Yanga kibaruani leo Taifa

MABINGWA watetezi Tanzania Bara Yanga wana kibarua kizito cha kusaka ushindi katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Ruvu Shooting utakaochezwa kwenye dimba la Taifa.

Mara ya mwisho zilikutana katika mchezo wa kirafiki wa maandalizi ya ligi kwenye Uwanja wa Azam Complex Chamazi, ambapo Yanga ilifungwa bao 1-0. Timu zote zimetoka kupata matokeo mabovu katika michezo iliyopita, Yanga ikilazimishwa sare ya 0-0 kwenye Uwanja wa Uhuru dhidi ya Mwadui, huku Ruvu Shooting ikichapwa na Stand United bao 1-0.

Mchezo wa leo ni mgumu kwa kila mmoja, Yanga itacheza kwa presha ikijua wazi kuwa kama itapoteza itazidi kushuka katika nafasi iliyopo na kupoteza imani yake ya kutetea taji na kadhalika, Ruvu iko kwenye mstari wa kushuka daraja ikifungwa hali itakuwa mbaya zaidi.

Yanga ina pointi 23 na kabla ya michezo ya jana ilikuwa ikishika nafasi ya tano kwenye msimamo wa ligi. Kushuka kwake kunategemea na matokeo ya jana kati ya Tanzania Prisons dhidi ya Azam FC.

Siyo tu itashuka kama itafungwa au kupata sare, bali itazidi kuachwa mbali dhidi ya wanaoongoza, kwa maana ya Simba yenye pointi 29, Azam 27, Mtibwa 24 na Singida 23 ambazo pointi zao zilitarajiwa kupanda baada ya michezo ya jana.

Ruvu Shooting siyo timu ya kudharau na kwa sababu hiyo ni lazima itapambana siyo tu kupata matokeo mazuri bali inajua inakutana na mabingwa watetezi itajitahidi ili kuiadhibu.

Pointi 11 walizonazo hazitoshi kuwapa nafasi ya kujiachia, ni dhahiri wako kwenye presha ya kutafuta matokeo mazuri na kujiondoa kwenye hatari waliyopo. Yanga inakabiliwa na wachezaji majeruhi akiwemo Donald Ngoma, Thaban Kamusoko, Abdallah Shaibu ‘Ninja’ na Geofrey Mwashiuya waliokosa mchezo uliopita.