Kama Mzazi: Mabasi ya abiria yasioneshe video za picha, miziki ya ngono

KUKUA na kusambaa kwa teknolojia ya habari na mawasiliano (ICT) ndani na nje ya Tanzania, kuna faida na hasara zake.

Leo, nitajikita upande mmoja wa madhara hususan maonesho ya video zenye picha na miziki yenye maudhui ya ngono katika mabasi ya abiria kwani imekuwa ada kwa magari hayo, kutumbuiza abiria wawapo safarini ili kupunguza makali ya safari bila kujali uwepo wa mchanganyiko wa abiria wa umri, jinsia na mahusiano tofauti.

Hili si jambo jema. Teknolojia ya Habari na Mwasiliano sasa inatumika vibaya. Badala ya kujenga jamii yenye maadili, maonesho ndani ya mabasi yanakiuka maadili kadiri ya mila, tamaduni na desturi zetu za Kitanzania.

Baadhi ya vyombo vya usafiri, vinajaribu kuendeleza juhudi hatari za kutuhamisha kutoka mfumo wa analogia kwenda mfumo wa digitali, bila kujali madilifu, mila na desturi zetu.

Katika miaka ya 70 na 80 hatukuwa na televisheni, hivyo hatukuona taarifa za habari na burudani moja kwa moja au sinema, maigizo, vichekesho na muziki.

Kutokana na teknolojia ya habari na mawasiliano, vyote hivyo sasa vinapatikana kwa wingi tena kwa mfumo wa kidigitali. Ulazima wa kutafuta na kuzifuata burudani hizo katika nyumba za sinema kama ilivyokuwa miaka hiyo, haupo.

Nyumba nyingi za sinema zilizokuwapo katika miji kama Dar es Salaam na makao makuu ya mikoa mbalimbali, zimefungwa. Simu za mkononi pia zimekuwa kiunganisha kinachowezesha watumiaji picha na miziki mbalimbali kadiri ya mahitaji mradi tu, simu iwe na kifurushi cha kutosha.

Nia njema iliyokuwepo zamani kutoruhusu watoto kuona au kutazama picha zisizowahusu kiumri ili kuwalinda kimaadili, imeanza kutoweka katika jamii na kuifanya jamii ilazimike kuchukua hatua kuidhibiti katika maeneo ambayo jamii kadiri inavyowezekana licha ya ugumu uliopo.

Kama Mzazi ninasema, baadhi ya mabasi ya abiria yanakiuka mila na desturi za Kitanzania kwa kuthubutu kuonesha miziki na picha chafu na vichekesho vyenye sura na maudhui ya ngono, bila kujali mchanganyiko wa abiria waliopo ndani ya basi.

Huu ni ukatili wa kimaadili dhidi ya watoto na watu wanaokuwapo katika vyombo hivyo. Kama Mzazi inanikera kwani hakuna asiyejua kuwa huduma nyeti za umma kama usafiri, hazina vizuizi vya umri.

Katika basi, wanafamilia, ndugu, jamaa, baba, mama na watoto wa kike na wa kiume wanasafiri kwa pamoja. Miziki na picha za chafu mbele ya watu hao, ni ukatili na unyanyasaji usiopaswa kuvumiliwa, bali kukomeshwa.

Ndiyo maana Kama Mzazi nasema, mamlaka zinazohusika na wanajamii kwa jumla (abiria), waungane kuzuia uvurugaji huo wa maadili, mila na tamaduni zetu.

Utumbuizaji katika vyombo vya usafiri uzingatie uwepo wa watoto, wazazi, walezi na ndugu wa kike na wa kiume hivyo ili wasikwazwe kwa matashi ya madereva.

Ndiyo maana Kama Mzazi, natoa mwito kwa madereva na wamiliki wa mabasi yaendayo mikoani na yanayofanya safari za katika miji kwenda na kurudi kazini, yawe makini ili yasioneshe video, picha na mambo mengine yenye jumbe za ngono.