Zari atangaza kuachana na Diamond

MAMA wa watoto wa mwanamuziki maarufu wa muziki wa kizazi kipya, Naseeb Abdul 'Diamond Platinumz', Zarina Hassan ‘Zari’ ametangaza kuachana na msanii huyo.

Zari ambaye amezaa watoto wawili na Diamond, amewatangazia mashabiki wake kuachana na Diamond kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Instagram.

Alisema sababu ya kuamua kuchana na Diamond ni matukio mfululizo ya usaliti wa kimapenzi.

Licha ya kuwa na Zari, lakini mara kadhaa Diamond amekuwa akikumbwa na kashfa za kutoka kimapenzi na wasichana wengine akiwemo Video Queen Tunda, na mwezi uliopita kuna msichana alisambaza picha ya video inayomuonyesha yuko Madale nyumbani kwa msanii huyo na alipoulizwa alidai kuitwa na kulala na msanii huyo.

Mwaka jana aliingia kwenye kashfa ya kuzaa na mwanamitindo Hamisa Mobeto mtoto wa kiume, Abdul kabla ya kufikishana mahakamani kwa ajili ya matunzo ya mtoto huyo ambapo Diamond aliamuliwa kutoa fedha kila mwezi.

Kana kwamba haitoshi, mwishoni mwa mwezi uliopita, Diamond alionekana na mpenzi wake wa muda mrefu Miss Tanzania 2006 Wema Sepetu katika hafla ya kumtambulisha msanii mpya wa WCB Maromboso.

Licha ya wawili hao kukanusha kwamba hawajarudiana, lakini mikao yao kwenye hafla hiyo ilizua maswali mengi. Zari aliandika ujumbe mrefu kwenye ukurasa wake juzi na kuweka wazi sababu za kuamua kuachana na nyota huyo aliyezaa nae watoto wawili, Latifa na Nillan.

“Elewa hiki ni kitu kigumu sana kwangu kukifanya, kumekuwa na tetesi mbalimbali baadhi kati ya hizo zimekuwa na ushahidi ambao umekuwa ukisambaa katika vyombo vya habari kuhusiana na usaliti wa kimapenzi unaofanywa na Diamond, kwa huzuni nimeamua kuvunja uhusiano wangu wa kimapenzi na Diamond kwa heshima yangu”.

“Tunaachana kama wapenzi lakini sio kama wazazi hii hainipunguzii mimi kuwa mtu wa kujitegemea, mama mwenye kujali na Boss Lady, wote mnatakiwa kufahamu hilo nitaendelea kujijenga kama mwanamke mwenye ushawishi, nitawahamasisha wanawake wote duniani kuwa maboss Ladies,”

“Nitawafundisha watoto wangu wanne wa kiume kuwaheshimu wanawake na nitamfundisha binti yangu ni nini maana ya heshima, nimekuwa katika kiwanda cha burudani kwa miaka 12 sasa pamoja na changamoto zote hizo lakini nimefanikiwa kuwa mshindi kwa sababu mimi ni mshindi nawatakiwa wote siku njema ya wapendanao,” aliandika Zari.

Baada ya ujumbe huo, mashabiki wa wawili hao walitoa maoni yao, wengine wakisikitika na wengine wakifurahi. Aidha mpaka jana mchana, Diamond hakuzungumza chochote kuhusu jambo hilo na waandishi wa gazeti hili walimsaka bila mafanikio.

Kadhalika msanii huyo ambaye pia hupenda kutumia mitandao ya kijamii kuzungumzia masuala yake mbalimbali, jana hakuandika chochoe kuhusu tukio hilo na mpenzi wake huyo raia wa Uganda, zaidi ya kupost vitu vingine ikiwemo taarifa ya kundi lake la WCB kufungua tawi lingine Nairobi, Kenya kwa ajili ya kuendeleza vipaji.