Arsenal kujenga kituo cha soka Uganda

MIAMBA ya Ligi Kuu England, Arsenal inajiandaa kufanya ziara Uganda Juni mwakani, ikiwa ni sehemu ya mradi wa utalii michezoni, kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Baraza la Michezo la Taifa (NCS), Bosco Onyik.

Kiongozi huyo amethibitisha mpango huo uko katika hatua za mwisho na kwamba, The Gunners watatoa ofa kwa makocha wa Uganda kwa kuwekeza katika vifaa vya mazoezi kwa taifa hilo la Afrika Mashariki.

"Tulikwenda London mwezi uliopita Januari 16 na kufanya vikao vitatu na uongozi wa Arsenal FC wenye lengo la kujenga urafiki nao,” Onyik aliiambia Xinhua.

"Tulikubaliana kwamba watafundisha baadhi ya makocha wetu, wataipa Uganda Cranes nafasi ya kufanya mazoezi uwanja wa Emirates London, kujenga kituo cha soka na pia timu yao itutembelee mwakani Juni na kucheza baadhi ya mechi”.

Chanzo hicho cha habari kutoka China kilisema Waziri wa Michezo, Charles Bakkabulindi, amethibitisha kwamba maelezo zaidi na kuhusu mkandarasi atakayejenga kituo hicho vitakuwa wazi Machi.

"Kuwa na kituo kikubwa na kizuri Uganda kutasaidia maendeleo ya soka nchini,” alisema Bakkabulindi.

"Makocha wetu kufundishwa kutawasaidia kuendeleza mchezo huo nchini,” alisema.

"Mpira wa miguu ni mchezo mkubwa na wenye soko na hiyo inaelezea kwanini tumefikiria kuwa na urafiki na timu hiyo kubwa”.