SALIM AHMED 'GABO': Anayekuja na mapinduzi katika Bongo Movie

WAKATI soko la filamu za Tanzania likiendelea kushuka kwa kasi, wasanii wa tasnia hiyo maarufu kama Bongo Movie, wamekuwa waathirika wakubwa kiuchumi. Soko limewapoteza na baadhi kulia ugumu wa maisha.

Wapo walioamua kujificha na kutoonekana tena kwenye hadhara ya watu kwa kuhofia kuchekwa au kuulizwa juu ya hali zao na mbwembwe za matanuzi waliozokuwa nazo kabla ya upepo kubadilika.

Lakini takribani wiki tatu au nne tumeshuhudia mwigizaji Salim Ahmed `Gabo Zigamba’ akizindua filamu katika mtindo wa kipekee ambao naweza kusema ndio unatambulishwa katika soko la filamu.

Aliamua kujikita kwa kuuza kazi zake kupitia mtandaoni kwa kipakua programu (App) ya Uhondo na filamu ya Kisogo ambavyo vinapatikana mtandaoni kwa Sh 500, badala ya Sh 1,500.

Mwandishi wa makala haya, alifanya mazungumzo na Gabo ili kujua kilichomsukuma kufanya hivyo, huku akithubutu kumshirikisha mwanadada ghali katika tasnia ya filamu nchini `Bongo Movie’, Wema Sepetu ‘Madam Wema’ kucheza filamu ya Kisogo ya dakika 15, lakini nusu yake unaweza kuiangalia bure na sehemu inayobakia inalipiwa kiasi cha Sh 500 tu.

Akifafanua, alisema aliamua kuja kivingine kutafuta soko la kazi za filamu baada ya kushindwa kuuza filamu zake madukani kama alivyofanya katika filamu ya Safari ya Gwalu.

“Nilianza kupata wazo hilo nikiwa na watu ambao tunafanya kazi pamoja, maana kila kwenye nyumba wanaweza kuwa na simu, lakini runinga zikawa mbili,” alisema Gabo ambaye aliingia rasmi katika Bongo Movie mwaka 2006, yaani miaka 11 iliyopita.

Alisema ndipo akaanza kuwa na fikra za kuibua upya soko, akiwaza kwanini wasianze kuuza filamu zake kwenye mtandao wa simu, kupitia programu ‘App’ ambayo mtu atapakua na kuwa nayo kwenye simu yake.

Anaongeza kuwa, ili kuvutia watu wengi kupakua programu, aliamua nusu ya filamu itazamwe bure, lakini ili mtazamaji aweze kumalizia uhondo, alazimike kulipia Sh 500 tu. Kuhusiana na faida anayoweza kuipata kupitia mtandao huo, alisema kwanza anahitaji kupata heshima kwa kuweza kufanya jambo ambalo wasanii wengi wanahofia kulifanya.

Anasema kukamilika kwa mchakato mzima mpaka watu wanaweza kupata filamu hiyo mtandao, amenunua nafasi katika mtandao wa kijamii ‘Saver’ ambapo ni fedha nyingi. Gabo anasema pia ametumia fedha nyingi katika kumchezesha mwigizaji Wema Sepetu, kwa kuwa ndiye anayejulikana kuwa ni ghali.

Katika Kisogo, alitumia fedha nyingi kugharamia kambi, kulipa wasanii na pia kwa ajili ya safari kutoka mkoa mmoja kwenda mwingine ili kukamilisha kazi hiyo. “Nilijua napoteza fedha nyingi kupitia mchakato huo, lakini nilijua mwisho wa siku watu watakuja kunielewa…,” alisema na kuongeza kuwa, anafahamu fika kuwa kwa gharama aliyotumia, inaweza kumchukua hata miaka miwili kurudisha fedha zake, lakini kikubwa kwake ni kufanikisha programu ya Uhondo kwa ajili ya kuuza filamu za wasanii wa Kitanzania mtandaoni.

Alisema baada ya filamu ya Kisogo, kuwekeza fedha, kinachohitajika ni kuungwa mkono tu….. Alivyoingia kwenye filamu Aliibukia katika uigizaji mwaka 2006 na filamu yake ya kwanza kuicheza ikiwa Olopang iliyotengenezwa na kuongozwa na Khalfani Abdallah kutoka katika kampuni ya Al Riyami ya Tanga.

Umahiri wake ulimfanya apate kazi zaidi, zikiwamo 007 Days, The Plan lakini funga kazi ya yote ilikuwa Bado Natafuta. Hii ilimwongezea mno umaarufu kutokana na kuuvaa vyema uhusika, akiigiza kama James, kijana masikini wa Kimakonde, muuza maji aliyekata tamaa ya maisha, licha ya kuwa na utaalamu wa ufundi magari.

Katika filamu hiyo, kijana huyo, akiwa katika mihangaiko anabahatika kupendwa na daktari, Patricia (Shamsa Ford) anayefanya kila njia ili aolewe na kijana huyo. Gabo pia amewahi kuchukua tuzo mbili kupitia kazi yake ya uigizaji, akiwa na tuzo ya mwigizaji bora wa kiume wa tuzo za Action & Cut Viewers Choice 2014 / 2015.

Pia alishinda mwigizaji bora nchini Kenya kupitia filamu ya Queen Masai. Amenufaikaje na filamu? Anasema filamu imempa manufaa mengi, ikiwa ni pamoja na kufahamiana na watu wengi, kushiriki kazi nyingi za kijamii na kuaminiwa na jamii na viongozi mbambali.

Alisema kuwa na gari, nyumba na vitu vingine ni vitu vya kawaida kwake, lakini kikubwa ni jamii kumuamini na kwamba sasa anamiliki kampuni yake ya Sarafu inayokuja na mapinduzi mapya ya kutafuta soko la filamu.

Nje ya Bongo Movie

Nje ya filamu, Gabo pia ana kipaji cha utangazaji. Kwa miaka miwili alirusha kipindi cha Bondeni kupitia televisheni ya taifa, TBC 1. Alikuwa akizungumza nchi mbalimbali kwa lengo la kuzungumza na kuangalia maisha ya Watanzania wanaoishi katika nchi mbalimbali za Afrika.

Hata hivyo, alishindwa kuendelea kutokana na kukosa wadhamini. “Yapo makampuni ambayo yalijitolea kunisafirisha na huko niliweza kuongea na Watanzania wengi, na kunieleza mafanikio na matatizo yao,” alisema na kuongeza kuwa, waliokuwa katika mateso katika nchi za watu, walimuona sawa na mkombozi akiwamini atawasaidia kurudi nyumbani.

Lakini pia anasema alibahatika kupata marafiki wengi katika safari yake ya kazi katika nchi zaidi ya kumi zikiwamo Afrika Kusini, Zambia, Zimbabwe na Malawi. Alibahatika pia kuwa Balozi wa kinywaji vya kuongeza nguvu mwilini `Energy Drink’ kwa muda miaka miwili.

Ni safari zake hizo za kikazi ndizo zilizomuongezea upeo wa kuona jinsi kazi za wasanii wa Tanzania, hasa filamu zilivyokuwa zinauzwa kiholela. Anaongeza kuwa, ingawa, licha ya kuacha utangazaji, hana mpango wa kugeukia ushereheshaji katika shughuli mbalimbali `U-MC’ kama ilivyo kwa mastaa wengine.

Anasisitiza hawezi kufanya kazi hiyo wala kujiingiza katika muziki. Kwa sasa, ameshaingia mikataba na Azam Tv kwa ajili ya mchezo wa kuigiza, lakini anatarajia akimaliza aweze kuingia mkataba mwingine na DSTv kwa kuwa tayari walishamuomba kufanya hivyo tangu mwaka jana. Hafuati nyayo za mastaa wengine.

Na amekuwa na misimamo hiyo, ndiyo maana ni mara chache amekuwa na kashfa za ulevi, uasherati au mambo mengine, vitu ambavyo vinaonekana kuwa sehemu ya maisha kwa baadhi ya mastaa. “Namshukuru Mungu najiepusha na mambo mengi.

Hata wasichana kuna wanaojiweka karibu kwa lengo la mapenzi, lakini nawageuza kuwa marafiki wa kawaida na tunabaki kuwa hivyo. Kingine cha bahati ni kwamba sivuti sigara, sinywi pombe wala aina nyingine yoyote ya kilevi,” anasema na kuongeza kuwa, hajawahi kuwa na uhusiano wa kimapenzi na mwigizaji yeyote wa filamu wala msanii wa muziki wa kizazi kipya.

Ana mpango na siasa? Anasema wapo waliomfuata mwaka 2015, lakini hakuwa tayari kutokana na kuamini ni kitu kinachowagawa watu haraka, hivyo ameamua kujitenga na siasa ili abaki katika sanaa.

Anasisitiza hata mwaka 2020, hana mpango wa kugeukia siasa, zaidi ya kutumia haki yake ya kikatiba ya kupiga kura. Anasema mara kadhaa, nyakati za uchaguzi yeye na ndugu wengine wa familia yao, huhamia kwa muda nchini Kenya ili kuepeka chokochoko za uchaguzi.

Hurejea baada ya uchaguzi. “Mimi ndugu zangu wengine wanaishi Kenya, wameolewa kule wamejenga kule na huwa tunahama, kwa kuwa kipindi cha uchaguzi chochote kinaweza kutokea,” alisema. Kinachomuumiza Anachukia wanaume wanaonyanyasa wake zao.

Anasema kama kuna kitu kinachomuumiza na hataweza kukisahau ingawa mara nyingi hapendi kukizungumzia, ni wakati mama yake alipoachika, hivyo kumfanya aishi maisha magumu. Anasema alikuwa na umri wa kujitambua, hivyo anakumbuka ubaya wa jambo hilo.

Ingawa wadogo zake walichukuliwa na upande wa baba, Gabo aliamua kuhangaika na kuishi na mama yake. Huyo ndiye Gabo, shujaa mpya wa filamu za Kitanzania anayeonekana kuwa na dhamira ya dhati za kuikomboa tasnia hiyo iliyoyumba tangu kifo cha aliyekuwa mfalme wake, Steven Charles Kanumba.

Mbali ya uigizaji wake mahiri ulioongeza ladha katika tasnia ya filamu, kampeni zake za kutaka kurejesha hadhi ya Bongo Movie na wasanii wake, Gabo ni miongoni mwa mambo yanayomfanya aonekane mwenye kiu ya kuleta mapinduzi katika tasnia hiyo.

Gabo anajua anachokifanya.

Angalia filamu kama 007 Days, The Killer, Safari, Fikra Zangu, Kona kisha angalia Safari ya Gwalu, utaona kitu kipya kwa kijana huyu, hasa baada ya ukimya wa mastaa wa fani hiyo kama Vincent Kigosi `Ray’, Jacob Steven `JB’ , Mahsein Awadhi `Dk Cheni’, Hemedi Suleimani `PhD’, Yussuf Mlela `Mlela’ na wengine. Hakika, kwa jinsi alivyoanza, kama akiungwa mkono, kuna kila dalili kwamba Gabo anaweka kutimiza ndoto yake. Hata hivyo, ni jambo la kusubiri na kuona