HAYA NDIO MAISHA: Wazazi tuwe makini na malezi ya watoto

WAPENDWA wasomaji wetu habari za Jumapili, ni matarajio yangu wote hamjambo kwa neema ya Mungu aliyetupa uhai wa kuiona tena siku njema ya leo. Naomba nianze kwanza kwa kuwapa pole wazazi waliopoteza watoto wiki iliyoisha kutokana na kujifungia ndani ya gari.

Ni jambo la kusikitisha na kuhuzunisha kwa wazazi waliopenda watoto wao na kisha kuwapoteza ghafla, hasa ukizingatia kilichowaondoa ni chombo kinachomilikiwa na mzazi, inaumiza sana.

Hakuna jinsi ya kuwarudisha zaidi ya kushukuru kwa kila jambo kama Neno linavyosema, tumshukuru Mungu kwa kila jambo, limeshatokea na hakuna wa kurudisha uhai wa watoto hao.

Napenda kuwapa pole wazazi waliopoteza watoto hao na kuwaombea kwa Mungu awape faraja, maana ni jambo zito na gumu kulimeza kama wanadamu lakini kwa neema ya Mungu yawezekana.

Tukio hili ndio limenigusa leo na kunisukuma kuamua kuandika jambo ama kutaka kukumbusha wazazi juu ya umakini katika kuwalea watoto wetu. Unajua watoto hasa wakiwa wadogo ni wadadisi sana, wajanja sana na wengine husema watoto ni watundu. Mimi sitaki kukiri hili la watoto watundu maana maneno huumba ila niseme tu watoto huwa ni wadadisi kupitiliza.

Ukifuatilia tukio la watoto wale waliopoteza maisha kwa kujifungia garini, unaona mzazi aliweza kuwaona na kuwafukuza, lakini kimya kimya walirudi tena wakaingia ndani ya gari, masikini mzazi kwa sababu alishawafukuza hakujua na kuwafungia hadi walipotafutwa ndio wakaonekana.

Kwa mzazi huyu siwezi kusema alikuwa mzembe au alifanya kosa, maana hakika hakuwaona tena. Lakini sasa tukio hili litufumbue macho wazazi na walezi, kwamba watoto huwa ni wajanja na wadadisi na hakika wanapenda michezo, hawajui kama ni hatari au salama, lakini kile kinachowasukuma kufanya kwa wakati wao hufanya.

Kwa mantiki hiyo, mzazi, mlezi au wale wanaokuwa ama kubaki na watoto ni vyema wakati wote kukaa na tahadhari, hakikisha kila sekunde unajua mtoto au watoto wako wanacheza wapi, na nani na sehemu gani.

Kuna baadhi ya wazazi au walezi hawana muda, yaani mtoto akishaamka, akanywa chai akatoka kucheza, yeye hana hata habari anaridhika kabisa kuwa mtoto yuko nje anacheza.

Unaweza kukuta mtoto yuko mtaa wa tatu huko anakatiza, yaani mzazi au mlezi hana hata habari, hajui anacheza na nani au anacheza michezo gani, ukimuuliza anakujibu bila wasiwasi yuko huko anacheza na wenzake!’ Hebu wazazi, walezi na jamii kwa jumla tuwajibike katika kuwalea watoto kwa vitendo ikiwa ni pamoja na kufuatilia alipo, anacheza wapi na nani?

Siku hizi kuna matukio ya ajabu, watu wazima wamekuwa na akili za uovu, watoto wanafanyia vitu vya ajabu na watu wasiowajua na wengine ni watu wanaowafahamu kabisa, sasa likimkuta mwanao utamlaumu nani?

Mwito kwa wazazi na walezi na jamii kwa ujumla kuwa ni wajibu wao kuwatunza na kuwalinda watoto wakati wote, usiridhike kuwa mtoto anacheza nje, usichoke kumfuatilia ili kuepuka majanga ambayo asilimia kubwa kama ungekuwa makini ungeweza kumuokoa mtoto au watoto. Jumapili Njema.