Azam hao waifuata Majimaji

BAADA ya kufanikiwa kubeba ubingwa wa Kombe la Mapinduzi, Azam FC leo inakwenda Songea kuifuata Majimaji kwa ajili ya mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara Alhamisi.

Msemaji wa mabingwa hao wa Kombe la Mapinduzi mara mbili mfululizo, Jaffar Idd alisema wachezaji wako katika hali nzuri, hivyo kilichobaki ni kwenda kupambana na kuvuna alama tatu muhimu.

Alisema kikosi ni kilekile kilichocheza katika mchezo wa fainali dhidi ya URA, hivyo hakutakuwa na mabadiliko na kusisitiza watajitahidi kucheza vyema ili kupata ushindi. “Tunaondoka kesho (leo) nafikiri hata hivyo tumechelewa maana mechi ni Alhamisi, lakini wachezaji wapo katika hali nzuri kikosi ni kilekile tu kwahiyo tutapambana kupata ushindi,” alisema Idd.

Alisema wachezaji hawatakiwi kuchoka kwani mpira ndio kazi yao, hivyo wanatakiwa kujipima na kuibuka na pointi zote tatu. Mbali na kucheza na Majimaji kuanzia saa 8:00 Mchana, Azam pia itacheza mchezo mwingine Nyanda za Juu Kusini, ambapo itakwaana na Tanzania Prisons ya Mbeya Januari 22 kuanzia saa 10:00 Jioni.

Azam inashika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu ikiwa na alama 26 sawa na vinara, Simba walio juu kwa wastani wao mzuri wa mabao. Kikosi hicho kitaendelea kumkosa mchezaji wake, Mbaraka Yusuph ambaye ni majeruhi na ataungana na timu itakaporejea kutoka katika mkoani Ruvuma na Mbeya.