EDGA EDWARD: Kijana aliyegeuza mifuko ya plastiki kuwa fursa

NENO Tanzania ya Viwanda limekuwa kama nyimbo kila siku masikioni mwa watanzania kwa sasa. Ili kukamilika kwa ndoto hiyo masuala ya teknolojia yanatakiwa kupewa nafasi kubwa katika kuhakikisha kuwa dhana nzima ya Tanzania ya Viwanda inakamilika.

Tanzania ya viwanda inayotakiwa inaenda sambamba na matumizi ya nguvu kazi ya vijana viwandani ili ndoto hizo zipate kutimia. Lakini kutokana na kuwapo kwa maendeleo ya teknolojia kwa sasa katika sekta mbalimbali vijana wengi wamejikita katika matumizi ya teknolojia hiyo ili kujitimizia ndoto zao na za taifa.

Kijana Edga Edward ni mwanafunzi wa kidato cha nne katika Sekondari ya St Jude iliyopo mkoani Arusha anayechukua masomo ya mchepuo wa biashara. Edga amebuni mradi wa kiteknolojia unaolenga kukabiliana na taka ngumu kwa kuzibadilisha na kuzitumia kutengenezea matofali madogo.

Kijana huyu amebuni mashine ambayo inatumika kutengenezea matofali hayo ambayo inatumia moto wa gesi kuyachoma. Anasema alianza kutengeneza mashine hiyo miaka miwili iliyopita akiwa shuleni hapo na alikuwa akionesha shuleni kuonesha kipaji chake na anaongeza kuwa wazo la kuanzisha mradi huo lilikuja kufuatia kuwapo kwa kanuni inayokataza matumizi ya mifuko ya lailoni kutokana na athari ya mifuko hiyo katika uharibifu wa mazingira.

Edga anasema aliposikia agizo hilo la serikali kwa upande wake aliamua kutafakari ufumbuzi na kuumiza kichwa wakati huo akiwa kidato cha pili na ndipo alipokuja na wazo la utengenezaji wa matofali kutokana na mifuko hiyo.

“Nafahamu sayansi ni kuchukua changamoto na kuifanyia kazi ili ilete tija… hicho ndio nimeamua kukifanya,” anasema kijana huyo na kuongeza kuwa, “ niliona kuwa ninaweza kutengeneza matofali kutokna na mifuko hiyo ambayo imekuwa ikitupwa na imekuwa mingine ikiachwa kama takataka na kwa sasa inaweza kuwa tofali dogo,” anasema.

Anafafanua kuwa akiichukua mifuko hiyo anaikatakata na kisha kuiweka kwenye mashine yake hiyo na kisha kuichoma, kisha anaichoma kwa kutumia mashine yake hiyo ambayo inakuwa imeunganishwa na moto wa gesi na halafu anaichoma kwa muda mrefu kabla ya kuja kupatikana kwa tofali dogo.

Edga anasema akishamaliza kuichom, kwa kuwa anakuwa ameiunganisha na malighafi nyingine ikitoka inakuwa imeshakamilika na kuwa ni tofali.

Anaweka wazi kuwa tofali hilo linakuwa sio kama yale ya kujengea nyumba ambayo yamezoeleka kuwa ni makubwa na yenye kutumia saruji, ila matofali hayo ni madogomadogo ambayo yanatumiwa kwenye sehemu za kuegeshea magari.

Anasema tofali hizi hutumika kwa kuvitandaza kwenye viwanja vya nje majumbani au katika sehemu za wazi kubwa na unakuta tofali ndogo ndogo zinapangwa chini ili kuzuia mchanga kwenye eneo husika.

Edga anasema malighafi anayotumia kuchanganya na mifuko hiyo ni mchanga ili kutengeneza matofali hayo na hivyo anakuwa ameyajengea nguvu na uimara zaidi ili kumudu vitu vizito.

Anaweka wazi pia kuwa matofali hayo yanaweza kuziepusha nyumba dhidi na majanga mbalimbali ya asili kama vile tetemeko la ardhi na mafuriko. Anasema kama wahusika wakiamua kujengea matofali hayo anayatoboa katikati na kisha anaingiza chuma , hivyo kama likitokea janga nyumba sio rahisi kuanguka yote.

Kijana huyo anasema changamoto zinazoikabili kazi yake hiyo ni mtaji, jambo ambalo limekuwa likirudisha nyuma harakati zake hizo. “Nashindwa kuchukua zabuni kubwa kutoka kwa wateja kwa kuwa nashindwa kuzitekeleza, mtaji wangu sio mkubwa kuniwezesha kumudu zabuni hizo,” anasema kijana huyo.

Anasisitiza kuwa mashine anayoitumia inatumia mfumo wa gesi na hivyo inakuwa ni vigumu kwake kutengeneza matofali mengi na kuongeza kuwa anatakiwa kutumia mashine kama zile za viwandani ambazo zinakuwa zimeunganishwa na umeme na zina uwezo wa kuchoma tofali pange zote.

Edga anasema mashine hizo zinauzwa bei na yeye bado ni mwanafunzi anatakiwa pia kuendelea na masomo kwa hiyo itakuwa ni ngumu kuwekeza kwenye biashara yake hiyo.

"Najua ili kazi iwe kazi imara kunatakiwa pia kuwapo kwa teknolojia zaidi, nilifanikiwa kutengeneza mashine ya kufanyia kazi hii lakini sasa, ili mashine hiyo ifanye kazi ni lazima iunganishwe na umeme na mimi nimeunganisha na gesi. “

Iwapo hilo likikamilika kwa upande mmoja naweza kutumia mifuko ya plastiki inayotupwa na hata magunia ili kuimarisha zaidi ufanisi katika kazi hiyo ya kutengeneza matofali kwa kutumia mifuko,” anasema.

Edga ni mtoto wa pili kuzaliwa kwenye familia ya watoto wawili ambapo ana mdogo wake aitwae, Clara baba yake ni Mzee Edmund na mama yake anaitwa Scola. Wazo hilo la Edga pia limeendelezwa na Kampuni ya Inspire ambayo kwa kiasi kikubwa imekuwa ikichukua mawazo ya vijana ya kibunifu na kisha kuyaendeleza.

Edward Lidiko ambaye ni Mkurugenzi wa kampuni ya Inspire anasema kuwa iliona kazi ya kijana huyo na wamekuwa wakimrikisha kwenye matamasha mbalimbali ambapo wiki hii alikuwa mmoja kati ya vijana walioshiriki katika kongamano la Bits & Bytes lililolenga kuhamasisha mawazo ya kibunifu ya kisayansi katika kuchochea maendeleo katika jamii.