Kila la heri Jukwaa la Biashara Mwanza

LEO Mkoa wa Mwanza unaandika historia ya kuwa mkoa wa pili nchini kuwa mwenyeji wa Jukwaa la Biashara linaloandaliwa na Shirika la Magazeti ya Serikali (TSN), wachapishaji wa gazeti hili (HabariLeo), Daily News na SpotiLeo kwa kuushirikisha mkoa husika.

Jukwaa la biashara hutumiwa na wadau mbalimbali wa maendeleo kwa kuwasilisha mada kuhusu namna ya kuboresha biashara, fursa mbalimbali zilizopo na namna ya kuzitumia fursa hizo kwa ufanisi.

Jukwaa la kwanza lilifanyika mkoani Simiyu Februari mwaka huu ambako washiriki takribani 160 walipata wasaa wa kusikiliza mada mbalimbali zihusuzo namna ya kukuza biashara zao, kupata mitaji, masuala ya kodi na kuuliza maswali.

Kadhalika, walipata fursa ya kuanzisha mtandao mpya wa mawasiliano baina yao na wadau wa maendeleo.

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella, ambaye ofisi yake imeshirikiana vyema na TSN katika kufanikisha jukwaa la leo linalotazamiwa kuhudhuriwa na watu zaidi ya 300, ana matumaini makubwa kwamba litawasaidia wawekezaji na wafanyabiashara mkoani mwake kuona fursa zaidi na kubadilika kimtazamo.

Kwa mujibu wa Mongella, Mkoa wa Mwanza una wawekezaji wengi wazawa, lakini pia wengi wao hawajui ni namna gani wanaweza kuingia kwenye uwekezaji mkubwa na wenye tija.

Baadhi ya wadau watakaotoa elimu muhimu kwa wafanyabiashara ni pamoja na mabenki ya NMB, TIB (Development), TIB (Corporate) na Benki ya TPB.

Taasisi hizi za fedha zinatazamiwa kueleza, pamoja na mambo mengine, namna wafanyabiashara wanavyoweza kupata fedha za mitaji kwa kuzingatia masharti muhimu watakayoelimishwa na wataalamu husika.

Wadau wengine ni Kampuni ya Simu ya nchini (TTCL), Mfuko wa Bima ya Afya (NHIF), Kampuni ya Simu ya Vodacom, hoteli ya kisasa jijini Mwanza ya Victoria Palace na Mfuko wa Pensheni wa PPF.

Wengine ni Mamlaka ya Mapato (TRA), Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC), Bohari ya Dawa (MSD) na Watumishi Housing Company (WHC).

Mkoa wa Mwanza ulianzishwa rasmi mwaka 1963 ukiwa na wilaya nne za Ukerewe, Geita, Mwanza na Kwimba. Kwa sasa mkoa una wilaya 8 za Nyamagana, Ilemela, Magu, Kwimba, Misungwi, Sengerema, Buchosa na Ukerewe.

Idadi ya wakazi kwa makadirio ya mwaka 2016 ni 3,155,498 kwa kasi ya ongezeko la asilimia 3 ikilinganishwa na ongezeko la kitaifa la asilimia 2.7.

Mkoa una fursa nyingi za kibiashara, kilimo, uchukuzi, uvuvi, utalii, maendeleo ya makazi na viwanda na ni mkoa wa pili kwa kuongoza katika pato la taifa nchini baada ya mkoa wa Dar es Salaam.

Mkoa pia una fursa ya kuwa kitovu cha uchukuzi na biashara cha Afrika Mashariki na Kati kwani kupitia uwanja wa ndege wa Mwanza, Reli ya Kati na njia za barabara na meli, ni rahisi kuzifikia nchi za Kenya, Uganda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Rwanda, Sudan Kusini na Burundi.