Yanga, Simba mguu sawa kimataifa

SAFARI ya wawakilishi wa Tanzania kimataifa, Yanga na Simba ni leo kwenda kutafuta ushindi katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho Afrika.

Yanga inasafiri kwenda Shelisheli kucheza mechi ya marudiano dhidi ya St. Louis ya huko ikiwa na wachezaji 20 na viongozi 10, kati ya hao benchi la ufundi wanane na wajumbe wawili wa Kamati ya Utendaji.

Katika mchezo huo wa marudiano utakaochezwa Jumatano ya wiki ijayo, Yanga itamkosa mshambuliaji wake tegemeo, Obrey Chirwa aliyedaiwa kupata maumivu ya misuli kwenye mechi iliyopita ya ligi dhidi ya Majimaji.

Wengine watakaobaki ni Amis Tambwe, Donald Ngoma, Yohana Nkomola na Abdallah Shaibu ‘Ninja’.

Kwa mujibu wa Ofisa Habari wa Yanga, Dismas Ten watakaosafiri ni Ramadhan Kabwili, Beno Kakolanya, Youthe Rostand, Hassan Kessy, Juma Abdul, Mwinyi Haji, Gadiel Michael, Nadir Haroub, Pato Ngonyani, Kelvin Yondani, Said Juma, Papy Tshishimbi, Pius Buswita, Raphael Daud, Yusuf Mhilu, Ibrahim Ajibu, Said Mussa, Emmanuel Martin, Geofrey Mwashiuya na Juma Mahadhi.

Mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu soka Tanzania Bara wanatarajia kucheza mchezo huo wa ugenini wakihitaji sare yoyote baada ya kushinda bao 1-0 katika mechi iliyochezwa nyumbani wiki iliyopita. Yanga ikiitoa timu hiyo itacheza na mshindi kati ya Al Merrikh ya Sudan au Township Rollers ya Botswana katika raundi inayofuata.

Katika mechi ya awali Rollers ilishinda mabao 3-0.

Akizungumzia safari hiyo, Ten alisema kikosi kilifanya mazoezi ya mwisho jana na kiko tayari kwa safari hiyo ya Shelisheli. “Tumefanya maandalizi yote kuhakikisha tunakwenda kupambana na kupata ushindi utakaotuwezesha kusonga mbele,” alisema.

Kwa upande wa vinara wa Ligi Kuu Bara, Simba, pia itasafiri na wachezaji 20 ikibakiza majeruhi akiwemo Jamali Mwambeleko, Juma Luizio, Salim Mbonde, Said Nduda na Haruna Niyonzima ambao walishaanza mazoezi mepesi.

Simba inatarajia kucheza mchezo wa marudiano dhidi ya Gendarmerie ya Djibout keshokutwa ikiwa na matumaini makubwa ya kusonga mbele baada ya mchezo wa kwanza kushinda 4-0 kwenye Uwanja wa Taifa.

Ikisonga mbele itakutana na mshindi kati ya Al Masri ya Misri na Buffaloes ya Zimbabwe. Katika mechi ya kwanza, Masri ilishinda mabao 4-0 kwenye uwanja wa nyumbani na hivyo kufanya mechi yao kuwa nyepesi.

Msemaji wa Simba, Haji Manara alisema kikosi chao kipo imara akiwemo nahodha John Bocco aliyeumia kifundo cha mguu walipocheza na Mwadui, Alhamisi ya wiki hii.