Zanzibar yastahili pongezi kuanza kutafuta mafuta

KATIKA gazeti letu la jana kulikuwa na habari moja isemayo kuwa ‘Zanzibar yaanza kutafuta mafuta’.

Kwa mujibu wa habari hiyo, kazi ya utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi asilia Zanzibar, imeanza rasmi juzi kwa Kampuni ya Bell Geospace Enterprises Limited ya Uingereza, kufanya utafiti huo kwa niaba ya Kampuni ya Rak Gas ya Ras Khaimah.

Kuanza kwa kazi hiyo ni baada ya hatua ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Ali Mohammed Shein kutia saini Sheria ya Utafutaji na Uchimbaji wa Mafuta na Gesi Asilia, Novemba mwaka jana.

Uzinduzi wa utafiti huo ulifanyika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume mjini Unguja juzi na mgeni rasmi alikuwa Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Balozi Seif Ali Idd.

Tunapongeza kauli iliyotolewa na Makamu huyo wa Pili wa Rais, aliyesema kwamba utafiti huo unafungua milango katika rasilimali ya mafuta na gesi asilia.

Kuna watu walikuwa wakisema kwamba Zanzibar haitachimba mafuta, lakini sasa wananchi wenyewe wanashuhudia kazi imeanza.

Kwa mujibu wa Balozi Seif, serikali haifanyi mambo kwa kubahatisha na kwamba Zanzibar inaendesha utafiti huo wa kwanza kwa kutumia teknolojia ya kisasa ya utafutaji na uchimbaji wa mafuta.

Anawaasa wanasiasa, kuacha kuwapotosha wananchi juu ya suala zima la utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi asilia, kwamba suala hilo halihitaji ushabiki wa kisiasa.

Kwamba suala la mafuta na gesi asilia, sasa linasimamiwa Zanzibar moja kwa moja baada ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kufanya marekebisho ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 na kuliondoa suala hilo katika orodha ya mambo ya Muungano.

Chini ya marekebisho hayo, shughuli za uendeshaji wa mafuta na gesi asilia Zanzibar, zitafanywa kwa kusimamiwa na kuendeshwa kwa mujibu wa sheria za Zanzibar.

Kwa hakika, kazi hiyo ya utafiti wa mafuta na gesi asilia ni hatua muhimu katika uchimbaji wa mafuta, ambapo inaweza kuchukua miaka mitano kukamilika kwake.

Ni jambo linalohitaji muda, lakini yapo matumaini makubwa ya kufanikiwa kwa suala hilo. Tunawaomba wananchi wa Zanzibar, wawe na utulivu na wasiwe na hofu yoyote watakapoona ndege za utafiti wa mafuta na gesi, zikipitapita katika sehemu za bahari na nchi kavu.

Kwa mujibu wa Balozi Idd, ndege hizo huenda zitapita chini sana, kiasi cha mita 120 juu ya ardhi, lakini kwamba utafiti unaofanywa, hauna athari yoyote kwa binadamu na hata kwa wanyama na mimea.

Tunaunga mkono maoni yaliyotolewa na wataalamu mbalimbali wa uchimbaji mafuta, kwamba wana matumaini makubwa ya kufanikiwa katika utafiti huo.

Kwa hakika, tumevutiwa mno na maelezo ya Kiongozi wa timu ya watafiti kutoka Kampuni ya Bell Geospace Enterprises Limited ya Uingereza, Stefan Kuna, kwamba watatumia muda wa miezi mitatu, kufanya utafiti huo katika visiwa vya Unguja na Pemba.

Kwamba ndege yao ya utafiti, itakuwa ikiruka kila siku mapema asubuhi na itakuwa angani kwa muda wa saa sita, wakitafiti maeneo yote ya nchi kavu ya visiwa vikubwa na vidogo vilivyopo Zanzibar na Pemba na maeneo ya bahari, iliyozunguka visiwa hivyo.