ANGELINA MAKOYE: Mtanzania aliyeandika historia China

NIKIWA ubalozi wa Tanzania nchini China kwa shughuli zangu za kikazi, nashtuliwa na msichana mdogo anayenikumbatia na kujitambulisha kwangu kuwa ni Angelina. Namkumbuka na tunasalimiana kwani tumekuwa tukiwasiliana kwa simu kwa mwezi mzima bila kuonana mara baada ya kufika nchini China na kupewa namba yake kama Katibu wa wanafunzi Watanzania wanaoishi katika mji wa Beijing.

Baada ya kukutana naye siku hiyo, ananiomba msamaha kutokana na kubanwa na kazi nyingi pamoja na shule, anafanya ujasiriamali wa aina mbalimbali ikiwemo kusuka, kutafsiri lugha mbalimbali kama Kichina, Kiswahili na Kiingereza. Namfahamu na kila anapopata muda amekuwa akiwasiliana na mimi hata kunitembeza katika mji huu wa Beijing na ndipo ananidokeza kuandaa tukio la kihistoria kwa Tanzania na Watanzania waliopo nchini China na hasa mji wa Beijing.

Angelina Makoye (24) alifika nchini China mwaka 2015, ni mwanafunzi wa Shahada ya Kwanza ya Biashara ya Kimataifa (International Trade) katika Chuo Kikuu cha Beijing Information Science and Technology akichukua masomo yake kwa lugha ya kichina inayotumika darasani.

Msichana huyo wa Kitanzania ambaye amekuwa gumzo katika mji huu, mbali na shule huwa anafanya biashara ndogo za mitandaoni kuuza vitu wakati mwaka 2016/17 amekuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Wanafunzi wa Tanzania wanaosoma Beijing ikijulikana kama ‘TZSub’. Anasema akiwa na nafasi hiyo, ameweza kutafuta nafasi za udhamini kwa wanafunzi wa Kitanzania na kuwa wakala wa kutangaza nafasi za masomo kwa viwango vyote yaani masomo ya Shahada ya Kwanza hadi Shahada za Uzamivu.

Angelina anasema aliamua kufanya hivyo bila kutoza gharama zozote kwa lengo la kusaidia Watanzania waweze kupata elimu na licha ya kumaliza nafasi hiyo bado anaendelea kusaidia wanafunzi wanaotaka kusoma China kwa bei nafuu na vyuo vyenye kukidhi Elimu ya Tanzania. “Kama binti wa Kitanzania nimekuwa mwanaharakati wa kijamii yaani social activist. Ninaendelea kujifunza kila leo kwa kushiriki katika jamii ili kila mmoja afurahie uwepo wake.

Anaeleza kuwa kilichomfanya kuandaa tamasha hilo ni kuwa wakati akiwa nchini Tanzania alifahamiana na makundi tofauti ya vijana na alipofika China hakupata nafasi ya kukutana na vijana wenzake wala kina dada wenzake kujadili mambo yanayozunguka katika jamii. “Baada ya kupata uongozi nilipata nguvu ya kuwa nakutana nao ila tu kuna jambo likawa la tofauti kwangu ndipo niliamua kuandaa tamasha kwanza la wanawake ambalo halitakuwa moja tu bali endelevu la kutukutanisha kila baada ya muda fulani kukumbushana kupeana mambo mawili matatu,” anasema.

Anaeleza kuwa alitamani mara nyingi wanawake wote wa Beijing na nje ya mji wajue nafasi ya upendeleo waliyonayo na kuitumia vizuri. “Tusijisahau kuwa tupo China ila tukumbuke kuna vitu vya kufanya na kujifunza hata tukirudi katika nchi zetu tukirudi kazini au kama mwanamke huna kazi ujiajiri wenyewe,” anasema.

“Women for women, women for the society” alieleza kuwa ana maana kubwa na anaamini kuwa karne hii wanawake wengi wamejikwamua ila wapo pia ambao serikali na taifa inafanya kazi kuwafanya kuwa wanawake wana haki fulani na kuondokana na changamoto.

Akizungumzia jinsi anavyofanya shughuli zote yaani shule, ujasiriamali na mengineyo anaweka wazi kuwa hata yeye anaamini inavyokuwa. Anakumbuka baba yake wakati wote huwa anamueleza kuwa “fanya la muhimu kwanza haya mengine yatafutia,” hivyo kabla ya yote kipaumbele chake kwanza ni shule, yaani elimu kwanza. Angelina anasema hayo mengine hayaingilii ratiba ya shule na huyafanya pale anapopata muda wa kuwa huru na mara nyingi muda mwingi kazi zake hutumia simu.

Anaongeza kuwa wazazi wake wamechangia kwa kiasi kikubwa yeye kufika hapo alipo kwani wamejitoa kuhakikisha ndoto zake zinakuja kutimia kwani mambo kadhaa yanawapa nguvu wazazi wake kuendelea kutoa mchango wao.

“Nilipofika mwaka wa kwanza baba alinilipia kila kitu, baada ya mwaka shule ilikuwa inatoa zawadi kwa wenye matokeo mazuri darasani wanapatiwa scholarship hivyo ikatokea kuwa nami ni mmoja wa waliotunukiwa kusoma shule kwa scholarship kila mwaka kwa kuangalia matokeo yangu, naamini hili swala lingemfurahisha mzazi yeyote,” anasisitiza.

Anaeleza kuwa kabla hajamaliza masomo yake ameanza kula matunda kwani kutokana na kufahamu Lugha ya Kichina amekuwa akitumika kutafsiri katika kampuni kutoka Tanzania kama Goshen Safaris, Bright African safaris na mengine mengi wanapokuwa katika mikutano China au kufanya mikutano na maonyesho.

Anasema wakihitaji mtu wa kutafsiri na ratiba za shule hazijambana huwa anafanya kazi ya kuwatafsiria Kichina kwenda Kiswahili au Kiingereza. Angelina anasema bado kutokana na matokeo mazuri darasani chuo kinaendelea kumfadhili, hivyo kuwapunguzia wazazi majukumu.

Anasema katika kumkomboa mwanamke ana nafasi kubwa kwani hajawahi kuona ukombozi ambao haupati maswahibu, na yeye anasema anapenda anapopata changamoto kwani zinampa nguvu ya kufanya jambo kubwa zaidi.

“Katika kumkomboa mwanamke nitaendelea kuwaelimisha wanawake ambao bado wapo nyuma, ambao wao wanaona jambo fulani ni kwa ajili ya watu wengine sio wao, elimu ni kila kitu kitendo cha kumfundisha mtu mambo yanayomuhusu yeye na jinsi ya kujisaidia hio ndio njia sahihi,” anasema.

Anaeleza kuwa huwa anapinga sana kumpa fedha mwanamke bila kumfundisha namna ya kuipata, huko ni kudumaza akili, hivyo ni vyema kumfundisha jinsi ya kuipata itasaidia kuinua kipato chake na familia yake. Anashauri makundi ya wanawake kutokukata tamaa kuendelea kutoa elimu kwa wenzao bila kuchoka katika kukabiliana na changamoto mbalimbali.

Angelina ni mtoto wa pili kati ya watatu katika familia ya mzee Makoye Ng’erere wa jijini Mwanza. Anasema elimu ya awali mpaka kidato cha sita amesoma nchini. Anapongeza desturi ya Watanzania kuwa pamoja nyakati zote kwani hata alipofika nchini hapa hakupata taabu kutokana na Watanzania kuwa karibu kwa kushirikiana na Ubalozi.

“Watazania tuliopo China tuna umoja sana nafurahi sana huwa naona tatizo la mmoja ni tatizo la Watanzania wote na furaha ya mmoja ni ya wote, ila pia Watanzania hushiriki maonyesho mengi sana ya utamaduni hivyo kama Watanzania kwa pamoja huwa tunasaidiana kuitangaza nchi yetu kwa mataifa mengine kupitia nyimbo, chakula, kucheza, vinyago, makablasha yaliyoelezea nchi, mlima kilimanjaro, mbuga zetu zote na maandalizi mengine mengi,” anasema.

Anataka Watanzania wanaoishi maeneo mengine duniani kuiga tabia hiyo kwani inafanya kuwa ndugu na kujenga umoja mkiwa maeneo ya ugenini. Angelina anasema anapenda kuangalia filamu na vipindi vya ‘social activist’ wa kimataifa, ila lingine kufahamiana na watu kwani anaamini popote akikanyaga anapenda kuacha alama yake .

Anasema China ni sehemu nzuri ya kujifunza na kurudisha nyumbani Tanzania ujuzi tofauti, kwani wachina wanafanya kazi sana, hivyo wachche wanaopata fursa ya kuja huku kutumia vema, ili ukirejea kuendeleza taifa.

Anawashauri wasichana kuwa ni vyema kuthubutu kufanya jambo ambalo anaona litaleta tofauti siku za mbeleni, kwani sio lazima wote wahudhurie maonyesho, sio lazima wote waandae matamasha ila waangalie lengo la haya matamasha ni nini na lipi la kujifunza, hamna mwanamke alijaribu bila kukata tamaa akashindwa.

“Hamna kitu kirahisi tusiwe watu wa kutaka njia za mkato katika maisha, mimi nimeona ni bora uchukue njia ndefu na katikati utakumbana na mengi yatakayokujenga ukifika tamati unajikuta una tofauti sana na aliyechukua njia fupi,” anasema.

Anawaomba akinadada kuthubutu, “wadada wenzangu kwani ndiyo tegemezi la jamii ya kesho, je tutawafunza nini watoto wetu kama tunachagua ‘short cut’, tafakari!” Anasema kati ya wanawake anaowakubali sana ni mama yake kwani ni mwanamke wa kawaida sana na mama wa nyumbani ila anafanya kazi sana.

Pia katika jamii anampenda Asha Rose Migiro kwani ni mwanamke wa nguvu, huku kwa wanawake vijana ni Jennifer Shigoli, kwani amekuwa mdada wa tofauti kwa kuanzisha kiwanda. Angelina anasema akibahatika kukutana na Rais John Magufuli sasa atampongeza, kazi nzuri aliyofanya tangu Rais huyo aingie madarakani, ila pia atamkumbusha tu asiache wanawake, awapiganie pia