Kama Mzazi: Ajira ya ya wafanyakazi majumbani iwekewe mkakati

Katika safu yetu ya Kama Mzazi wiki hii naomba nianze kwa kuwapa pole wazazi vijana kwa maana ya wale wanaojiunga katika kundi hili hivi sasa la kuwa wazazi na walezi wa watoto wetu.

Hakuna ubishi kwamba enzi zetu sisi za miaka 47 kulikuwa na urahisi wa aina yake wa kuweza kupata watumishi wa ndani wa kuweza kuwalea watoto wakati wazazi wakiendelea na shughuli zao nyingine za kuwaingizia kipato cha kuendesha familia zao.

Wazazi waliokuwa wanahitaji huduma hii ni pamoja na wale walioajiriwa na wasioajiriwa kwa kuwa kuna wakati ambao hulazimika kuondoka nyumbani kwenda kutekeleza majukumu yao mbali na wanapoishi au hapohapo wanapoishi lakini wasingeweza kutekeleza majukumu hayo wenyewe bila kuwa na wasaidizi wa kuyashughulikia masuala ya ndani ya familia zao ikiwa ni pamoja na usafi, uandaaji wa chakula na utuzaji watoto.

Upatikanaji wa watoto wa kazi kama wanavyoitwa siku hizi ni kinyang’anyiro kikubwa kiasi kwamba baadhi ya wazazi vijana hivi sasa wanaona ni kama adhabu ya aina yake kuzaa au kuanzisha familia.

Wakazi katika mitaa,miji na majiji yetu mbalimbali hususan ni wazazi vijana hivi sasa wanafikia hatua ya vuta nikuvute kati ya mmoja wao kubaki nyumbani au kuacha kazi kwa ajili ya kukosa mtoto wa kazi.

Mmoja wa wazazi vijana ambaye ni mwanamama anayesoma shahada ya pili katika moja ya vyuo vikuu vya jijini Dar es Salaam nyakati za jioni anasema,ni muda wa miezi sita sasa tangu msichana wake wa kazi aondoke na hajapata mwingine wa kuchukua nafasi yake.

Mama huyo ambaye kutokana na miiko ya kazi siwezi kulitaja jina lake ana watoto wawili, mmoja kati yao ni msichana wa miaka 11 huku mdogo wake akiwa na miaka mitano.

‘’Sina jinsi. Hivi sasa wakirudi shuleni hujipikia wenyewe. Nikirudi kutoka darasani ni majira ya kati ya saa 4 na saa 5 usiku. Wakati mwingine huwakuta wameshalala,’’ alisimulia na kuongeza kwamba ‘’wanakua kabla ya wakati wao lakini sina jinsi.’’

Alisimulia kuwa msichana wa kazi aliyeondoka alimfanyia vituko miezi miwili tu baada kuanza kazi hivyo kulazimika kumwodoa.

’’Hali ni ngumu,’’ alisema kwa kukata tamaa. Ukipata wasaa wa kuzungumza na wazazi vijana watakuelezea kila mmoja wao madhila wanayokabiliana nayo katika kusaka huduma adimu ya watoto wa kazi.

Kuna ombwe na mahitaji makubwa ya huduma hii kwa sasa lakini pia upatikanaji wake hauna uhakika. Pengine wakati umefika wa kuanzisha kwa makusudi mafunzo ya watoto wa kazi katika utaratibu rasmi na kisha watakaofuzi mafunzo hayo wajiunge katika kampuni ambayo itaweza kuweka matangazo ya ajira za watoto wa kazi.

Vyombo husika vichukue hatua mahususi kuwasajili rasmi na kuwa ajira kama ajira nyingine kwa kufuata taratibu na sheria za kazi.

Hatua hii ni muhimu na kinyume chake wazazi vijana na watoto wao wataendelea kuishi kwa kadhia kubwa na hatari. Watoto wanaolelewa katika hali ya kubahatisha ya aina hii inawezekana kabisa wakawa hapo baadaye kama watoto wa mitaani.

Kama suala la ajira linaendelea kukua siku hadi siku, kwa nini tushindwe kubuni aina hii ya ajira kwa kuiwekea utaratibu unaoeleweka ili kila mmoja wetu aipate huduma hii kwa uhakika? Tusikate tamaa tuungane tujaribu kuikabili hali inayotishia ustawi wa jamii yetu.