Yanga, Azam fanyeni kweli

WAWAKILISHI wa Tanzania katika michuano ya kimataifa, Yanga na Azam leo na kesho watakuwa na kibarua cha kumenyana na Zanaco ya Zambia na Mbabane Swallows ya Swaziland.

Mabingwa wa soka bara, Yanga wataivaa Zanaco leo kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam ikiwa ni mechi ya awali ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Azam kesho ikitarajiwa kuikaribisha Mbabane kwenye Uwanja wa Azam Complex Chamazi katika mechi ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Yanga ilifuzu hatua hiyo kwa ushindi wa jumla ya mabao 6-1 dhidi ya Ngaya ya Comoro, huku Azam ikianza moja kwa moja hatua hiyo.

Kwa takriban wiki nzima hii timu hizo zimekuwa kwenye maandalizi kwa ajili ya mechi hizo na kwa nyakati tofauti makocha wake wamejinasibu vikosi vyao kuwa vizuri kwa mapambano.

Lakini pia mbali na maandalizi hayo, timu hizo bado zipo kwenye michuano ya Ligi Kuu na ile ya Kombe la Shirikisho ‘FA’ zikifanya vizuri kwa maana hiyo, wachezaji wake bado wapo kwenye hali ya mapambano kutokana na miili yao kutoka kucheza mechi hivi karibuni.

Tunaamini kwa mazingira hayo timu hizo zitafanya vizuri katika mechi zake na hivyo kusonga mbele kama ilivyo matamanio ya watanzania wengi. La muhimu ni kwa wachezaji wa timu hizo kutoingia uwanjani kwa dharau dhidi ya wapinzni wao wakidhani watazifunga kirahisi.

Tunazikumbusha Yanga na Azam kwamba mpira una mambo mengi na lolote linaweza kutokea, hivyo ni wajibu wao kucheza kwa tahadhari na kumaliza kazi nyumbani ili wakienda ugenini iwe rahisi kumaliza kazi.

Hatuna shaka kwamba mabenchi ya ufundi ya timu hizo yamewapa mafunzo ya kutosha wachezaji wao na hivyo watanzania watarajie kufurahi, badala ya kununa kila msimu kwa timu zao kufanya vibaya kwenye michuano ya kimataifa.

Aidha, tunatoa angalizo kwa mashabiki wa pande zote kuziunga mkono timu hizo kwani zinawakilisha nchi.

Mtindo wa kuingia uwanjani na kushangilia timu pinzani tunaamini umepitwa na wakati hasa katika wakati huu ambao Tanzania inapambana kupata mafanikio kwenye mchezo huo wa mpira wa miguu unaopendwa na wengi.

Kila la kheri Yanga na Azam, malizeni mchezo mapema.