ANNA MSHANA, Mwanafunzi Bora anayeamini katika dhamira njema

JANUARI 30 Mwaka huu ni siku ambayo haitasahaulika kichwani kwa Anna Mshana, mmoja wa mabinti waliofanya vizuri katika mtihani wa kidato cha nne uliofanyika mwishoni mwa mwaka jana na matokeo yake kutangazwa Jumatatu ya wiki iliyopita.

Anna (17) binti wa kwanza kwa wazazi wake Benjamini Mshana, Mwalimu wa Shule ya Sekondari ya Jitegemee ya Jijini Dar es Salaam na Zahara Mustapha, Mwalimu katika Shule ya Sekondari ya Juhudi iliyopo Manispaa ya Ilala Jijini Dar es Salaam, na historia ya kipekee ambayo inachangiza kuibuka na matokeo aliyoyapata katika mtihani huo.

‘Kipaji hicho’ kilichoibuka na matokeo mazuri kutoka Shule ya Wasichana ya Marian iliyopo nje kidogo ya Wilaya ya Bagamoyo, ni miongoni mwa wasichana wanne, watatu kutoka katika Shule hiyo ya wasichana ya Marian huku mmoja mwingine akitokea katika Shule ya St. Francis Girls (Mbeya).

Mbali na Anna, wasichana wengine waliofanya vyema na kufanikiwa kuingia katika orodha ya wanafunzi kumi bora kitaifa ni pamoja na Elizabeth Mangu Marian Girls (Pwani), aliyeshika nafasi ya pili kitaifa, Lilian Katabaro, Marian Girls (Pwani), aliyeshika nafasi ya tisa pamoja na Eveline Mlowe kutoka shule ya St. Francis Girls (Mbeya), aliyeshika nafasi ya kumi kitaifa.

Anna ambaye ni mtoto wa kwanza kwa wazazi wake, alifanya mtihani wake kama ilivyo kwa wanafunzi wengine waliomaliza kidato cha nne mwishoni mwa mwaka jana akiwa na malengo ya kuibuka mshindi wa kwanza kitaifa katika matokeo ya mtihani huo, licha ya azma yake hiyo kugonga mwamba na kuishia kuibuka mshindi wa tatu.

“Niliamini nitakuwa wa kwanza wa wanapaswa kuwa na dhamira ya kweli kutoka mioyoni kwani ndiyo silaha ya ushindi,” anasema Anna huku akitabasamu. Anasema malengo yake ni kuwa Msanifu Majengo (Architecture), kutokana na kuipenda sana kazi hiyo akiamini kuwa bado kuna uchache wa wataalamu wa kazi hiyo nchini kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo za baadhi ya wanafunzi kuogopa masomo ya sayansi, wakiamimini kuwa ni magumu, suala analosema kuwa siyo kweli kama utaamua kuyawekea mkazo.

Anna anasema licha ya changamoto mbalimbali zilizopo katika sekta hiyo zikiwemo za uvamizi na uporaji wa viwanja vya watu na nyingine nyingi, anaona bado ana fursa ya kuwa mmoja wa wataalamu watakaofanya kazi kwa weledi ndani ya sekta hiyo na kulisaidia taifa lake kuondokana na migogoro hiyo anayosema tiba yake ni kwa watendaji hao kuwa wazalendo wa kweli.

Anasema ukiacha sababu ya kumudu vyema masomo ya sayansi na hivyo kumfanya kuipenda kazi ya Usanifu Majengo, pia ana kipaji kizuri cha uchoraji tangu akiwa mtoto, suala linaloungwa mkono na wazazi wake wanaoanza kwa kuelezea historia ya binti huyo tangu akiwa mdogo.

Baba mzazi wa Anna, Benjamini Mshana anasema tabia ya Anna kupenda shule ilianza tangu akiwa mtoto mdogo ambapo mara nyingi alipokuwa akiwaona watoto waliomzidi umri kidogo wakienda shule, alikuwa akilia sana na kutaka na yeye apelekwe shuleni licha ya umri mdogo ambao bado ulikuwa haumruhusu kwenda shule.

“Alikuwa akilia sana hadi unaweza kumuonea huruma, nakumbuka siku moja tukiwa sokoni mimi na mama yake aliona begi linauzwa, huku tukiwa na mpango wa kumnunulia viatu siku hiyo, aligoma na kutaka tumnunulie begi, bahati nzuri fedha ilibaki kidogo ikaweza kununua na viatu, hapo tukaona sasa tuna kila sababu ya kumpeleka shule walau ‘chekechea’ ili kumuepusha na ‘kilio’ cha kila siku,” anasema.

Anasema hata alipoanza masomo yake shule ya msingi ilionesha wazi kuwa njia yake kimasomo itakuwa nyeupe, kwani mara nyingi alikuwa akifanya vizuri katika mitihani yake mbalimbali shuleni, ukianzia ile ya kufunga shule na mitihani mingine ya majaribio.

Anna anasema wakati wote huo alipokuwa akisoma katika Shule ya Msingi ya Holy Cross iliyopo Temeke Jijini Dar es Salaam, hakupenda michezo mingi na wenzake, zaidi ilikuwa akijisomea kila wakati, tabia aliyojijengea hadi alipofika Sekondari.

Mshana anasema katika mtihani wa Taifa wa Darasa la nne, Anna alipata wastani wa alama ‘A’ katika jumla ya masomo yote matano waliyoyafanya katika mtihani huo Mwaka 2010, huku akipata tena alama hizo katika matokeo ya mtihani wa Darasa la Saba Mwaka 2013.

Anasema kama hiyo haitoshi, binti huyo mpole kwa sura pia katika mtihani wake wa kidato cha pili mwaka 2015, katika mtihani wenye jumla ya masomo kumi walioufanya alipata alama ‘A’ kumi na alama ‘B’ moja, hatua aliyosema ilizidi kumpa matumaini kuwa siku moja ataweza kuwa namba moja kitaifa kama alivyojiwekea katika malengo yake.

Mzazi huyo anasema kabla ya matokeo hayo ya mtihani wa Taifa wa kidato cha nne yaliyotangazwa hivi karibuni na kumfanya ashike namba tatu kitaifa kwa kupata alama ‘A’ kumi katika masomo yote kumi aliyoyafanya, pia mtihani wa ‘mock’ uliofanyika miezi michache kabla ya mtihani huo wa Taifa alipata alama ‘A’ kumi kama ambazo amefanikiwa kuzipata katika mtihani huo wa Taifa.

Kwa upande wake Mama yake, Zahara Mustapha anasema alitegemea mwanaye kufaulu katika mtihani huo, isipokuwa akili yake ilijielekeza kuona kama mwanaye, je! ataibuka kuwa miongoni mwa wanafunzi 10 bora katika orodha inayotolewa na Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA), kutokana na imani aliyokuwa nayo kwa binti yake.

Anasema yeye kama mwalimu, wakati mwingi binti yake akiwa likizo alitumia muda wake mwingi kuhakikisha anamsaidia binti yake katika masomo mbalimbali, kitendo ambacho hata baba yake alikuwa akikifanya muda alipopata nafasi ya kuwa karibu na binti yake huyo.

Zahara anasema kwa mara ya kwanza kupata taarifa za matokeo ya mwanaye huyo alikuwa kwenye simanzi kubwa, kutokana na tukio la kuibiwa vifaa mbalimbali katika gari yake lilifanywa na watu wasiojulikana usiku wa kuamkia siku hiyo ambayo matokeo yalikuwa yakitolewa.

Anasema aliposikia kuwa binti yake kashika nafasi ya tatu na kuibuka ndani ya kumi bora, alifurahi sana kiasi cha kusahau ‘maswahibu’ ya kuibiwa vifaa vya gari yake na kuamua kumuachia Mungu, huku yeye akiendelea kuwa karibu zaidi na bintiye huyo akimuona kama mgeni mpya ndani ya nyumba yake.

Mama huyo anasema anaamini kuwa huo ni mwendelezo mzuri wa safari ya kimasomo ya Anna kutokana na jitihada mbalimbali anazozionyesha wakati wote awapo katika masomo yake, huku akimsifu pia bintiye huyo kutokana na kuwa na nidhamu nzuri.

Bahati Joseph alikuwa Mwalimu wa Darasa wa Anna katika shule ya Marian , anasema anaamini kuwa kufanya vyema binti huyo ni kipaji alichonacho kutoka kwa Mungu, kutokana na uwezo mkubwa aliokuwa nao tangu anaanza kidato cha kwanza shuleni hapo.

Anasema tangu ajiunge na masomo shuleni hapo, Anna hajawahi kutoka nje ya wanafunzi 10 bora katika mitihani yote waliyofanya shuleni hapo licha ya uwepo wa wanafunzi wenzake walioonekana pia kuwa na uwezo mkubwa wa kimasomo.

“Hata upande wa nidhamu kwa sababu mimi pia ni mwalimu wa nidhamu hapa shuleni, Anna hakuwahi kuonyesha utovu wowote wala kunisumbua katika eneo hilo, naamini safari yake ya mbeleni itakuwa nzuri na salama kutokana na mwanzo mzuri au dalili anazozionyesha wakati wote, ” anasema Mwalimu Bahati.

Aidha anasema hata katika mitihani ya shule za Kikatoliki iliyokuwa ikihusisha mikoa ya Pwani na Dar es Salaam, ukihusisha wavulana na wasichana, Anna aliweza kushika nafasi ya nne miongoni mwa wanafunzi wote, suala linaloonyesha kuwa binti ana kipaji maalumu katika masomo. Mwisho