Yanga yaipumulia Simba

MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga wameendelea kupeleka presha kwa Simba baada ya jana kuibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Kagera Sugar katika mchezo uliofanyika kwenye Uwanja wa Taifa Jijini Dar es Salaam.

Kwa matokeo hayo, Yanga imerejea katika nafasi ya pili na kuendelea kumfukuza mnyama kimya kimya kwa kufikisha pointi 43 ikizidiwa pointi tatu na Simba huku kila timu ikiwa imeshuka dimbani mara 20. Jadi kipindi cha kwanza kinamalizika, timu hizo zilikuwa suluhu na kuwafanya mashabiki wa Yanga kuwa na hofu wakihofia timu yao huenda ikalazimishwa sare.

Kipindi cha pili kilikuwa na neema kwa Yanga, ambapo mnamo dakika ya 53, Ibrahim Ajibu alifunga bao la kwanza kwa njia ya penalti, baada ya beki mmoja wa Kagera Sugar kuunawa mpira katika eneo la hatari. Yanga iliendeleza makali katika kipindi cha pili na katika dakika ya 77 ya mchezo huo, 77, Emmanue Martin alifunga bao la pili baada ya kupata pasi ya Chirwa na kufanya timu hiyo kuwa mbele kwa mabao 2-0.

Kazi nzuri ya Mhilu ilizidi kuzaa matunda tena, ambapo katika dakika ya 88, Godfrey Taita alijifunga, kufuatia kazi nzuri ya Mhilu aliyepiga shuti kali lilisababisha mchezaji huyo wa Kagera kujifunga. Yanga sasa ina pointi 43 ikiwa nafasi ya pili, huku Simba ina alama 46, na Azam imeshuka hadi nafasi ya tatu ikiwa na alama zake 41. Yanga imeibuka na ushindi huo baada ya Jumanne kupokea kichapo cha mabao 2-1 kutoka kwa Township Rollers ya Botswana katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa wa Afrika kwenye Uwanja wa Taifa.