioni 5. Mchezaji bora wa mashindano hayo ni Shafik Batambuze wa Singida United alizawadiwa Sh milioni 1 na Feisali Salum wa JKU alikuwa mchezaji bora chipukizi.