Yanga yawaendea Waethiopia Morogoro

KLABU ya Yanga imerudisha makazi yake Morogoro kujiandaa na mchezo ujao wa kimataifa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Welaita Ditcha ya Ethiopia utakaochezwa Jumamosi.

Yanga iliyokuwa na mchezo wa Shirikisho Azam (FA) wiki iliyopita uliochezwa mkoani Singida, imetolewa kwenye michuano hiyo kwa mikwaju ya penalti 4-2 baada ya sare ya bao 1-1 ndani ya dakika 90 na hivyo, nguvu zake kubwa kwa sasa ni mchezo wa kimataifa. Ofisa Habari wa klabu hiyo, Dismas Ten aliliambia gazeti hili jana kuwa timu imeamua kusahau yaliyopita na kujikita katika maandalizi kuelekea mchezo huo.

“Tunaangalia mbele hivyo, ni lazima tusahau yaliyopita, tunashukuru Mungu timu iko Morogoro na leo (jana) ilianza mazoezi kwenye Uwanja wa Jamhuri, wachezaji wote wanaendelea vizuri kiafya,” alisema. Kocha Msaidizi wa Yanga, Shadrack Nsajigwa alisema wanajipanga kufanya vizuri katika mchezo wao ujao ikiwezekana kupigania nafasi ya kupata matokeo mazuri kwenye uwanja wa nyumbani.

Alisema walijifunza kutokana na makosa kupitia michezo iliyopita ya Ligi ya Mabingwa hivyo, hawataki yajirudie tena. “Tunahitaji kujiweka vizuri na kuhakikisha tunatumia nafasi ya uwanja wa nyumbani kupata matokeo mazuri, ni lazima tujipange vizuri na kuwaandaa wachezaji kisaikolojia,”alisema.

Yanga iliangukia katika michuano hiyo baada ya kutolewa na Township Rollers ya Botswana kwa kufungwa 2-1 nyumbani na mchezo wa marudiano kutoka sare 0-0 ugenini katika mchezo wa Ligi ya mabingwa Afrika. Wapinzani wa Yanga, Welayta Dicha walitarajiwa kuja jana, ikiwa ni mara ya pili kutua Tanzania baada ya Februari kuja dhidi ya Zimamoto ya Zanzibar na kushinda kwa jumla ya mabao 2-1, ikitoa sare ya 1-1 Uwanja wa Amaan, kabla ya kushinda 1-0 Ethiopia.