SALOME KAGANDA: Gwiji katika mapambano dhidi ya mfumo dume

“KWA kweli kesi ambazo sikuzipenda kabisa nilipokuwa Jaji, ni hizi za mauaji hasa ya kukusudia kwa sababu, mtu akitiwa hatiani, sheria inataka utamke adhabu yake iwe kunyongwa mpaka afe.”

“Sasa siku unatoa hukumu, unaona ndugu wa mshitakiwa kwanza wanakuangalia kwa huruma, wakiona unaanza kumtia hatiani, wanaanza kuonesha sura za kukuchukia kisha, vinaanza vilio; hasa adhabu ya kifo.”

Ndivyo anavyosema Jaji mstaafu Salome Kaganda ambaye pia ni Kamishina mstaafu wa Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma alipozungumza na gazeti hili nyumbani kwake Dar es Salaam. Gazeti hili lilitaka kujua katika majukumu yake akiwa Jaji, alikuwa anapata hisia gani anapotoa hukumu ya kifo kwa mtu.

Anasema, “Unajua majaji wengi wanamwogopa Mungu; ni waamini wazuri, hivyo kabla ya hukumu humuomba Mungu ili hukumu wanayoitoa iwe ya haki. “Kwa mfano mimi, nilikuwa namwambia Mungu, Mungu! Hukumu hii ingekuwa yangu, ningeibadilisha, lakini ni matakwa ya sheria katika kutenda haki...

Unajua kama umeonea, umependelea au kumkomoa mtu, nafsi itakusuta sana, lakini kama umetenda haki kwa mujibu wa sheria, nafasi haikutesi.” Japo aliipenda na kuitumikia kiuadilifu kiasi cha kuwa miongoni mwa wanawake waliotambuliwa na mradi wa kuwatambua na kuwaibua wanawake wasiojulikana, lakini waliotumikia jamii kiuadilifu na kuwa mfano bora kwa utumishi unaoendeshwa na Kituo cha Usuluhishi (CRC) kwa ufadhili wa Mfuko wa Wanawake Tanzania (WFT), anasema, “Kazi ya Mahakama ni muhimu katika jamii, ingawa inatengeneza maadui kila siku maana katika kesi, lazima awepo mshindi na aliyeshindwa; sasa karibu wanaoshindwa wote, wanasema rushwa imetumika.”

Kesi nyingine anazokiri kuwa hakuzipenda tangu akiwa hakimu katika ngazi mbalimbali, anasema ni zile zinazohusu ukatili wa kijinsia hasa dhidi ya mwanamke kutoka kwa mume na dhidi ya watoto. Kuhusu sababu ya kutopenda kusikiliza kesi hizo, anasema, “Unajua, wanawake wana uchungu na hasira wakati wa tukio, lakini, sheria ikianza kutumika, wanaona huruma ukitoa adhabu au talaka, baada ya muda unaona au kusikia wamerudiana. Unabaki unashangaa.”

MFUMO DUME UNAVYOTESA

Jaji mstaafu Salome Kaganda ambaye ni mwanamke wa kwanza kuwa Mkurugenzi wa Mahakama za Mwanzo Tanzania mwaka 1993, anasema madhara ya mfumo dume akiwa katika mahakama, alianza kuyaona mwaka 1975 alipokuwa Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo ya Kilosa Mjini.

Anasema, “Aliletwa mshitakiwa mmoja wa kesi ya wizi wa mifugo mbele yangu. Nikamuuliza kama ni kweli au si kweli. Akaniangalia akakaa kimya. Niliporudia kumuuliza akasema, ‘nikwambie nini wewe si ni mwanamke tu.”

Anasema askari walipoanza kuchachamaa huku mwenyewe akiwazuia, mshitakiwa akasema, “Mi nimesema sikuiba.” Kaganda anasema, “Ilibidi nimweke ndani kwa siku saba...” Kesi nyingine anayosema hataisahau katika unyanyasaji na ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake, ni ile ambayo mwanaume alimng’ata mkewe pua na kuitoa kabisa kiasi cha kumharibia sura mwanamke huyo.

Anasema kutokana na hali aliyokuwa nayo mwanamke huyo majeruhi, aliagiza mume apelekwe rumande wakati mkewe anauguza majeraha. Anasema, “Nikashangaa mama yule majeruhi anasema, sasa aende rumande, nani atanihudumia... Kwa kweli kesi za namna hii, zinapasua kichwa...” Mama huyu anasema kesi ya ukatili iliyomtia simanzi zaidi katika maisha yake ya ujaji akiwa Mahakam Kuu, ni ya mauaji aliyofanyiwa binti aliyekuwa ameolewa katika umri mdogo.

Anasema, mwanzoni mwanamume alikataa kuwa hakumuua mkewe, bali amedondokewa tawi la mti na kumdhuru mkewe. “Nilimrudisha rumande na siku nyingine akakiri kuwa wivu wa kupita kiasi ndio ulisababisha atende tukio hilo.”

“Kilichoniumiza sana, ni kujua kuwa kwanza, alikuwa ameoa msichana mdogo, hivyo anaendana endana na wenzake, lakini huyu akaona kwa vile wanalingana umri wa ujana, basi eti akamuua kwa madai kuwa wana uhusiano mbaya na vijana. Iliniuma sana kwa kweli,” anasema.

NINI MATAMANIO YAKE KUHUSU UNYANYANSAJI NA UKATILI WA KIJINSIA

Jaji mstaafu Kaganda anasema, mfumo dume ukiondoka, unyanyasaji wa kijinsia ukakoma na familia zikaungana na kuishi kwa upendo wa dhati, watoto watalelewa vizuri na taifa litakuwa na watu wazuri zaidi. “Elimu zaidi dhidi ya ukatili wa kijinsia itolewe.

Kazi kama inayofanywa na Tamwa (Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania) na wadau wengine kuelimisha umma, iungwe mkono na akinamama wawezeshwe kuwa na kipato japo kidogo kusaidia familia na kuondoa utegemezi wa kila kitu kutoka kwa mume.”

“Akina mama washiriki ujasiriamali na juhudi za Tanzania kuwa ya viwanda; washiriki ipasavyo maana ndio wakulima wakuu... Mungu hakukosea kumuumba mwanamke kama kiwanda cha uzalishaji; wakombolewe kiuchumi.”

Anasema, “Hii itasaidia kuondoa unyanyasaji maana mwanamke akitajirika, hakimbilii kuoa mwanamume mwingine, lakini mwanamume akitajirika, wengi wanakimbilia kuoa wanawake wengine; unaona sasa!” Hata hivyo anakwenda mbali na kukiri, “Unyanyasaji na ukatili unaonikera zaidi, ni ule wa kimwili kama vipigo kwa wanawake na watoto; pamoja na udhalilishaji kama matusi mbele ya watu na ukeketaji.”

AMBACHO HATASAHAU Anasema, “Sitalisahau sakata la Escrow; ilikuwa kazi ngumu maana viongozi wengi waliguswa wakiwamo majaji, viongozi wa dini na hata wafanyabiashara wakubwa.”

HISTORIA YA JAJI MSTAAFU KAGANDA IKOJE?

Ni mzaliwa wa tisa kati ya 10 wa familia ya Mwalimu Marko Benito Gwaja. Alisoma katika shule ya msingi Nduwika darasa la kwanza hadi la nane. Anasema, “Nikiwa darasa za tano, muhula wa kwanza; Middle School ya Ndewika, wazazi waliamua kumsomesha mtoto wa kiume pekee; mimi wakasema basi kwa kuwa watoto wa kike eti tunafeli, maana dada zangu wengi walishindwa kuendelea na masomo.”

“Kwa kweli niliumia sana. Nikaamua kuondoka nyumbani kimya kimya kwenda mashambani. Nyumbani walinitafuta sana siku hiyo hadi usiku nipoogopa na kurudi taratibu nikalala jikoni.” Anasema tumaini lake lilianza kurudi baada ya siku tatu kwani anafahamisha akisema, “Headmistress (Mkuu wa Shule ya Wasichana) alikuja nyumbani na kumkemea sana baba.

Baba akaelezea sababu ya kunizuia nisiendelee na masomo.” “Headmistress naye akaelezea namna nilivyokuwa bright (kuwa na akili) darasani. Akamwambia mama apewe ajira shuleni ili apate ada ya kunisomesha na mama akakubali.”

Anasema anashukuru akiwa katika Sekondari ya Wasichana ya Mtwara, Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere alitoa agizo kama alivyofanya Rais John Magufuli kwamba, hakuna kulipa ada ya shule; elimu bure.

“Kwa kweli watoto wa maskini tulijisikia kama tuliokuwa kwenye sikukuu ya Krismasi. Nikaendelea na masomo na hatimaye nikafaulu na kuchaguliwa kujiunga na Chuo cha Ufundi Dar es Salaam (Dar Tech) ambako nilipata ujauzito mwaka 1967.”

Kwa mujibu wa Jaji mstaafu Kaganda, hali hiyo ilimlazimu kuolewa na Mzee Kaganda akiwa na umri wa miaka 20. “Mzee Kaganda alisema, lazima tufunge ndoa.” Anakiri kuwa kilichomponza ni akili za utoto.

UTUMISHI

Kwa mara ya mwisho, Jaji mstaafu Salome Kaganda ameitumikia Tanzania kama Kamishina wa Tume ya Maadili kwa Viongozi wa Umma baada ya Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete kumteua katika jukumu hilo Desemba 2010.

“Hata baada ya Uongozi ya Mheshimiwa Kikwete, Mheshimiwa Magufuli (Rais John Magufuli) naye alipoingia madarakani, akanitaka niendelee na ndipo Desemba 2016, nikastaafu. Ninamshukuru Mungu kwa hili,” anasema.

Jaji Kaganda aliwahi kuwa Msimamizi wa Kanda ya Songea hadi alipostaafu mwaka 2009. “Katika utumishi wangu kwenye Idara ya Mahakama, nimewahi kuwa Mkurugenzi wa Mahakama za Mwanzo Tanzania. Hii ilikuwa mwaka 1993.

Nilikuwa mwanamke wa kwanza. “Mwaka 2004, nikapanda hadi kuwa Jaji Mahakama Nyota/ Mapishi Kuu. Kwa kawaida, unaanzia Dar ili kupata uzoefu, kisha nikahamishiwa Mtwara kwa mwaka mmoja.”

MWITO NA MATAMANIO YAKE

“Natamani kuona viongozi wanapopewa dhamana wasijione wameukata, bali wamepewa utumishi wa utumwa hivyo wajinyenyekeze na kutumikia umma kwa upendo na uadilifu.

Waioneshe serikali na jamii shukrani zao kwa kuwa inawaangalia maslahi yao tangu ugonjwa hadi jeneza, lakini wanaotumikiwa (wananchi) wako katika hali tofauti; ya chini hivyo, vipato wanavyopata viongozi, wasividharau, bali waridhike navyo.

Anasema, “Kwa sasa nimesajiliwa kama wakili binafsi, lakini sijisikii tena kusimama mahakamani; sanasana kutoa ushauri dhidi ya vitendo vya unyanyasaji watoto maana hilo ni eneo linalohitaji utetezi mkubwa kwa kuwa hawawezi kujitetea ‘mentally’ wala ‘physically’ (kiakili na kimwili).

“Mahakamani mtoto wanaogopa na sasa akimuona mshitakiwa aliyemfanyia ubaya, akili yake inarudi kulekule kwenye tukio alilofanyiwa… Mtoto ni shahidi asiyejiamini ndiyo maana ninasema, kesi za watoto ni changamoto inayohitaji uelewa mkubwa wa sheria na busara za kiutu.”

Alipoulizwa ana nini cha kujivunia katika maisha na utumishi wake, Kaganda alisema kwa kifupi, “Mungu ameniumba mwanamke na nimeshiriki katika uzazi... Ninamshukuru mume wangu Mzee Kaganda (sasa marehemu), maana alinitia moyo; akaniambia nikiacha shule na nyumbani kwake niondoke na akanipa support mbalimbali nikamaliza vizuri masomo.”