Azam, Yanga ni patashika

KIKOSI cha Azam FC, ambacho kipo chini ya kocha Mromania, Aristica Ciaoba, leo kitawakabili mabingwa watetezi Yanga, katika mwendelezo wa mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara.

Mchezo huo umepangwa kupigwa kwenye uwanja wa Azam Complex Chamazi ambako ni nyumbani kwa Azam FC, umepangwa kuanza majira ya saa 10:00 jioni. Hiyo ni mara ya kwanza kwa timu hizo kukutana msimu huu, na kila upande umejitapa kushinda mchezo huo ili kujiweka katika nafasi nzuri kwenye msimamo wa ligi hiyo inayoshirikisha timu 16.

Wenyeji Azam wapo katika nafasi ya pili kwenye msimamo wakiwa na pointi 30, na wataingia kwenye mchezo huo kwa nguvu kubwa baada ya ushindi wa mabao 2-0, walioupata Jumapili iliyopita dhidi ya Tanzania Prisons kwenye Uwanja wa Sokoine, Mbeya.

Mbali na ushindi huo, lakini Cioaba, atakuwa anafurahia kurejea wa washambuliaji wake wawili, Mbaraka Yusufu na Wazir Junior waliokosa mechi za Kanda ya Ziwa kutokana na majeruhi, huku pia safu yake ya ulinzi ikizidi kuimarika baada ya beki Mghana Daniel Amoah kurejea kikosini.

“Naiheshimu Yanga kwa sababu ni timu kubwa yenye historia nzuri na ndiyo mabingwa watetezi, lakini mchezo wa kesho tumejipanga kuhakikisha tunachukua pointi zote tatu,” alisema na kuongeza: “Nafurahi maandalizi yetu yanakwenda vizuri na wachezaji wote wapo fiti kwa ajili ya mchezo huo ambao tumepania kuonesha ubora na dhamira yetu ya kutaka ubingwa,” alisema Cioaba.

Kwa mupande wao Yanga kupitia kwa kocha wao mkuu George Lwandamina, amesema mchezo utakuwa mgumu, lakini lengo lao ni kuhakikisha wanashinda ili kuzidi kuzikimbiza Simba na Azam zilizopo juu yao.

Lwandamina alisema wachezaji wake wote wapo vizuri na wana usubiri kwa hamu mchezo huo baada ya kufanya mazoezi makali wiki hii kwenye Uwanja wa Uhuru Dar es Salaam.

Lwandamina atamkosa kiungo mshambuliaji Pius Buswita, lakini ameonekana kuwa na furaha baada ya kurejea kwa mshambuliaji wake anayeongoza kwa mabao Obrey Chirwa, aliyemaliza adhabu yake ya kufungiwa mechi tatu na beki Kelvin Yondani ambaye alikosa mechi iliyopita baada ya kuwa na kadi tatu za njano.

“Tumejipanga kuhakikisha hatupotezi pointi nyingine najua presha ni kubwa, lakini kitu cha msingi kwetu ni pointi tatu ili kurudisha matumaini ya ubingwa kwa mashabiki wetu,” alisema Lwandamina.

Kocha huyo huenda leo akaendelea kutokuwepo katika benchi la Yanga na akakaa jukwaani endapo Yanga watakuwa hawajafanikiwa kupata kibali chake cha kikazi. Wenyeji Azam wanahitaji ushindi ili kuendelea kuifukuza Simba iliyopo kileleni wakitofautiana kwa pointi mbili na kama ikishinda itaongoza ligi, huku ikisikilizia mchezo wa Jumapili kati ya Simba na Majimaji.

Kwa upande wa Yanga yenye pointi 25, inahitaji ushindi ili kuisogelea Azam wanayotofautiana nayo pointi tano na kuzikimbia timu za Mtibwa Sugar na Singida United, ambazo wanatofautiana nazo kwa wastani wa pointi moja na magoli ya kufunga.

Mchezo huo utachezeshwa na mwamuzi Israel Nkongo, ambaye tayari pande zote mbili zimeonesha kutokuwa na imani naye kufuatia matukio mbalimbali mabaya wakati akizichezesha timu hizo hasa ile ya Machi 13 msimu wa 2011/13, ambapo wachezaji wa Yanga walilazimika kumrushia ngumi wakimtuhumu mwamuzi huyo kuipendelea Azam, ambayo kwenye mchezo huo iliibuka na ushindi wa mabao 3-1.

Msemaji wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Clifford Ndimbo alisema jana kuwa hakuna mabadiliko yoyote kwani malalamiko hayo nao wanayaona katika mitandao. Alisema kuwa hakuna timu yoyote kati ya Azam na Yanga iliyowasilisha kwao malalamiko kuhusu mwamuzi Nkongo.

“Mpaka mwamuzi anapangwa anakuwa ameshafanyiwa uchungzi na kuonekana anafaa kwa mechi husika ikitokea mwamuzi anabadilishwa siyo sababu klabu fulani imesema ila ni kwa sababu zao TFF au Bodi ya Ligi au ile ya Waamuzi,” alisisitiza Ndimbo.