Huduma bora za afya zitawezesha Tanzania ya viwanda

TOLEO la jana la gazeti hili lilikuwa na habari isemayo “Vifaa vya hospitali, tiba vyagawiwa nchi nzima.”

Habari hiyo ilizungumzia hatua ya Serikali kuanza kusambaza vifaa vya hospitali nchi nzima. Ilisema Serikali ya Awamu ya Tano inayoongzwa na Rais John Magufuli, imezindua usambazaji wa vifaa vya hospitali kwa halmashauri zote nchini.

Usambazaji huo ni sehemu ya utekelezaji wa ahadi za Serikali katika mkakati wa kuboresha huduma za afya nchini kwa kuhakikisha wananchi wanapata huduma kwa kiwango na wakati stahiki.

Wakati wa uzinduzi huo wilayani Kongwa katika Mkoa wa Dodoma juzi, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu alisema hatua hiyo pia ni utekelezaji wa ahadi za Serikali kwa wananchi.

Katika uzinduzi huo, Waziri Ummy alisema Serikali imefanya uwekezaji mkubwa katika maeneo kadhaa ya upatikanaji wa dawa na kwamba hata bajeti ya dawa imeongezeka kutoka Sh bilioni 31 mwaka 2015/2016 hadi Sh bilioni 251 katika mwaka wa fedha wa 2016/ 2017.

Sisi tumefarijika kusikia ahadi ya Rais John Magufuli, kununua na kusambaza vitanda kwenye vituo vya umma kwamba tayari wizara kwa bajeti ya mwaka 2016/ 2017, ilitenga Sh bilioni nne kuwezesha kununua na kusambaza vifaa hivyo kwa halmashauri 184 nchini.

Tunasema tumefarijika kwani taarifa zimebainisha kuwa vifaa vya hospitali vitakavyosambazwa katika halmashauri zote 184 nchini ni pamoja na vitanda 3,680, vitanda 920 vya kujifungulia wajawazito, magodoro 4,600 na shuka 9,200.

Kazi ya kusambaza vifaa hivyo inatarajiwa kukamilika kabla ya Juni 30, mwaka huu. Sisi tunaipongeza Serikali kwa uungwana wa kutambua kuwa ahadi ni deni na hivyo kuonesha dalili za wazi kuwa ahadi zozote ilizotoa kwa wananchi itazitekeleza. Hili ni jambo la faraja, kujivunia na kuipongeza Serikali ya Awamu ya Tano.

Tunasema hivyo tukiamini kwa dhati kuwa huduma afya zinapoimarika nchini, zinawawekea wananchi uhakika wa afya bora na hivyo taifa kwanza, kuonesha waziwazi uwajibikaji kwa maslahi ya watu wake, na pia kuonesha umakini katika sera ya kuifanya nchi kuwa ya uchumi wa viwanda.

Tunaipongeza Serikali kupitia Wizara inayohusika na huduma za afya, kwanza kwa kuikumbuka na kuitekeleza ahadi ya Rais Magufuli, na pia kutambua upungufu au mahitaji ya hospitali nchini.

Hii itamarisha safari ya kuelekea Tanzania ya viwanda na hatimaye, Tanzania ya uchumi wa viwanda. Tunasema huduma bora za afya, zitawezesha Tanzania ya viwanda kupatikana na dalili ziko wazi.