Vyakula visivyofaa kwa matumizi vidhibitiwe

KATIKA ukurasa wa 3 wa gazeti hili toleo la jana, kulikuwa habari iliyohusu Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA) kushikilia tani 100 za mchele kutoka Pakistan ikisema, “Tani 100 za mchele zashikiliwa Dar.”

TFDA ndiyo iliyotoa taarifa ikithibitisha kushikilia shehena hiyo ambayo hadi jana, ilikuwa haijafahamika kama ni salama kwa matumizi ya binadamu, au hapana.

Hata hivyo, Meneja wa TFDA Kanda ya Mashariki, Emmanuel Alphonce, mchele huo uliokamatwa kwenye ghala moja huko Majumbasita, Ukonga Dar es Salaam, ulikuwa na nembo inayoonesha kuwa, mwisho wa matumizi yake ni Oktoba mwaka huu, licha ya kudaiwa kuwa uliingizwa nchini miaka mitatu iliyopita na kwamba haukuwa umeuzwa mpaka sasa.

Katika kutilia shaka usalama wa mchele huo, kwa sasa umezuiliwa kusambazwa kwenda kwa walaji. Tunalipongeza Jeshi la Polisi kwa kutilia shaka bidhaa hiyo na hata kutoa taarifa kwa mamlaka husika ya udhibiti wa chakula na dawa ambayo imechangamka kufuatilia taarifa na vipimo vya mchele huo.

Sisi tunasema hiyo ni hatua nzuri kwani mara kadhaa tumekuwa tukishuhudia bidhaa ya vyakula vibovu au ilikwisha muda wa matumizi ikiendelea kuingizwa sokoni na kuuzwa bila kujali afya za watumiaji.

Hii ni kwa kuwa wafanyabiashara wengi wana kasumba ya kuangalia na kujali zaidi faida itokanayo na bidhaa wanazouza, kuliko usalama wa watu jambo ambalo ni hatari kwa umma.

Wakati tukiwapongeza TFDA na Jeshi la Polisi kwa kutilia shaka na kufuatilia ukweli kuhusu usalama wa mchele huo, tunatumia fursa hii kuziomba mamlaka hizo kutoishia hapo.

Tunasema, Mamlaka ziongeze kasi ya msako na ukaguzi wa mara kwa mara katika maghala yanayohifadhi bidhaa na kwenye maduka ili kuhakikisha tabia ya baadhi ya wafanyabiashara kuwalisha Watanzania vyakula na bidhaa zisizo na ubora inakoma.

Wafanyabiashara wote wajiulize kuwa, endapo watawalisha wateja wao sumu na kuangamiza afya na maisha yao, watamuuzia nani bidhaa zao.

Kimsingi, wafanyabiashara wanapaswa kubadilika katika hili. Wananchi kwa upande wao, wajenge utamaduni wa kuchunguza tarehe za kumalizika muda wa matumizi wa bidhaa wanazonunua na unapogundulika utata kuhusu ubora na muda wa matumizi, watoe taarifa kwa mamlaka husika ili hatua stahiki zichukuliwe.

Jamii isifanye kosa la kuacha jukumu hilo kwa Polisi na TFDA pekee kwani hiyo itachukua muda mrefu kupambana na hatimaye kuwashinda wahuni hao wanaohatarisha afya za watu.

Tunasema, ulinzi wa afya za wananchi unapaswa kuwa hasa jukumu la kila mmoja, kwa kuwa vyakula visivyofaa ni hatari kwa binadamu.