Real Madrid yamtaka Hazard kwa gharama yoyote

REAL Madrid inajiandaa kumtoa Gareth Bale pamoja na pauni milioni 100 katika harakati zake za kumnasa mchezaji wa Chelsea, Eden Hazard.

Vigogo hao wa soka wa Hispania wamemuweka Hazard kuwa chaguo lao namba moja katika usajili katika kipindi cha majira ya joto.

Hazard yuko mbioni kusaini mkataba mpya na klabu yake hiyo yenye maskani yake Stamford Bridge, wakati ikijulikana kuwa mchezaji huyo anataka kuhamia Real Madrid.

Vigogo hao wa Hispania wanajiandaa kubomoa kikosi chao baada ya kuwa pointi 20 nyuma ya Barcelona msimu huu.

Pia timu hiyo iko mbioni kuachana na kocha wake, Zinedine Zidane, ambaye Hazard anapenda kufanya kazi naye.

Manchester United inamtaka Bale kwa msimu miwili iliyopita lakini klabu yake ya zamani ya Tottenham inamhitaji pia mchezaji huyo endapo klabu kubwa kiuchumi zitashindwa kumnasa.

United sasa inaonekana haina tena hamu ya kumfukuzia Bale baada ya kumsajili Alexis Sanchez kutoka Arsenal mwezi uliopita.

Novemba mwaka jana, Hazard aliiambia televisheni ya Ufaransa ya Canal: "Kila mmoja anajua nia iko kwenda Real, lakini kwa sasa niko Chelsea.”