JICHO: Nchi yangu kwanza

WIZARA ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo kwa kushirikiana na taasisi zake imetangaza kampeni ya kitaifa ya uzalendo.

Kampeni hiyo imelenga kuhimiza uzalendo na utaifa katika taifa kama alivyokaririwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe hivi karibuni.

Kwa mujibu wa Waziri Mwakyembe, wizara inaona ni muda muafaka sasa kuonesha njia sahihi ya kujenga nchi kwa kuimarisha uzalendo na utaifa kama ambavyo Rais John Magufuli amekuwa akiwahimiza Watanzania.

Chini ya kampeni hiyo, panahitajika kutoa elimu kwa vijana wajue nchi ilikotoka na inakokwenda. Hatua hii inazingatia ukweli kwamba vijana wengi waliozaliwa baada ya uhuru wamekuwa wakiuliza mara nyingi maana ya uzalendo.

“Na vijana hawa ndio ambao tunatarajia waongoze nchi katika karne hii,” anasema Dk Mwakyembe. Katika kitabu cha Kampeni ya Uzalendo na Utaifa; “Nchi Yangu Kwanza”, uzalendo unaelezewa kuwa ni hali ya mtu kuipenda sana nchi yake kiasi cha kuwa tayari kufa kwa ajili ya kuitetea.

Kwa upande wa utaifa, ni jumla ya mambo yote ya kijamii, kiuchumi, kisiasa na kisheria yanayowaunganisha watu kuwa nchi moja. Kitabu hicho kilichoandaliwa na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa kushirikiana na Kikundi cha Sanaa cha Mpoto na vikundi vingine vya utamaduni, sanaa na ubunifu, kinaweka bayana historia ya uzalendo.

Katika kitabu hicho kilichopigwa chapa na Tanzania Standard (Newspapers) Limited, inaelezwa kuwa historia ya uzalendo ilianza wakati wa kupigania uhuru wa nchi ambapo mababu walipigana uso kwa uso na wakoloni kukataa kutawaliwa kwa nguvu na kuchukuliwa rasilimali zao.

“Katika harakati hizo, wazee wetu hao waliuawa kwa kunyongwa au kupigwa risasi wakati wengine walifia magerezani,” sehemu ya kitabu inaeleza. Kinamtaja Chifu Mkwavinyika Munyigumba Mwamuyinga (Mkwawa) aliyejipiga risasi hadi kufa kwa kukataa fedheha ya kutawaliwa na wakoloni.

Aidha ipo orodha ya baadhi ya wapiganaji wa awali walionyongwa na wakoloni kwa kukataa kutawaliwa ambao ni Omari Makunganya, Isike na Machemba. Malkia Kundenda wa Tunduru na Bibi Leti wa Ughandi (Singida) pia walivamiwa na kuuawa na vikosi maalumu vya jeshi la Wajerumani.

Wazalendo wengine wanatajwa kuwa waliendelea na mapigano ya silaha dhidi ya wakoloni katika vita ya majimaji. Baadhi ya viongozi wa vita hiyo ni Kinjekitile Ngwale, Selemani Mamba na Kibasila ambao walinyongwa.

Mkoani Ruvuma, jumla ya mashujaa wa vita vya majimaji wapatao 68 wakiwemo machifu (Nkosi), wasaidizi wa machifu, wajumbe na wananchi, walinyongwa na kuzikwa katika kaburi la pamoja; mmoja wao akiwa mwanamke shupavu Nduna Nnkomanile wa Lugongolo (Kitanda).

Inaelezwa kwamba kabla ya kunyongwa kwa mashujaa hao wa majimaji, kiongozi wa Manduna, Mpambalyoto Soko alisema: “mnatuonea sisi, mtakuja kupambana na watoto wetu nao watawafukuza katika nchi hii…”.

Wakati ikiwa imepita miaka zaidi ya 100 tangu mashujaa hawa wapoteze maisha kwa ajili ya kupigania utu na uhuru wa taifa, swali linalojitokeza ni je, kwa kiasi gani Watanzania wamerithi uzalendo wa mashujaa hao wa kihistoria?

Katika kujibu swali hili, suala la utandawazi linatajwa kuwa na athari kutokana na kuwepo mmomonyoko wa maadili unaochangiwa na mwingiliano kijamii, kiuchumi na kiutamaduni unaochochewa na maendeleo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama).

Kampeni ya Uzalendo na Utaifa (Nchi Yangu Kwanza) itakayozinduliwa Desemba 8 mwaka huu ambayo itakuwa endelevu, pamoja na masuala mengine, inaangalia suala zima la mmomonyoko hasa kwa vijana,.

Kupitia kitabu hicho cha wizara inaelekeza kuchukua hatua za makusudi kuelimishana, kukumbushana na kuhuisha tunu za taifa kwa ujumla. Kwa hiyo kampeni imelenga kuhamasisha uzalendo na utaifa miongoni mwa Watanzania kupitia vyombo vya habari, matamasha, kazi za sanaa na mihadhara.

Kampeni itatumia pia elimu ya darasani, sanaa za maonesho na njia zingine za Tehama kujenga na kuimarisha uelewa wa vijana kuhusu utamaduni, sanaa, mila na desturi. Aidha, kampeni itaandaa majukwaa ya majadiliano kila mwaka kuhusu tunu za taifa, historia yetu, ulinzi na ukuzaji wa utamaduni wetu.

Matarajio ni kwamba, kampeni italeta matokeo chanya ikiwemo kurejesha/kuimarisha moyo wa uzalendo na utaifa kwa Watanzania. Kampeni itakuwa ikifanyika kila Oktoba kama sehemu ya maadhimisho ya kifo cha Baba wa Taifa, Julius Nyerere.

Chini ya kampeni hiyo, Watanzania kama taifa moja wana wajibu wa kurithisha kizazi cha sasa yale wanayoyajua ya nyuma ili kuliimarisha taifa kuwa moja na lenye msimamo mmoja; litakaloleta faida kwa Watanzania wote kwa misingi iliyojengwa na waasisi.

Kama alivyosema Mkurugenzi Maendeleo ya Sanaa, Leah Kihimbi wakati wa kutangaza kampeni hii jijini Dar es Salaam, Watanzania hawana budi kuthamini nchi yao kwa kuendeleza kaulimbiu ya ‘Nchi Yangu Kwanza.’

Naye Katibu Mtendaji Bodi ya Filamu, Joyce Fissoo anasisitiza kwamba kila Mtanzania anapaswa kujiona ni wa kwanza katika kuhakikisha dhana sahihi ya uzalendo inawafikia Watanzania wote na kujiweka katika nafasi ya kutambua kuwa anakwenda kuokoa kizazi cha sasa na kijacho.

Hii ni pamoja na kuhakikisha vizazi hivyo vinakuwa wazalendo, wanakuwa katika maadili na wanaepuka mmomonyoko wa maadili unaoletwa na maendeleo ya sayansi na teknolojia.

Ni dhahiri kuwa kaulimbiu ya ‘Nchi Yangu Kwanza’ ikitawala mioyo ya Watanzania huku wakirejelea historia ya mashujaa waliopigania utu na uhuru wa taifa, uzalendo na utaifa utakuwa sehemu ya maisha yao kiuchumi, kisiasa, kiulinzi, kiutamaduni na kijamii.