MJOMBA 'PILI' HUSSEIN: Mama ‘aliyejigeuza’ mwanaume aweze kufanya kazi mgodini

KAMA si kukimbia maisha ya mateso katika ndoa yake iliyodumu kwa miaka 11, pengine leo hii asingekuwa na mafanikio aliyonayo. Amepata utajiri wa fedha na mali kutokana na uthubutu wake, baada ya kunyoosha mikono katika ndoa na kuamua kufanya kazi yoyote halali, kwa kuwa awali hakuwa amepata fursa ya kusoma kabisa.

Huyu ni Mjomba ‘Pili’ Hussein, mama ‘aliyejigeuza’ mwanaume aweze kufanyakazi mgodini. Wakati anaamua kuikimbia ndoa yake, alikuwa na umri wa miaka 21. Na kwa kuwa alikuwa na mtoto mdogo mwenye umri wa miezi sita tu, alikwenda kumwacha ‘malaika’ huyo kwa wazazi wake mkoani Singida, naye kuamua rasmi kutafuta maisha kwa staili yoyote ile.

Na baada ya miaka 39 ya uamuzi wake huo (sasa ana umri wa miaka 60), mwanamama huyo ana kitu cha kujivunia maishani, kwani haishi tena ‘kilofa’, ameyapatia maisha ingawa bado ana ndoto kali zaidi, akisema; “Ninahitaji kupata angalau Shilingi bilioni 900 tu hizi kazi niwaachie vijana.” Kilichomfikisha hapo ni uthubutu wake wa kuamua kujichanganya na wanaume katika kazi ngumu ya kuzama katika migodi ya madini adhimu ya Tanzanite, huko Mererani wilayani Simanjiro, Manyara.

Ndiyo, Aprili mwaka 1978 alitua Mererani akiwa na rafiki yake wa kike (jina tunalo). Alielezwa mambo mengi juu ya utajiri katika madini ya Tanzanite ambayo yanapatikana Tanzania pekee. Alitamani kuingia mgodini, lakini kikwazo kikawa jinsia yake ya kike, baada ya kuelezwa kwamba wanawake hawaruhusiwi. Kwa mwezi mmoja, alikuna kichwa na hatimaye kuingia rasmi mgodini baada ya rafiki yake kupata mamilioni (jina tunalo) aliyemrudisha Arusha mjini na kumuoa.

“Alitaka tuondoke wote, nikamkatalia kwa sababu sikujua nitakwenda kufanya nini. Sikuwa nimesoma hivyo niliamua kupambana na maisha. Maisha yangu yote kabla ya kuolewa nilikuwa nachunga ng’ombe, sikusomeshwa na hata nilipokwenda kuishi na shangazi yangu huko Upareni, bado sikusoma…ndipo nikaolewa. “Niliposhindwa kuvumilia adha za ndoa, niliondoka nikiwa na kitoto kichanga…

Baadaye nikajikuta Mererani ambako niliamua kutafuta maisha,” anasema mama huyo aliyeweka historia ya kuwa mwanamke wa kwanza kuingia mgodini kuchimba madini sambamba na wanaume. Kama wanawake hawakuruhusiwa, ilikuwaje akafanikiwa kupata nafasi mgodini? Anasema, baada ya kufuatilia nyendo za utendajikazi, alijiaminisha ataweza. Akaomba apelekwe kuomba kazi, lakini hakuna aliyemkubalia huku wakimtadharisha kuwa, akionekana, yeye na aliyempeleka wangeweza kuuawa.

Ndipo akapata akili ya ziada, alikwenda kununua mavazi ya kiume, suruali, mashati ya mikono mirefu, kofia na viatu vya kiume, vikiwemo raba. “Zile suruali nilizikata zikawa kama kaptura ili kimavazi nionekane kama mwanaume,” anasema na kuongeza kuwa, ili kukamilisha ndoto yake, alibadilisha pia jina lake, akijiita Uncle (Mjomba) Hussein. “Sikumwambia yeyote kuhusiana na jina langu halisi ambalo ni Pili. Hata leo hii ukifika katika kambi hiyo kwa lengo la kunitafuta, hutanipata kwa jina la Pili, bali Hussein,” anasema huku akiangua kicheko katika mazungumzo kwa njia ya simu yaliyodumu kwa takribani dakika 36, na hatimaye kuzaa makala haya.

Anasema, hakufanya makosa, kwani baada ya kuingia kwenye migodi hiyo yenye joto, uchafu mwingi na wenye kina cha meta zaidi ya mia moja chini ya ardhi, alifanya kazi kwa juhudi kubwa kwa kati ya saa 10 hadi 12 kwa siku. “Nilikuwa na nguvu nyingi na nilifanya kazi pengine zaidi ya wanaume. Hakuna aliyenishuku kuwa mimi ni mwanamke, vaa yangu, lugha yangu ilikuwa zaidi ya mhuni wa kiume. Humo nilipigana na kuwashikisha adabu, niliogopewa.

“Lugha za hovyo hazikukauka mdomoni mwangu, na mara nyingi nilikuwa na sime mithini ya mmasai…,” anasimulia na kuongeza kuwa, vitu kama bangi alikuwa navyo mara nyingi na hata kuwapa wenzake, lakini kamwe hakuwahi kuvuta hata sigara wala kunywa pombe, ingawa hakuwa anakosekana katika maeneo ya aina hiyo, huku akimwaga ofa kwa waliomzunguka. Mwaka mmoja ulikatika bila kushitukiwa kuwa ni mwanamke.

Ilipotimu mwaka mmoja na miezi saba akiwa katika kazi hiyo, alibahatika kupata kiasi kikubwa cha madini, lakini kwa kuwa hakuwa anayajua vyema, alijikuta akitapeliwa. “Kuna kijana yule aliyenionyesha kule, nilimwamini nikamwambia akaangalie kama ni yenyewe ili tupate fedha . Nakuambia, hakurudi. Siku ya pili aliyenunua akaja na kunitafuta akiulizia Mjomba Hussein, aliponipata akawauli Lakini fungakazi ilikuwa baada ya kumuonesha baba yake mabulungutu ya fedha yaliyokuwa kwenye begi.

Bila kusema neno, baba alikimbilia polisi, akiamini binti yake huyo kati ya watoto 38 aliokuwa nao, pengine alikuwa amejiingiza kwenye ujambazi. “Hakuamini kabisa baba. Baada ya Polisi kuja na gari lao, wanilihoji na nikawaeleza ukweli, wakaondoka. Lakini kwa fedha Azile niliwajengea mama zangu sita (wake wa baba yake) kila mmoja nyumba yake, nikagawa fedha za mitaji kwa kaka zangu na ndugu wa karibu. “Hakika ilikuwa neema iliyofunguka. Nikajenga pia msikiti kijijini.

Hata Mererani nilijenga msikiti ambao hata hivyo uliteketea kwa moto mwaka jana ambao ulifanya uharibifu mkubwa katika migodi zaidi ya 15 Mererani,” anasema mama huyo wa mtoto mmoja. Ubakaji wamuumbua Miaka kumi ya kuuhadaa umma kuwa yeye ni mwanaume, ilikoma baada ya kuwapo kwa tukio la mwanamke mmoja kubakwa na wachimba madini eneo lao. Mjomba Hussein alikuwa miongoni mwa washukiwa na wenzake walipobanwa walidai kuwa yeye ndiye mhusika mkuu.

“Nikapelekwa kituo cha Polisi, mbali sana na pale, tena kwa mguu. Hakuwa na jinsi, zaidi ya kutoboa siri yake kuwa yeye si mwanamume, hivyo asingeweza kubaka. Hili liliwashangaza sana askari wale, hawakuamini… “Nikawaomba wanitafutie askari mwanamke, ilipothibitika kweli mimi ni mwanamke, niliachiwa huru…wachimbaji wenzangu hawakuamini hata baada ya kuthibitishiwa na Polisi,” anasema na kuongeza kuwa, waliamini mwaka 2001 alipoolewa.

Hata hivyo anasema haikuwa rahisi kuanzisha mahusiano na mwanaume, kwani wengi walimchukulia kuwa ni mwenzao. Anasema mtu aliyemwoa, naye ilimchukua miaka mitano kujiridhisha kama kweli Mjomba Hussein ni mwanamke na ndipo wakaanzisha mahusiano. Kwa sasa, anasema anaishi maisha ya kawaida kama mwanamke mwingine, ingawa ilimchukua muda mrefu, hadi miaka mitatu iliyopita alipoanza kuvaa tena mavazi ya kike na pia kujichanganya na wanawake wenzake katika shughuli mbalimbali.

Faida mgodini Anasema amenufaika kwa mambo mengi, ikiwa ni pamoja na kupata leseni ya kumiliki mgodi, huku akiajiri wachimbaji takribani 70, watatu kati yao wakiwa wanawake ambao ni wapishi. Ameweza pia kujenga nyumba kadhaa katika miji ya Arusha, Babati, Mererani na Singida, lakini pia akifanya shughuli za kilimo katika mashamba makubwa. Anamiliki matrekta mawili ili kufanikisha shughuli zake za kilimo. Pia anafuga, akiwa na ng’ombe takribani 100, mbuzi na aina nyingine za mifugo.

Lakini kama kuna kitu anajivunia, ni kufanikiwa kusomesha watoto zaidi ya 32, miongoni mwao akiwa Hassan Gwaay, mwanafunzi kinara katika masomo ya sayansi katika matokeo ya kidato cha sita mwaka 2016. Hassan, kwa sasa ni mwanafunzi wa uhandisi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM). Kijana huyo alihitimu elimu ya kidato cha sita katika Shule ya Sekondari ya Wavulana Tabora (Tabora Boys) aliyojiunga nayo akitokea Shule ya Sekondari Benjamin William Mkapa iliyopo Mererani mkoani Manyara alikosoma kidato cha kwanza hadi cha nne.

“Mimi sikusoma, ila naona kuna kitu muhimu nilikikosa, ndiyo maana nawiwa sana kusaidia wengine kielimu…,” anasema mama huyo jasiri mmwenye wajukuu watano sasa. Kilio chake Akiwa mchimbaji wa kwanza wa madini mwanamke aliyethubutu kuingia mgodini yeye mwenyewe, anasema kiu yake ni kupata wawekezaji atakaoshirikiana nao kufanya uchimbaji wa kisasa ili aweze kunufaika zaidi. “Serikali itusaidie kwa kweli.

Tumepambana vya kutosha, lakini tutanufaika zaidi tukipata wawekezaji, binafsi nawakubali sana Wachina, nikimpata mwekezaji wa kushirikiana naye, aaah…maisha yatakuwa mazuri muda si mrefu. Asaka bilioni 900/- Hata hivyo, anasema kwa kuwa amefanya kazi kwa muda mrefu, kama Mungu akimbariki na kumwezesha kupata angalau Sh bilioni 900, angependa kuanzisha miradi mikubwa ya kijamii ikiwamo ujenzi wa shule za kisasa, hospitali na kadhalika, ili aweze kuisaidia jamii.

“Hakika Mungu akinijalia kupata angalau kiasi hicho, ndoto yangu na kugeukia upande wa huduma za kijamii. Bado nina malengo makubwa, tatizo ni fedha, labda wakipatikana hao wawekezaji mambo yanaweza kunyooka,” anasema mama huyo anayekataa kutaja kiasi kikubwa cha fedha alichowahi kukishika kwa kuuza madini, lakini kwa ujumla akisema fedha alizopata kwa miaka yote ni zaidi ya Sh bilioni 10. Inatoka Uk. 14