Kama Mzazi: Mafunzo yaanze uendeshaji bodaboda ufuate

USAFIRI wa kutumia pikipiki maarufu kama bodaboda kutoka eneo moja kwenda lingine mijini na vijijini unazidi kushika kasi ya umaarufu na kuwa moja ya njia za uhakika za vijana kujipatia ajira katika udereva wa vyombo hivyo huku wamiliki wa vyombo hivyo wakijipatia kipato.

Kama Mzazi, nimechunguza na kubaini kuwa, idadi kubwa ya madereva wa bodaboda ni vijana na wengine wakiwa wenye umri wa chini ya miaka 18 na ambao wengi huwakuwahi kupata mafunzo yanayostahiki kuendesha vyombo hivyo.

Kama Mzazi miongoni mwa wazazi wengine, nimebaini ukosefu wa mafunzo ya udereva na utoto kwa maana ya chini ya umri wa miaka 18, vimekuwa visababishi vikubwa vya ajali zinazohatarisha maisha ya watu, kuwatia wengine katika hali ya kuishi na ulemavu, pamoja na uharibifu wa mali.

Haya ni mambo yasiyopaswa kuachwa yaendelee kwa kuwa yanayochangia kuwapo kwa umaskini licha ya juhudi za serikali kupambana na umaskini kwa watu wake.

Utoto, ukosefu wa mafunzo ndiyo mambo yanayosababisha hata jana wakati wa Sikukuu ya Pasaka, wameonekana vijana wengi wakiendesha bodaboda kwa mbwembwe za kitoto, bila kujali kuwa wamebeba abiria na kadhalika, bila kujali usalama wao na mali walizo nazo.

Dosari hizo za utoto, ukosefu wa mafunzo ya uendeshaji pikipiki na uzembe hasa wa ukiukaji kanuni na sheria za usalama barabarani kwa baadhi ya madereva wa bodaboda, ni mambo ambayo jamii nzima haina budi kuungana kuyakemea tangu familia, abiria, wamiliki wa vyombo vyote vya usafiri, madereva wenyewe na mamlaka za kisheria likiwamo Jeshi la Polisi.

Mara nyingi, jamii inashuhudia namna vijana wetu wanavyochezea maisha wakati wakiendesha pikipiki hizi kwa mzaha na utoto utoto hali inayowagharimu wao, na watumiaji barabara wengine, bila kuziacha nyuma familia zao.

Kama Mzazi, inaniuma kuona baadhi ya madereva hao wakiendesha kwa mwendo wa kutisha, wakiyapita magari na kufanya ushindani usio na tija bila kujali kanuni na sheria za usalama barabarani.

Hii ni pamoja na wengi wao kutotambua kuwa barabarani wapo watumiaji wengi hivyo, kuwa na utaratibu sahihi wa utumiaji barabara sambamba na vyombo hivyo.

Hata hivyo, licha ya juhudi kubwa zinazoendelea kufanywa na Jeshi la Polisi huku abiria wengi wakianza kupata mwamko sahihi wa kutokubaliana na ukiukaji wa kanuni na sheria za usalama barabarani, bado katika maadhimisho ya kuteswa, kufa na kufufuka kwa Yesu Kristo (Pasaka) yanayoendelea hadi leo, bado utoto na uzembe huo, unaendelea kufanywa na baadhi ya bodaboda.

Vijana hawa wamekuwa na kasumba ya kudharau hata alama za barabarani na ishara za askari hasa wanapokuwa katika taa za kuongozea magari na kujaribu kuonesha kama kwamba, sheria za usalama barabarani haziwahusu.

Taarifa ya Jeshi la Polisi, Kikosi cha Usalama Barabarani zinasema mwaka 2016, ajali za bodaboda zilisabaisha vifo vya watu 820 na majeruhi 1,998 huku wengine wakiachwa yatima, wajane na wagane.

Kama mzazi, nitumie fursa hii kuipongeza Serikali kwa kupiga marufuku uzalishaji, uuzaji na utumiaji wa pombe maarufu kama viroba kwani tangu kuanza kwa zuio hilo, taarifa za watu na mamlaka mbalimbali nchini, zinabainisha kuwapo upunguffu wa ajali hasa zinazohusisha bodaboda.

Umefika wakati wamiliki wa vyombo vya usafiri hasa bodaboda, kuunganisha nguvu na Jeshi la Polisi na serikali za mitaa husika, kuwa na sheria kali zinazowabana waendesha bodaboda wasiozingatia sheria na kanuni za usalama barabarani.

Kwa mfano, vituo vya bodaboda ambavyo naamini vyote vina uongozi rasmi, inapobainika kuwa mmoja wa wanachama wa kituo husika cha bodaboda hakidhi vigezo aidha kwa kutokuwa na umri unaokubalika au mafunzo, basi uongozi huo nao uwajibishwe kwa kumruhusu kujiunga nao na kumsajili.

Kadhalika, serikali za mitaa zihusishwe zaidi katika usajili wa madereva katika vijiwe. Kwamba, usajili wa vijiweni (vituo vya bodaboda), pamoja na mambo mengine, uambatane na barua toka serikali za mitaa ili wanapobainika kinyume, uongozi ulioshiriki kuthibitisha nao uwajike.