Hukumu ya Masogange Februari 21

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu Februari 21 mwaka huu imepanga kutoa hukumu katika kesi ya dawa za kulevya inayomkabili Malkia wa video (video Queen), Agnes Gerald ‘Masogange’.

Hatua hiyo imekuja baada ya mshitakiwa Masogange kujitetea mwenyewe jana mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri kutokana na upande wa mashitaka uliokuwa ukiongozwa na Wakili, Constantine Kakula kufunga ushahidi wake baada ya mashahidi watatu kutoa ushahidi dhidi yake.

Akiongozwa na Mawakili wa utetezi, Nehemiah Nkoko na Ruben Simwanza, Masogange alidai kuwa hajawahi kutumia dawa za kulevya hata siku moja na kwamba mahakama imuachie huru kwa sababu hana kosa lolote.

Masogange ambaye alidai licha ya usanii, alikuwa mfanyabiashara wa nguo na kwamba Februari 14 mwaka huu Polisi walikwenda nyumbani kwake bila yeye kuwapo kwa sababu alikuwa amempeleka mjomba wake Orca deco kununua vitu hivyo walimkuta dada yake.

Alidai kuwa polisi hao walimweka chini ya ulinzi dada yake na kumtaka ampigie simu ajifanye anaumwa ili arudi nyumbani.

Masogange alieleza kuwa dada yake alimpigia simu na kumweleza kuwa anaumwa sana, naye akamjulisha kuwa atarejea nyumbani muda mchache kutoka saa hiyo alipopigiwa simu na kufika nyumbani saa 12:00 jioni.

“Nilipofika nyumbani kwangu getini kabla sijashuka kwenye gari, nilimuona mlinzi amekaa na watu wanne, niliwasalimia na kuingia ndani. Nilipofika ndani nilimkuta dada yangu, askari wa kike na askari wawili wa kiume, ambao waliniambia kuwa wananisubiri mimi na walijitambulisha kuwa wao ni polisi,’’ alidai Masogange.

Masogange alidai kuwa aliwauliza shida yao na walimweleza wamekwenda kufanya upekuzi, lakini hawakupata kitu chochote.

Alidai kuwa baada ya upekuzi huo, walimchukua na kupeleka Kituo Kikuu cha Polisi na walipofika mapokezi akaandikisha jina na wakampeleka rumande ambako alikaa siku tisa.

Alidai baada ya kukamatwa Februari 14, mwaka jana , siku iliyofuata akiwa polisi alipelekwa katika ofisi iliyokuwa na watu 15, ambako kwa nyakati tofauti walikuwa wakimuuliza maswali.

Masogange anakabiliwa na kesi ya kutumia dawa za kulevya aina ya Heroin na Oxazepam ambapo anadaiwa kuwa kati ya Februari 7 na 14 mwaka jana katika maeneo yasiyojulikana ndani ya jiji la Dar es Salaam alitumia dawa za kulevya aina ya Heroin (Diacety Imophine).

Pia anadaiwa kuwa kati ya Februari 7 na 14, mwaka huo huo alitumia dawa za kulevya aina ya Oxazepam.