Tushirikiane pamoja kujenga reli ya kisasa

UBOMOAJI wa nyumba zilizo ndani ya mita 30 kila upande kwenye Reli ya Kati, umeanza tangu wiki iliyopita na utahusu kipande cha kutoka Dar es Salaam mpaka Morogoro.

Ubomoaji huo unafanyika chini ya ulinzi mkali wa Jeshi la Polisi wakiwa na gari za maji ya kuwasha.

Kazi hiyo inafanywa kutokana na ujenzi wa reli ya kisasa (standard gauge), ambayo inatarajiwa kuanza kujengwa hivi karibuni. Tayari serikali imekwishatia saini na mkandarasi, atakayejenga reli hiyo.

Hata hivyo, jambo la kusikitisha ni kuwa baadhi ya wananchi katika jiji la Dar es Salaam, wameanza kulalamika kuwa ‘bomoa bomoa’ hiyo inakiuka sheria.

Hata Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, nayo imesema imesikitishwa na kitendo kilichofanywa na Kampuni Hodhi ya Rasilimali za Reli Tanzania (RAHCO) kubomoa nyumba zaidi ya 200 zilizojengwa pembezoni mwa reli katika eneo la Buguruni jijini Dar es Salaam, Machi 11, mwaka huu.

Kwa mujibu wa gazeti hili toleo la jana, Mwenyekiti wa Tume hiyo, Bahame Nyanduga alisema RAHCO ilitekeleza ubomoaji huo, wakati ikiwa na taarifa ya mwito wa tume hiyo kuhusu malalamiko ya wananchi, wanaoishi jirani na reli hiyo.

Tunasisitiza kuwa wananchi na vyombo vingine,waache kabisa kuiandama RAHCO na Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano ili watekeleze mradi huo muhimu na nyeti kwa Taifa. Tuache kelele. Tuache malalamiko.

Tushirikiane pamoja kujenga reli hiyo ya kisasa. Tunaunga mkono kauli iliyotolewa juzi na msemaji wa Rahco, Catherine Moshi aliyesema ubomoaji huo umefuata taratibu zote na kwamba unafuata ramani na Sheria ya Mipango Miji ya mwaka 2007.

Kwa mujibu wa Moshi, kabla ya bomoa bomoa hiyo, gari limekuwa likipita na kutangaza katika maeneo husika, kuwaeleza wananchi ubomoaji ungefanyika.

Pia tunaunga mkono kauli ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, ambaye amekuwa akisisitiza mara kwa mara kuwa serikali imedhamiria kujenga reli hiyo ya kisasa, itakayoleta mageuzi makubwa katika usafirishaji na uchumi wa nchi.

Anasema reli hiyo ya kisasa ya kutumia umeme, treni yake itabeba tani milioni 17 kwa mwaka na itakwenda kilometa 160 kwa saa. Ujenzi wa reli hiyo utatekelezwa ndani ya miezi 30.

Awamu ya kwanza ya ujenzi itahusu kilometa 205 kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro na kilometa 95 za kupishana na kupangia mabehewa.

Pia, utahusu ujenzi wa miundombinu ya umeme, stesheni sita za abiria, nyingine sita za treni kupishana na wigo wa usalama wa kilometa 102.

Reli ya sasa ilijengwa kwa mara ya kwanza na Wajerumani ikiwa na uwezo wa kubeba tani milioni tano kwa mwaka. Ilikuwa na injini inayotumia mvuke hadi Wajerumani walipoondoka.

Waingereza walipokuja baadaye na kutawala Tanzania, walifanya marekebisho kwa kuweka injini inayotumia dizeli. Treni ya sasa ya kawaida, inaendeshwa kwa mwendokasi wa kilometa 30 kwa saa; na kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza inatumia saa 36.