Sasa kazi kwenu walimu na wanafunzi wa sayansi

TAARIFA kwamba Serikali imepokea vifaa vya maabara kwa ajili ya shule za sekondari nchini vyenye thamani ya shilingi bilioni 16.9 kuwezesha wanafunzi wa sekondari kusoma masomo ya sayansi kwa nadharia na vitendo, imeleta hamasa, faraja na matumaini makubwa kwa watoto na wadau wa maendeleo ya sayanasi na teknolojia nchini.

Vifaa hivyo vinatoka kwa mzabuni aliyeshinda zabuni iliyotolewa na Serikali, Kampuni ya Lab Equip.

Kaimu Kamishna wa Wizara ya Elimu, Sayansi,Teknolojia na Ufundi, Nicolas Buretta alifafanua katika hafla ya makabidhiano ya vifaa hivyo Dar es Salaam akisema, vitasambazwa katika shule za sekondari 1,696 zilizokwishakamilisha ujenzi wa maabara.

Tunafarijika zaidi kuelezwa kwamba kati ya shule zitakazonufaika na mgawo huo, 1,625 ni za kata na 71 ni shule za sekondari kongwe.

Sambamba na vifaa hivyo, Serikali imepitisha pia majina ya walimu 3,104 walioomba nafasi za kufundisha masomo ya sayansi ili kupunguza uhaba wa walimu katika masomo hayo.

Tunaungana na Watanzania wote wenye mapenzi mema na nchi hususani katika maendeleo ya elimu, kuipongeza Serikali ya Awamu ya Tano kwa kuchukua hatua hizo madhubuti na muhimu.

Sisi tunasema, tunapongeza kwani hatua hii ni kichocheo cha wanafunzi kujifunza na kuiva sawia ili kwenda sambamba na uhalisia wa maendeleo ya sayansi na teknolojia yanayopiga hatua kwa kasi duniani kwa kuchukua hatua za makusudi kuwaandaa wataalamu wetu kuanzia ngazi hiyo.

Hakuna ubishi kwamba nyumba yoyote imara huanza kujengwa na msingi imara. Katika mkakati huo, Serikali inaliweka taifa katika msingi imara utakaoliwezesha kupata wataalamu watakaoingia katika sekta mbalimbali za sayansi kwenye ngazi za vyuo na vyuo vikuu.

Hakika hili ni jambo la kupongeza kwani linaifanya Tanzania katika hali bora zaidi ya kuwa na wataalamu wake na hatimaye, kwenda na wakati kama ilivyo katika nchi nyingine zenye wataalamu wake wa ndani.

Kila Mtanzania hana budi kukumbuka kuwa, hakuna kitu bora kinachopatikana bila gharama, hivyo kwa kuwa tupo katika njia sahihi kwenda tunakotaka, ni wazi lengo la kuwapata wataalamu wetu wenyewe litatimia.

Tunawakumbusha walimu waliochaguliwa kuwanoa watoto katika masomo ya sayansi, watimize kwa kuzingatia na kutimiza wajibu wao huku wanafunzi nao wakipaswa kujifunza kwa bidii zaidi.

Tunasema, endapo kila mmoja kati ya walimu na wanafunzi atatimiza wajibu wake ipasavyo, lengo la Serikali kufanya jitihada hizo kupata wataalamu wa sayansi, litafanikiwa.

Ndiyo maana sisi tunasema, wote watakaotaka kujaribu kukwamisha juhudi na mafanikio haya ili Watanzania wasifikie kilele cha malengo yao, eti kwa sababu zao binafsi, wasipewe nafasi hiyo na pale watakapobainika, wafikishwe mbele ya sheria.