Hugh Masekela: Kwaheri Baba wa Jazz

GWIJI wa jazz, Hugh Masekela kwa mara ya kwanza alishika tarumbeta katika miaka ya 1950: wakati ambao rangi ya ngozi yake ilimaanisha kwamba alikuwa raia wa daraja la pili katika nchi yake, Afrika Kusini.

Lakini katika miongo iliyofuata, akaibuka na kuwa mtu maarufu duniani kote kwa muziki wake na jukumu lake kama mwanaharakati wa kupinga ubaguzi wa rangi. Nyimbo kama Soweto Blues zilisaidia katika kufanikisha yote hayo.

Kufikia wakati wa kifo chake katika umri wa miaka 78 – takriban miaka 30 baada ya kumalizika kwa utawala wa weupe wachache – alifahamika kwa jina la Baba wa Jazz Afrika Kusini. Ramapolo Hugh Masekela alizaliwa Aprili 4, 1939, katika mji wa KwaGuqa, kilometa 100 mashariki kwa mji mkuu, Pretoria, katika eneo maarufu kwa muziki.

“Unajua kila mtu anayo santuri,” aliwahi kusema. “Mjomba wangu alikuwa na sauti nzuri sana kwa hiyo aliimba rekodi zote – Count Basie, Duke Ellington, Louis Armstrong.” Masekela alianza kuimba na kupiga piano akiwa na umri mdogo, na ilikuwa filamu ya Hollywood iliyohusu wasanii wa muziki wa jazz wa Marekani, ambayo ilimvutia na kumfanya aanze kupiga tarumbeta akiwa na umri wa miaka 14.

Tarumbeta yake ya kwanza alipewa na mwanaharakati wa ubaguzi wa rangi Mwingereza Trevor Huddleston, mwalimu katika Shule ya Sekondari ya St Peter’s nchini Afrika Kusini ambaye baadaye alikuwa Askofu Mkuu.

Muda mfupi, kipaji chake kikawa wazi, Masekela na baadhi ya wanafunzi wenzake wakaunda Huddleston Jazz Band, bendi ya kwanza ya dansi ya vijana nchini Afrika Kusini. Wakati huo huo, Padri Huddleston alikuwa amefungiwa kuingia nchini Afrika Kusini kutokana na harakati zake kupinga ubaguzi wa rangi.

Lakini uamuzi huo ulitoa fursa nyingine kwa Masekela. “Padri Huddleston… alikutana na mtu niliyevutiwa naye Louis Armstrong na alimueleza kuhusu bendi yetu. Majibu ya Louis yalikuwa: “Safi, nitawatumia moja ya tarumbeta,’ na alifanya hivyo.

Hii iliifanya bendi ijulikane na kutangazwa katika kurasa za mbele za magazeti yote makubwa ya Afrika Kusini – kundi la kwanza la Weusi,” Masekela aliuambia mtandao “Hatimaye wakati ndege iliporuka, ilikuwa kama mzigo mzito ulikuwa umeshushwa kutoka mwilini mwangu – ni kama vile nilikuwa na maumivu ya kufunga choo kwa miaka 21,” aliandika katika kitabu kinachoelezea maisha yake.

Hakurejea Afrika Kusini kwa miongo mitatu. Lakini akiwa ughaibuni, kamwe hakusahau mapambano ya familia yake na rafiki zake aliowaacha wakiwa chini ya utawala wa weupe wachache. Manyanyaso katika Afrika Kusini yalichagiza uanaharakati wa muziki na siasa.

Muziki wake uligusa mapambano, mateso, furaha na mapenzi kwa watu wa nchi yake. Mwaka 1964, alimuoa mwanamuziki mwenzake wa Afrika Kusini, Miriam Makeba – mwimbaji ambaye baadaye alikuja kufahamika kama Mama Afrika.

Miaka miwili baadaye, ndoa yao ilivunjika kwa kutalikiana, lakini waliendelea kutumbuiza pamoja kwa miaka mingi. Masekela pia alikutana na mwimbaji wa jazz wa Marekani, Harry Belafonte, ambaye pamoja na Makeba, walimshawishi mwanamuziki huyo kijana kujiunga na shule ya muziki jijini New York.

Ni katika shule hiyo alikutana na Armstrong, ambaye alimtumia tarumbeta miaka kadhaa nyuma na alikuwa mtu muhimu katika kumshawishi awe na staili yake ya muziki. Akikumbuka mkutano wake na Armstrong, Masekela aliiambia Wall Street Journal: “Aliniuliza kama naimba. Nilimwambia hapana.

Alisema kwa sauti yangu, Kama nitaimba, kila mmoja anaweza kuimba.” Mwaka 1967, alitumbuiza katika Tamasha la Monterey Pop pamoja na Janis Joplin, Otis Redding, Ravi Shankar, The Who na Jimi Hendrix.

Lakini ilikuwa ni mwaka uliofuata, aliibuka na kibao chake kilichomtambulisha: wimbo wa vyombo vitupu, Grazing in the Grass, ambao uliongoza katika chati za Marekani na kuwa wimbo uliotikisa duniani kote.

Katika miaka ya 1980, Masekela – ambaye wakati huo alikuwa akiishi Botswana – alitumbuiza pamoja na Paul Simon katika ziara ya Graceland, akimtetea Simon wakati alipotuhumiwa kuvunja zuio la kiutamaduni. Mwaka 1987, wimbo wake, “Bring Him Back Home’ ukawa ‘wimbo wa Taifa’ kwa ajili ya Nelson Mandela baada ya kuachiwa kwake kutoka gerezani.

Wakati Mandela alipoachiwa kutoka gerezani mwaka 1990, Masekela alirejea nyumbani. Hata hivyo, nyuma ya pazia Masekela alikuwa na mapambano yake binafsi. Alikuwa akipambana na ulevi wa pombe na uraibu wa dawa za kulevya, na aliomba msaada mwaka 1997 – tabia ambazo alikiri baadaye kwamba zilimgharimia mamilioni ya Rands, fedha ya Afrika Kusini.

Lakini hakukubali uraibu umteketeze, na alianzisha kituo cha kurekebisha tabia na wasanii wengine mwaka 2001. Mwaka 2008, aligundulika kuwa na kansa ya tezi dume, lakini hii ilishindwa kumfanya akae kitako.

Mwaka 2010, alipanda stejini pamoja na mwimbaji wa Nigeria, Femi Kuti katika ufunguzi wa sherehe za Kombe la Soka la Dunia ambalo lilikuwa linafanyika Afrika Kusini – onesho ambalo wengi mjini Soweto wasingeweza kulifikiria miongo miwili kabla.

Miaka miwili baadaye, alifanya ziara na rafiki yake wa zamani, Paul Simon kuadhimisha miaka 25 ya ziara yao ya Graceland. Hatimaye Masekela ameshindwa ‘vita’ dhidi ya saratani ya tezi dume.

Katika miaka yake ya mwisho, alijielekeza katika kuhifadhi urithi wa muziki wa Afrika Kusini, pamoja na kukabiliana na ubaguzi dhidi ya wageni. Kwa maneno yake mwenyewe, alikuwa anahofu na hali hiyo.

“Sitaki kuishi zaidi ya hapa nilipo sasa… na ninaishi siku kwa siku. Na nafikiri unapojihusisha na kile unachokiacha na mambo yote hayo, unaacha alama muhimu,” alisema Masekela mwaka jana.

Hata hivyo, urithi wake utaishi milele – na salamu za rambirambi zimekuwa zikimiminika kutoka sehemu mbalimbali duniani, muda mfupi baada ya familia yake kutangaza kifo, bila kusahau majonzi kwa mwanawe wa kiume, Sal.