REBECA GYUMI Binti aliyejitolea kutetea haki ya msichana

KWA macho unaweza kumtafsiri kuwa ni binti mdogo, mpole asiyekuwa na uwezo wa kuzungumza mbele za watu, lakini kijana huyu amegeuka kuwa jasiri katika kusimamia na kutetea haki ya wasichana na vijana. Anaitwa Rebeca Gyumi (30) mzaliwa wa Mkoa wa Dodoma ingawa wazazi wake ni wenyeji wa Mkoa wa Singida.

Rebeca amesoma Dodoma darasa la kwanza hadi kidato cha nne katika shule za serikali na baadaye kwenda kidato cha tano na sita mkoani Morogoro katika shule ya Sekondari ya Kilakala kabla ya kujiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

Rebeca pamoja na umri wake kuwa ni wa kati, ni Mkurugenzi wa shirika lisilo la kiserikali la Msichana Initiative linalotetea haki za wasichana kupata elimu. Hivi karibuni kijana huyo wa kike ametunukiwa Tuzo ya Malkia wa Nguvu, shindano lililokuwa likiendeshwa na Kituo cha Redio na Televisheni cha Clouds ambao walitambua mchango wake katika kupigania haki za mtoto wa kike na vijana.

Februari mwaka huu alipata Tuzo ya Serikali ya Marekani ambayo ilikuwa ikitolewa kwa vijana ambao wametumikia katika jamii yao kuleta mabadiliko. Mbali na hiyo jina lake kwa sasa limeingia katika kuwania nafasi ya kuwa mwakilishi wa vijana katika Umoja wa Mataifa ambapo amependekezwa pamoja na na Victoria Charles.

Kubwa zaidi Rebeca ameliweka jina lake katika historia ya nchi hii na hata kufi ka mbali zaidi baada ya kusimama kutafuta haki ya wasichana wengine kwa kufungua kesi ya Kikatiba kupinga Sheria ya Ndoa ya mwaka 2002.

Katika kesi hiyo, alipinga kipengele cha 13 na 17 ambavyo vinaruhusu watoto wa kike kuolewa wakiwa na umri wa miaka 14 kwa ridhaa ya Mahakama na pia kuruhusu kuolewa na umri wa miaka 15 kwa ridhaa ya mzazi.

Sheria hiyo ni kinyume na ibara ya 12, 13 na 18 ya Katiba ya nchi ya mwaka 1977. Historia yake Rebeca alizaliwa mwaka 1986 mkoani Dodoma, akiwa ni mtoto wa tatu kati ya watoto watano akitanguliwa na kaka zake wawili na kufuatiwa na wadogo wa wawili wa kike.

Alijiunga na Shule ya Msingi Dodoma na pia Sekondari ya Kata ya Kikuyu kabla hajajiunga na Sekondari ya Wasichana ya Kilakala. Mwaka 2008 hadi 2012 alisoma sheria ingawa wakati akiwa mdogo alitamani kutimiza ndoto ya baba yake ambaye alipenda mtoto wake huyo awe daktari.

“Mimi nimekulia katika familia ya kawaida kabisa ya kitanzania, Baba alikua amestaafu wakati mimi nakua, na mama anafanya biashara ndogondogo sokoni, na wakati mwingine anauza chakula kwenye maofi si,” anasema.

Anasema anakumbuka maisha ya sekondari alijifunza mambo mengi: “nilikuwa najitahidi sana shuleni katika masomo yangu na mimi nilikuwa ni mwanafunzi ambaye nilikuwa nikifanya vizuri sana katika Mkoa wa Dodoma.”

Rebecca anasema wakati huo serikali ilikuwa imeanzisha sekondari za kata hivyo pamoja na kufaulu vizuri alipelekwa katika shule hiyo ya kata ingawa hakupenda kutokana na ndoto alizokuwa nazo.

Anasema akiwa shule ya msingi alikuwa anasoma kwa bidii sana kwa sababu alikuwa anatamani kwenda Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Msalato. “Kwa hiyo nilikuwa najua nikipata maksi nzuri yaani alama A nitaweza kwenda Msalato, nilipata lakini sikuchaguliwa huko na mama yangu kwa uwezo wake hakuweza kunipeleka shule ya kulipia, mama aliomba sana lakini ilishindikana nikabakia kusoma hapo,” anasema.

Anasema alipochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza katika shule ya kata akiwa amefaulu kwa alama nzuri, aliona mapungufu ya vifaa vya kuwezesha mwanafunzi kufanya vizuri lakini akapiga moyo konde na kuendelea na masomo yake.

Anasema shule aliyokuwa akisoma ilikuwa na majengo machache hivyo alihamasisha wenzake kujenga majengo ambapo hatimaye wakapata madarasa na pia maktaba wakati huo alikuwa amechaguliwa kuwa kiongozi mkuu wa wanafunzi katika shule hiyo.

“Kwa kutumia nafasi hiyo nikahamasisha wanafunzi wenzangu kujitolea ili tujenge shule yetu, kila siku asubuhi tulikuwa tunatenga muda, tunakwenda kuchota maji na kumwagilia matofali ili ujenzi uende haraka,” anasema.

Anaongeza kuwa; “nilisikia furaha sana kwamba mafanikio ya shule yalikuwa yanajumuisha mchango wangu…kuanzia hapo niligundua kuwa kazi za kujitolea zina manufaa makubwa kwa jamii na pia kwa mtu ambaye anajitolea.”

Rebecca anasema mazingira yale yalimpa akili mpya, kwamba changamoto haziwezi kuwa kubwa kuliko yeye, anaweza kukabiliana nazo na akazishinda hivyo alijitahidi sana kusoma kwa bidii.

Anasema alihitimu kidato cha nne akipata Daraja la Kwanza na hiyo ikiwa ni ya kwanza na pekee kwa shule hiyo, huko nyuma hakuna mwanafunzi aliwahi kutoka shuleni hapo na alama hiyo.