Ujenzi wa hosteli za wasichana uimarishwe

GAZETI hili hivi karibuni lilichapisha habari ya kusikitisha iliyobeba kichwa cha habari: ‘’Wanafunzi wengi wa kike Busega wakatisha masomo yao kwa mimba.’’

Habari hiyo pia ilitoa takwimu kwamba kila wanafunzi 40 wanaojiunga na kidato cha kwanza wilayani Busega, mkoani Simiyu kila mwaka, kati yao 15 hadi 18 hukatishwa masomo yao kwa sababu ya kupata ujauzito.

Hakuna ubishi kwamba kama hali hiyo haitatafutiwa suluhisho la kudumu watoto wengi wa kike katika wilaya hiyo wataendelea kukatishwa tamaa katika harakati za kutimiza ndoto zao za kuwafikisha katika elimu ya juu na kupata ujuzi wa kuwasaidia maishani mwao kama ilivyo wenzao wa kiume.

Hapa tanapenda kumpongeza kwamba mbunge wa jimbo la Busega, Dk Raphael Chegeni kwa kushirikiana na viongozi wenzake jimboni humo kuliwekea mkakati wa kukabiliana vilivyo na tatizo hilo kwa watoto wetu wa kike wilyani humo.

Bila shaka sababu ziko nyingi lakini ile ya kukosa mabweni au hosteli na kusababisha wanafunzi wa kike kutembea umbali mrefu kwenda na kurudi shuleni lina mchango mkubwa katika kufanikisha nia ovu ya wanaume wanaopenda kuwarubuni wanafunzi kwa kutumia shida na udhaifu walionao ili kuwaharibia maisha yao ya kitaaluma.

Mkakati wa mbunge wa Busega, Dk Chegeni wa kujenga hosteli za wasichana kwa shule ya sekondari zilizopo pembezoni mwa jimbo hilo ziungwe mkono kwa kila hali ili kunusuru watoto wetu wa kike wilayani humo kukosa elimu ambayo ni ufunguo wa maisha.

Tunafarijika kupata taarifa kwamba tayari mradi huo wa ujenzi wa hosteli za wasichana umeshaanza kutekelezwa katika shule ya sekondari ya Ngasamo na shule nyingine nne ikiwa ni pamoja na Mkula,Malili,Kabita na Sogesca ziko mbioni kutekeleza mradi kama huo.

Tunapenda kuwapongeza wananchi wa jimbo la Busega pamoja na wadau na washirika wa maendeleo kwa kuunga mkono juhudi za utekelezaji mradi huo ili ufikie lengo lake la kuwapatia malazi karibu na shule zao wanafunzi wa kike.

Tatizo la ukosefu wa hosteli au mabweni ya wasichana halipo katika jimbo la Busega peke yake bali pia katika majimbo na mikoa mingine hapa nchini.

Hali kama hiyo ya wasichana kuingia katika vishawishi vya ngono na hatimaye kuishia kupata ujauzito lipo pia katika maeneo hayo mengine.

Wenzao wa jimbo la Busega wameonesha mfano wa kukabiliana na tatizo hilo na hivyo tungependa pia maeneo mengine nchini yenye tatizo kama hilo la wanafunzi kupata mimba kutokana na sababu za kuishi mbali na maeneo ziliko shule wanazosoma, wajiweke pia katika mipango yao ya maendeleo ya jamii, miradi ya ujenzi wa hosteli za wasichana.

Hapa tunapenda kutoa mwito kwa viongozi wa siasa, serikali, dini na jamii kwa ujumla kushirikiana na kushikamana katika kukabiliana na changamoto hiyo ili watoto wetu wa kike wasikose huo ufunguo wa maisha.