TUKUBALIANE KUTOKUBALIANA: Mashetani wanaoishi kama malaika tunazidi kuwaona

NI Watanzania wenzetu, watoto wa wakulima wa nchi hii na wengi wao ni wale waliosomeshwa bure kwa kodi za walalahoi.

Nchi iliwaamini, ikawapa majukumu makubwa ya kusimamia rasilimali zetu ili ziwe sababu ya kutuondoa kwenye lindi la umaskini, ziwe sababu ya kutoa elimu bora kwa watoto wetu, kutupa maji salama, kutujengea barabara, kutupa huduma za afya bora na kadhalika na kadhalika, lakini wakageuka kuwa shetani ili eti waishi kama malaika.

Rais John Magufuli aliposema kwamba Watanzania wengi wanaishi kwa taabu sana, wakati kuna wenzao wachache wanaishi kama malaika na sasa anataka waishi kama mashetani, wengi walibaki wanamshangaa.

Bila shaka, mbali na hatua alizokwisha chukua huko nyuma kama vile kudhibiti ukwepaji kodi bandarini na baadhi ya maofisa wa ngazi za juu kufukuzwa kazi na kuchunguzwa au kufikishwa kortini, lililotokea wiki iliyopita sasa linasadifu kila alichokisema.

Kauli kwamba anataka ‘malaika’ hawa waishi kama ‘mashetani’ ililenga kumaanisha kuwasaka waliko, kuwaondoa kwenye nyadhifa zao na kisha wagharimie makosa ya ushetani wao. Kwamba, hilo halifanyi kibabe, bali kisayansi ikiwemo kuunda kamati za uchunguzi kama ile ya Mruma.

Bila kumuonea mtu, ni vyema na haki kabisa sasa vyombo vya dola vikachukua hatua muhimu ya kuchunguza utajiri wa wote wanaotuhumiwa kwa ufisadi na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria.

Kwamba kama tulikuwa kila siku tunashughulika zaidi na “vijizi vya kuku na bata” mitaani au wezi wa viatu misikitini na vibaka wanaoiba hata chupa za chai nyumbani, sasa tushughulike na “majizi papa”, yanayosababisha uduni wa maisha kwa Watanzania kwa sababu ya ubinafsi wao, unyang’au wao na uchoyo wao.

Kwamba nyang’au hawa hawaguswi kabisa na umasikini na matatizo ya Watanzania wengi, alimradi wanatumia nafasi zao kushirikiana na wawekezaji wasio waaminifu kuinyima serikali mapato sasa iwe mwisho.

Kamati ya watalaamu wanane iliyoundwa na Rais John Magufuli imekuja na majawabu ambayo bila shaka yamewaweka vichwa chini wale waliojaribu kupinga na hata kukejeli agizo la Rais la kusimamisha usafirishaji wa makinikia (mchanga wa dhahabu) nje ya nchi.

Hawa jamaa, kama alivyosema Rais Magufuli kwamba hii ni vita, bado wako vitani wakitaka kuhakikisha tonge haliwatoki mdomoni na kujaribu kugeuza ukweli wa ripoti ya Kamati ya Mruma.

Na pia inasemekana wanataka kukimbilia kwenye mahakama za kimataifa ili waendelee kunyonya na kama ndivyo huu ndio wakati wa kujiondoa kwenye uanachama wa mahakama hizo kama zitakaa upande wa wezi na wanyonyaji.

Lakini kinachovutia ni kwamba wananchi wengi wako nyuma ya Rais John Magufuli na insha-Allah, Mungu pia hatokuwa upande wa wezi na wanyonyaji hao. Kwamba nchi yetu imekuwa ikipoteza mrabaha unaotokana na usafirishaji wa makinikia yenye thamani ya takribani Sh bilioni mia nane (dhahabu na madini mengine) hadi zaidi ya trilioni moja kila mwezi, ni jambo linalotoa machozi kwa mzalendo wa kweli wa Tanzania.

Hii ni kutokana na kauli ya Rais kwamba, ingawa tume nyingine aliyounda kuchunguza kadhia hiyo haijatoa mchanganuo halisi wa kiasi ambacho taifa limepoteza kwa muda wote, lakini makontena zaidi ya 200 yaliyojaa makinikia yamekuwa yakisafirishwa kila mwezi nje ya nchi.

Kwa lugha nyingine, kama serikali ikiweza kujenga kiwanda cha kuyeyushia makinikia hayo hapa Tanzania na kuyamiliki, basi kiwango hicho pekee ni takribani sawa na kodi inayokusanywa kila mwezi kutoka vyanzo lukuki! Kinachofikirisha sana ni kugundua kwamba vyombo tulivyoviweka kwa ajili ya kusimamia eneo hili, vimekuwa vikituangusha tangu usafirishaji wa makinikia nje ya nchi uanze kufanyika mwaka 1998.

Wakati Rais anaendelea kuchukua hatua nzuri na kusubiri ushauri wa kamati nyingine alizoziunda kuchunguza suala hili, ninashauri nchi yetu ianze kuangalia upya sheria za madini na sheria za kodi.

Ninamaanisha kwamba wakati sakata hili la makinikia linagusa zaidi uzembe na rushwa na hivyo kutoa nafasi kubwa ya usimamizi mbovu, bado kuna maeneo mengine ‘tunapigwa’ na wajanja kutokana na sheria zetu, mitazamo yetu na hata mikataba tunayoingia.

Imekuwa ikielezwa kwa mfano, kwamba baadhi ya sheria zetu zimekuwa zikitoa upenyo mkubwa kwa wawekezaji kujichotea rasilimali zetu na hivyo kutokuwepo kwa mazingira ya “mimi nipate na wewe upate”.

Kwamba baadhi ya sheria zinatoa muda mwingi kwa wawekezaji kutolipa kodi kama kivutio, lakini katika matumizi ya teknolojia za kisasa, mwekezaji anaweza kutumia muda mfupi kuchimba madini na kuondoka nayo huku akidai bado anayatafuta au hajapata faida na hasa kunapokuwa na usimamizi mbovu kama tuliouona kwenye makinikia!

Mwanasheria na Mkurugenzi wa Chama cha Wanasheria Watetezi wa Mazingira Tanzania (LEAT), Dk Nshala Rugemeleza, alikaririwa katika makala yaliyotoka katika gazeti hili Jumatano iliyopita akisema kwamba ili kukwepa kulipa kodi baadhi ya kampuni zimekuwa zinatumia mbinu ya kukopa kwa asilimia 100, hivyo kuonekana kama hawapati faida.

Si vibaya pia tukaangalia ushauri ambao umekuwa ukitolewa na Zitto Kabwe kama unatufaa. Kwamba ifikie mahala umiliki wa madini ubaki kuwa wa serikali na hawa wanaoitwa wawekezaji katika sekta hiyo, wabaki kuwa wakandarasi, walipwe kwa ukandarasi wao kutokana na mikataba itakayowekwa wazi, basi.

Katika muktadha huo wa sheria, wengi wamekuwa wakishangaa jinsi zisivyowatendea haki Watanzania kwani Mtanzania, kwa mfano, akimuuzia kampuni mwekezaji kutoka nje kampuni haitozwi kodi, lakini kampuni hiyo hiyo akiuziwa Mtanzania, kampuni inatozwa kodi.

Lingine la msingi ambalo Serikali imekuwa ikishauriwa kwa muda mrefu ni mikataba yote kwamba, kabla haijasaniwa, iwekwe hadharani ili Watanzania waone kilichomo ndani ya mikataba hiyo na kutoa mapendekezo yao. Swali ambalo halijawahi kujibiwa na kushibisha akili ni kwa nini mikataba inayohusu raslimali za Watanzania iwe siri.

Sambamba na hilo la mchanga wa dhahabu, ni vyema serikali ikanyoosha mambo pia katika madini ya Tanzanite na kuangalia jinsi madini hayo yanayopatikana nchini mwetu pekee yatakavyotunufaisha kuliko ilivyo sasa.

Takwimu zilizotolewa hivi karibuni na Dk Rugemeleza wa LEAT zinaonesha kwamba kampuni ya Tiffany ya Marekani inayonunua Tanzanite kwa wingi, inapata wastani wa Dola za Kimarekani kati ya milioni 500 hadi 600 kwa mwaka wakati Tanzania inapata Dola za Kimarekani kati ya milioni 13 hadi 16 tu.

Dk Rugemeleza anakariri ripoti ya mwaka 2013 ikionesha kuwa Tanzania ambayo ndiko Tanzanite inachimbwa, iliuza nje ya nchi madini hayo kwa thamani ya Sh bilioni 45 mwaka huo lakini Kenya ambayo haina Tanzanite iliuza nje ya nchi madini ya Tanzania yenye thamani ya Sh bilioni 173.

Hapo bila shaka kuna mashetani wanaoishi kama malaika. Kulingana na ripoti hiyo, nchi ya India iliuza madini ya Tanzanite yenye thamani ya Sh zaidi ya bilioni 500 mwaka huohuo, hali iliyosababisha baadhi ya wanunuzi wakubwa wa madini hayo kudhani kwamba madini ya Tanzanite yanachimbwa nchini India!

Ndipo Dk Rugemeleza anasema kutokana madini ya Tanzanite kupatikana Tanzania pekee, haoni kwanini nchi yetu ambayo ndio ‘Mungu’ wa Tanzanite isiamue kuanzia sasa kwamba hatua zote za uchimbaji hadi utengenezaji wa bidhaa zinazotokana na vito hivyo vya thamani zifanyikie Tanzania pekee.

Kwamba kwa hatua hiyo, kampuni kama Tiffany haziwezi ‘kupindua’ kwani hazitakuwa tayari kukubali kuanguka kibiashara kama tutatishia hata kufunga uzalishaji wa Tanzanite.

Hatua hii itakuwa muhimu sana kwani itawahakikishia Watanzania ajira kupitia kiwanda au viwanda vya Tanzanite vitakavyojengwa nchini na kuchangia kwenye ‘Tanzania ya Viwanda’ kuliko ilivyo sasa ambapo ni Wahindi na Wamerakani ndio wanaonufaika na viwanda vinavyotakana na bidhaa za Tanzanite.

Kwa lugha nyingine, Dk Rugemeleza anaamini kwamba wakati hatuwezi kuwa ‘Mungu’ wa madini mengine yanayopatikana kwingineko pia kama almasi, dhahabu, ruby na kadhalika, kwenye Tanzanite tunaweza.