46 msijisahaulishe

MBIO za kutwaa taji la Ligi Kuu zimezidi kunoga baada ya mabingwa watetezi Yanga kushinda mabao 3-1 dhidi ya Stand United jana.

Katika mechi hiyo iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam, Yanga ilitawala katika kipindi chote cha kwanza na ndipo ilipopata mabao hayo mawili. Matokeo hayo yanaifanya Yanga kufikisha pointi 46 sawa na vinara Simba wanaoongoza kwa uwiano mzuri wa mabao wakiwa na mechi moja kibindoni. Simba sasa italazimika kushinda mechi yake ijayo inayotarajiwa kuchezwa wiki ijayo.

Yanga ilipata bao la kuongoza katika dakika ya sita likifungwa na Yusuph Mhilu aliyeunganisha mpira wa krosi kabla ya mpira kumgonga beki wa Stand United na kujaa wavuni. Dakika sita baadaye Ibrahim Ajibu alifunga bao la pili baada ya kupewa pasi na Gadiel Michael kabla ya kuujaza mpira wavuni. Kipindi hicho cha kwanza Yanga walimiliki mpira kwenye idara zote na Stand United wakionekana ‘kutii’ kila wanachotaka mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu.

Kipindi cha pili, Stand walibadilika na kufanya mashambulizi ya mara kwa mara hali iliyowafanya wachezaji wa Yanga kurudi nyuma muda mwingi na kufanya mashambulizi ya kushtukiza. Juhudi zao zilizaa matunda katika dakika ya 85 walipopata bao lililofungwa na Tariq Seif aliyemalizia vizuri krosi ya Ally Ally.

Hata hivyo, bao hilo halikudumu kwani dakika moja baadaye Obrey Chirwa aliandika bao la tatu kwa Yanga baada ya kupokea mpira mrefu wa Martin akiwa ndani ya 18 na kuachia shuti lililojaa moja kwa moja wavuni. Matokeo hayo si mazuri kwa Stand United iliyo nafasi ya 13 kwenye msimamo, kwani sasa inachungulia ukanda wa kushuka daraja na isipojitahidi katika mechi zinazofuata, safari inaweza kuwakuta.