VIJANA: Tuwe waaminifu katika kazi zetu

NIAJE watu wangu! bilashaka mambo yanaenda vyema na Mungu anatupigania kila siku iitwayo leo na kutuwezesha kupata mkate wetu wa kila siku kwa namna moja au nyingine. Nawapongeza vijana wenzangu wote ambao mwaka wameuanza vyema kwa kutekeleza ipasavyo majukumu yao ya kijamii, familia na hata kitaifa.

Ndio! Katika hili lazima tupongezane maana kila mtu analia na mwezi Januari, huyu anafukuzana na karo za shule za watoto, ndugu na jamaa, na yule anafukuzana na kodi ya pango la nyumba au sehemu ya biashara yake.

Big up sana kwa wale ambao wamefanikisha hilo na sasa watoto au familia zao zinaishi kwa amani. Hakuna kitu kibaya kama kushindwa kulipa kodi ya nyumba kwa wakati halafu unaona simu ya mwenye nyumba wako ambaye siku mbili zilizopita alikwambia…”kijana! Nakupa siku tatu ulete fedha yangu hapa au uhame.”

Haya Mungu mwema hayo tuyaache na nimerudi kwa kile ambacho ninahamu ya kuwaambia hii leo vijana wenzangu na nimeona niseme kabla sijafika katika mstari wa kuuacha ujana na kuingia rika la uzee.

Vijana wenzangu tulio maofisini, mashambani au katika ajira mbalimbali zilizo rasmi na zisizo rasmi, tuzingatie sana kitu uaminifu kwa dhamana tuliyopewa katika ngazi mbalimbali za kijamii, familia na hata kitaifa.

Hivi karibuni mtaani kwangu kuna vijana walikula shavu la kufyatua matofali kw aajili ya ujenzi. Vijana wale walipewa dhamana na kufanya kazi vyema na kuikamilisha huku mwenye mali akiwepo.

Baada ya kupita juma moja zile tofali kukauka vizuri walipewa jukumu la kuzipanga ili uwanja ule uchimbwe msingi na ujenzi uanze. Vijana wale walianza kufanya kazi ile majira ya jioni wakati jua limepoa.

Kazi ilianza huku vijana wakijisimamia wenyewe, na ilipofika giza limeingia vijana wale wakaanza kubeba baadhi ya matofali yale katika mkokoteni na kuyapeleka kusikojulikana. Nidhahiri kuwa vijana wale walikuwa wakienda kuyauza matofali yale.

Na huo ni wizi wa kuaminika na ni kosa kubwa ambalo linatukabili vijana wengi. Sasa leo unapewa dhamana ndogo kama hiyo ya kupanga tofali halafu unaziiba, je kesho ukipewa dhamana ya kusimamia ujenzi wa nyumba husika, si unaweza iba vifaa vya ujenzi vyote na kusababisha hasara kwa mwenyenyumba.

Nashauri vijana tuwe waaminifu tukipewa kazi tuzifanye vyema ili kesho tena tupewe kazi na kufanya maisha yetu kuwa rahisi.