Yanga yatamba kushinda

IKIWA zimebaki saa 24 kabla miamba ya soka Tanzania, Yanga kuwavaa Welayta Dicha ya Ethiopia katika mchezo wa kufuzu hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho, Katibu Mkuu wa Yanga Charles Boniface Mkwasa amesema hawapo tayari kurudia makosa.

Hiyo ni nafasi pekee kwa Yanga ambayo awali ilikuwa ikishiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, kabla ya kutolewa na Township Rollers na kudondokea kwenye michuano hiyo ya pili kwa ukubwa katika ngazi ya klabu barani Afrika.

Akizungumza na gazeti hili, Mkwasa alisema huo ni mchezo wa kujitathmini na kuwathibitishia mashabiki wao pamoja na Watanzania kuwa waliteleza kwa kutolewa kwenye Ligi ya Mabingwa na wametambua makosa yao kwa kupata ushindi mnono mbele ya wahabeshi hao. “Tumejifunza kutokana na makosa ukweli tunajivunia maandalizi tuliyoipa timu yetu kabla ya kuwajua wapinzani wetu mchezo wa kesho tumedhamiria kuumaliza hapa hapa nyumbani kwa kushinda idadi kubwa ya mabao ili tuweze kuwa na kazi nyepesi tutakapokwenda ugenini lengo letu ni kucheza hatua ya makundi,” alisema Mkwasa.

Mkwasa alisema wanawaheshimu wapinzani wao Welayta Dicha, kutokana na rekodi yao nzuri huko walipotoka hadi kufikia hapo lakini kocha wao George Lwandamina amewahakikisha ushindi kwani hawapo tayari kuona rekodi mbaya ya kutolewa kwenye michuano hiyo inajirudia. Alisema ingawa watawakosa wachezaji wao muhimu katika mchezo huo lakini uwepo wa Donald Ngoma, Thabani Kamusoko na Amissi Tambwe pamoja na wachezaji wengine waliopo utawasaidia kuweza kupata matokeo hayo waliyokusudia na kujiwekea mazingira mazuri ya kutinga hatua ya makundi. Mkwasa aliwataka mashabiki wa Yanga kufika kwa wingi uwanjani kwa ajili ya kitimiza jukumu lao la kuishangilia na kuwapa sapoti wachezaji wao ili waweze kucheza kwa nguvu na kupata ushindi katika mchezo huo ambao ni muhimu kwao.