FRED NYANTORI Kutoka fundi ujenzi wa barabara hadi mpigapicha wa kimataifa

“NILIANGALIA picha zinazopigwa na wapigapicha wa hapa nyumbani tanzania nikaona ni za kawaida sana ukilinganisha na zile tunazoziona kwa mfano kwenye Televisheni za Kenya, nikaona mbona hii ni nafasi tunaiacha?” hayo ni maneno ya Fred Nyantori, mpigapicha za video maarufu nchini.

Anasema mawazo hayo yalikuwa yakizunguka ndani ya kichwa chake kila alipokuwa akiangalia televisheni za hapa nchini katika miaka ya 1990 na kumfanya aachane na taaluma yake ya ufundi mchundo aliyoisoma kwa miaka sita na kuamua kuweka maisha yake kwenye kamera tangu mwaka 1996.

Ufundi Mchundo Anasema alikuwa na mapenzi makubwa na kazi ya ufundi umeme, hivyo ilimbidi kuhamia Dar es Salaam kwa kaka yake mwingine ili ajiunge na masomo hayo, akitokea Tarime mkoani Mara alikokulia na kupata elimu ya msingi. “Wakati huo nilikuwa na mapenzi sana na masuala ya ufundi, nina kaka yangu mwingine yuko hapa Dar es Salaam nikaja kujiunga Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT, zamani Chuo cha Ufundi Dar es Salaam- Dar Technical), nikatoka darasa la saba nikajiunga hapo,” anasema Nyantori.

Kama ilivyokuwa kwa vyuo vingine vya ufundi, DIT ilitoa kozi ngazi ya Cheti katika Uhandisi (GCE) iliyoambatana na masomo mengine ya sekondari na mwisho kufanya mtihani wa taifa. Anasema alisoma chuoni hapi miaka mitatu na kufanya mtihani wa taifa huku akipata elimu ya ufundi lakini pia masomo mengine ya sekondari. Na baada ya kuhitimu na kufaulu vizuri alichaguliwa kuendelea na masomo ya ufundi mchundo katika chuo hicho kwa miaka mitatu kuanzia mwaka 1996.

“La ajabu likaja hapo sasa, nilikuwa na mapenzi ya ufundi wa umeme zaidi, lakini katika masomo ya ufundi nikapangiwa kozi ya ujenzi wa barabara, mimi ukiniuliza ujenzi wa barabara najua vizuri sana kuanzia mwanzo hadi mwisho,” anasema na kutolea mfano kuwa, alishiriki kuijenga barabara ya kwenda IPTL, Tegeta jijini Dar es Salaam yenye urefu wa kilometa 1.3 kuanzia mwanzo mpaka kuweka lami mwaka 1999.

Anasema aliifanya kazi hiyo akiwa chuoni, lakini chini ya usimaminzi wa kampuni ya Konoike ya Japan. Pamoja na kusomea utaalamu wa ujenzi wa barabara, anasisitiza aliendelea kuwa na mapenzi katika ufundi wa umeme. “Kazi ya ujenzi ina changamoto zake, ukitoka chuo uko msafi, lakini ukifika eneo la kazi unapigwa jua, vumbi ukijishika uso haufai, hii ilinifanya niichukie, pia kulikua na malalamiko ilikuwa ya kujilipia hivyo kwa kuwa aliipenda fani yake, alilazimika kuchukua fedha alizokuwa amejilimbikizia, lakini pia aliuza vitu vyake vingine alivyokuwa amejinunulia.

Hata hivyo, baada ya kufika Nairobi, kenya ambako safari ilikuwa ianze, ilishindikana na hivyo alirejea nchini. Na ili kukata kiu ya kujiendeleza, alitafuta chuo nchini ingawa hakukua na vyuo vingi vya kufundisha masuala ya kamera.

Alipata nafasi katika Taasisi ya Sanaa na Mawasiliano ya Umma (IAMCO) anakosema alikutana na walimu wazuri. “Pale ndipo nilipokuja kugundua kuwa kamera ina lugha yake, na nikaanza kuielewa, nikagundua kumbe shule ni tamu, unajifunza kuongoza, unajifunza sauti, taa, kamera yenyewe na kila kitu kinachohusika katika kupata video nzuri,” anasema na kuongeza kuwa, baada ya kuhitimu alijiunga na Kituo cha Televisheni cha EATV ikiwa ajira yake ya kwanza na akiwa mtanzania wa kwanza kwenye kampuni hiyo kazi aliyoifanya mpaka mwaka 2006 kama mtaalamu wa kamera kabla hajajiunga na kampuni ya Digital Art.

“Moja ya kazi zangu kubwa nilizozifanya hapo mwaka huo 2006 ni pamoja na kushiriki kuandaa vipindi vya washiriki wa shindano la urembo la Miss Tanzania, kuandaa maonesho ya moja kwa moja ya shindano ambayo ni kazi sana na huo ukawa ndio mwanzo wangu wa matukio ya mubashara,” anasema. Alifanya pia kazi katika Tuzo za Muziki za Kilimanjaro (Kilimanjaro Music Awards) na kutengeneza matangazo ya biashara ya kampuni kubwa.

“Baadaye nikagundua fani hii inaweza kuwa ni maisha sasa, nikatafakari nafanyaje sasa ili iweze kunipa ajira sasa, likaja wazo nitafute shule nzuri zaidi, nikasema safari hii nitajipeleka mwenyewe shule Marekani,” anasema. Anasema mwaka 2011 alijiunga na chuo kinachojulikana kama ‘New York Film Academy Universal Studios’, Hollywood huko California, Marekani kinachosifika kwa mafunzo kwa vitendo.

“Chuo hiki ndiko kitovu cha filamu duniani kilipo, kuna walimu na waongozaji wazuri wa filamu na nilijifunza utaalamu wote wa kamera. “Ikitokea huna mhariri wanakufundisha uongoze mwenyewe, sauti, taa, unakaa darasani dakika 20 muda mwingine wote unautumia kwenye vitendo… hapo ni kitovu cha upigaji picha duniani na madarasa yangu yalikuwa ni Universal Studios kwenye studio kubwa za kutengeneza filamu duniani,” anasema Nyantori.

Baada ya kumaliza mafunzo alirejea nchini na kuendeleza kampuni yake aliyoifungua kabla ya kwenda masomoni, akiandaa matangazo, kurekodi matukio mbalimbali kwa ajili ya vyombo vya habari duniani.

“Kampuni hii sasa imeniunganisha na vyombo vikubwa mbalimbali vya habari duniani, sasa hivi sijui ni televisheni gani duniani ambayo sijafanya nayo kazi, Aljazeera, BBC, CNN wote hawa naendelea kuwafanyia kazi na mwaka jana nimeanza na UBC ya Australia,” anasema. Nyantori anasema anafanya pia kazi na vituo vya televisheni vya nchi za jirani kama Kenya na Uganda kuwapigia picha za matukio mbalimbali.

Anasema miongoni mwa matukio ambayo hatayasahau ni alipochaguliwa kuwa Mwongozaji na Mwandaaji wa Tuzo ya Mwandishi Bora Afrika mwaka 2014, kazi aliyopewa na Kituo cha Habari cha Kimataifa cha CNN kinachorushwa na takribani nchi 200 duniani. Anafanya kazi pia na kampuni ya Endemol ya Afrika Kusini, watayarishaji wa shindano la Big Brother Africa (BBA) kwa miaka saba sasa.

Ni mpigapicha mahiri, anaizungumziaje filamu za hapa nchini, yaani Bongo Movie? Anasema kuna wasanii wazuri, wenye vipaji na wanaofanya vizuri ingawa hawajasomea fani hiyo, ingawa amekosoa tafsiri ya maneno yanayoandikwa kutoka Kiswahili kwenda Kiingereza, akisema yanatafsiriwa vibaya na hayaeleweki.

Huyo ndiye Fred Nyantori, aliyezaliwa miaka 41 iliyopita katika kijiji cha Nyarero, Tarime akiwa ni mtoto wa sita kati ya wanane wa baba, William Nyantori ambaye ni mkulima na mama, Esther Nyantori mfanyabiashara ndogondogo aliyekuwa anamiliki mgahawa maarufu ulioitwa Desemba kijijini Nyarero.

Alisoma Shule ya Msingi Nyarero na baadaye kuhamia shule ya Shule ya Msingi Sabasaba iliyoko Tarime mjini alikohitimu mwaka 1991. Kutoka kijijini Nyarero hadi umaarufu kimataifa, Nyantori amethibitisha kuwa juhudi katika kazi hulipa, hivyo kustahili kuwa mfano wa kuigwa na vijana wengi nchini.