Ushirikishaji wadau katika shughuli za maendeleo upewe kipaumbele

MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, jana alizindua rasmi barabara kutoka Shimo la Udongo, EPZD hadi Kilwa, yenye urefu wa kilometa moja katika Manispaa ya Temeke, ambayo imejengwa kwa zege.

Ni barabara yenye shughuli nyingi, kwani barabara inayokwenda pia bandarini, inapita pia kwenda eneo la uwekezaji lakini pia barabara hii hutumiwa na wananchi wengi.

Hivyo, kukamilika kwake hakuna shaka kwamba ni ukombozi wa uhakika kwa watumiaji wake. Kabla ya ujenzi huo, barabara hii ilikuwa kero kutokana na kuwa na mashimo makubwa mithili ya mahandaki, hivyo kusababisha foleni kubwa zilizochelewesha shughuli nyingi kwa watumiaji wake.

Hivyo tunachukua fursa hii kumpongeza Mkuu wa Mkoa kwa kuona ubovu wa barabara hiyo, na hivyo kubeba jukumu la kuiomba kampuni ya kizalendo ya Grand Tech Ltd iangalie uwezekano wa kusaidia ujenzi wa barabara hivyo.

Aidha, tunaipongeza kampuni hiyo kwa uzalendo wake wa kubeba jukumu hilo na kukamilisha ujenzi kwa gharama ya Sh milioni 350, bila kuiomba hata senti moja kutoka serikalini.

Aidha, imejenga barabara bora, yenye uwezo wa kutumika kwa muda mrefu tofauti na zile zinazojengwa na wakandarasi wanaotafuna fedha za walipakodi, lakini wakijenga barabara zisizolingana na thamani ya pesa wanazolipwa.

Hakika uzalendo wa Grand Tech ni wa aina yake na unaopaswa kupigiwa mfano kwa wawekezaji wengine, ama wa ndani au wa kigeni. Tunaamini, nchi hii ina wazalendo wengi wenye nia ya kuisaidia serikali, pengine kinachokosekana ni uhamasishaji tu.

Kama imewezekana kwa kampuni ya Grand Tech, bila shaka wafanyabiashara wakubwa, kampuni na hata taasisi mbalimbali zikihamasishwa, zinaweza kushiriki kikamilifu kuondoa kero nyingi za miundombinu, ikiwamo ya barabara, afya, elimu na hata maji, badala ya kuisubiri serikali itoe kila senti kufanikisha shughuli za maendeleo.

Hata hivyo, tunadhani jukumu la ushawishi lisiachwe kwa viongozi aina ya Makonda pekee, bali kila mmoja katika eneo lake la utawala aangalie uwezekano wa kushirikisha wadau katika kufanikisha maendeleo katika maeneo yao.

Ni kwa njia hii, tunaamini kasi ya maendeleo itaonekana na hivyo kuondoa manung’uniko na kuililia serikali kila kukicha, wakati mwingine kwa vitu vidogo visivyohitaji nguvu na sauti kubwa.

Kama kila mmoja akitimiza wajibu wake, kazi ya kulifanyia maboresho Jiji la Dar es Salaam haitakuwa ngumu, na kwa upande mwingine, itasaidia wananchi kujikita katika shughuli zao za kiuchumi, badala ya kuhangaika na kero kila kukicha.

Ndiyo maana tunasema, kilichofanywa na Makonda, ingawa amefanya mengi katika Mkoa wa Dar es Salaam katika muda mfupi wa uongozi wake, anapaswa kuungwa mkono kwa kuwatafuta wadau wa maendeleo wenye dhamira ya kuisaidia nchi, kama walivyofanywa Grand Tech Ltd.