Maromboso asema hashindani na Aslay

MSANII wa muziki wa Bongo fleva, Mbwana Kilungi,Maromboso, amesema hana mpango wa kushindana na Asley Isihaka katika kufanya muziki bali anaheshimu anachokifanya.

Akizungumza na gazeti hili jana, Maromboso alisema, mashabiki wanamchukulia kuwa amekuja kwenye muziki huo kuleta ushindani kwa Aslay kitu ambacho hajafikiria.

“Naheshimu muziki wa Aslay kwa sababu ni mtu ambaye nimemkuta kwenye tasnia pia ni kaka yangu tunaheshimiana na namheshimu sana,” alisema Mbosso.

Maromboso na Aslay walikuwa pamoja katika kundi la Ya moto kabla ya kusambaratika ambapo Aslay aliamua kusimama mwenyewe na Maromboso kusajiliwa na kundi la WCB chini ya Naseeb Abdul, Diamond.

Wengine waliotoka kwenye kundi hilo na kufanya kazi zao wenyewe ni Beka Flavour na Enock Bella.

Hata hivyo katika wasanii hao, Aslay ndiye anayeonekana kuwa juu zaidi kwa kujizolea mashabiki baada ya kutoa nyimbo zaidi ya 15 mpaka sasa.

Beka ametoa nyimbo nne mpaka sasa, Bella ana nyimbo mbili na Maromboso ndio ameingiza wimbo wake wa kwanza sokoni, Watakubali.