Mwadui yazungumzia ilivyoibana Simba

BAADA ya Mwadui kupata sare ya mabao 2-2 dhidi ya vinara wa Ligi Kuu, Simba, katikati ya wiki hii, nahodha wa timu hiyo Awadh Juma amesema waliisoma Simba kipindi cha kwanza na kujua wapi pa kuwashika.

Mwadui imekuwa ya kwanza kuitibulia Simba kwa kupata sare hiyo baada ya wekundu hao wa Msimbazi kushinda mfululizo takriban mechi tano. Mabao yote hayo Simba ndio ilianza kufunga kabla Mwadui haijachomoa.

Mwadui walionekana kucheza mpira wa kasi na kujituma muda wote huku ikionekana kuhitaji kupata matokeo ya ushindi kiasi kilisababisha Simba kupotea eneo la kati pamoja na kupoteza mipira mara kwa mara.

Nahodha huyo alisema kipindi cha kwanza walikuwa wakiwasoma Simba ili wafahamu sehemu muhimu za kuwakamata vinara hao kisha waanze kupambana, ingawa waliambulia sare.

"Ujue sisi tulikuwa tunawasoma dakika 45 za mwanzo ndo maana umeona kipindi cha pili tumerudi kwa kasi," alisema.

Aliongeza, kitendo cha mwamuzi wa mchezo huo kutoa kadi nyingi za njano,huenda zikawagharimu kwa namna tofauti kutokana na michezo migumu iliyopo mbele yao.

"Kadi zitatugharimu sana, mbele kuna michezo migumu, unakuta mchezaji amepata kadi kizembe halafu ni muhimu na anahitajika kwenye michezo mingine sasa anapokosekana kwa adhabu ya kadi hapo ndio inatugharimu,” alisema.