Maandalizi Michezo Madola yaanze sasa

MICHEZO ya 21 ya Jumuiya ya Madola itafanyika Gold Coast kuanzia Aprili 4 hadi 15 na Tanzania ni moja ya nchi zinazotarajia kupeleka timu katika michezo hiyo.

Ni muda wa mwaka mmoja tu umebaki kabla ya kufanyika kwa michezo hiyo, ambayo hufanyika kila baada ya miaka minne na tayari watu makini wameanza maandalizi kwa ajili ya michezo hiyo.

Tanzania imekuwa na historia kubwa na nzuri katika michezo hiyo, kwani imekuwa ikifanya vizuri ukilinganisha na mashindano mengine makubwa duniani kama ile ya Olimpiki.

Kwa mara ya kwanza Tanzania ilipata medali ya kwanza kutoka katika michezo hiyo mwaka 1970 wakati bondia Titus Simba (marehemu) alipotwaa medali ya fedha katika ndondi za uzito wa juu.

Wachezaji wa Tanzania waliendelea kufanya vizuri kwa kurudi na medali katika kila michezo ya Madola kuanzia ile ya mwaka 1970 baada ya kuendelea kutwaa medali hadi mwaka 2006.

Tunasema kuwa Tanzania ina historia kubwa katika michezo hiyo, kwani mbali na kutwaa medali pia mwanariadha wake, Filbert Bayi alivunja rekodi ya dunia kupitia michezo hiyo katika mbio za meta 1,500.

Bayi alidumu na rekodi hiyo ya dunia kwa miaka mitano hadi pale alipopokonywa na Muingereza Sebastian Coe, ambaye sasa ni Rais wa Shirikisho la Kimataifa la Vyama vya Riadha (IAAF).

Hatahivyo, pamoja na Bayi rekodi yake ya dunia kuvunjwa baada ya miaka mitano, lakini mwanariadha huyo wazamani bado anashikilia rekodi ya Jumuiya ya Madola ya meta 1,500 kwa miaka 43 sasa bila kuvunjwa.

Kiujumla kuanzia mwaka 1970 hadi 2006, Tanzania imetwaa jumla ya medali 21, huku za dhahabu zikiwa sita na fedha sita wakati shaba ni tisa.

Medali hizo na mafanikio hayo hayakuja kama mvua ila yalifanyiwa kazi, yaani uwekezaji mkubwa ulifanywa na ndio maana tulifanikiwa na hata maandalizi yalifanywa kwa muda mrefu.

Kwa hiyo, hapa siri ya mafanikio ni kufanya maandalizi ya mapena tena ya muda mrefu na sio kusubiri siku zimeisha na kukurupuka kuanza maandalizi, huku tukijua kuwa hatuwezi kufanya vizuri.

Viongozi wa vyama au mashirikisho ya michezo ndio wenye wachezaji na dhamana ya kuwaandaa, lakini wao ndio wamekuwa wakwepaji wakubwa wa kufanya maandalizi mapema au kutafuta fedha.

Viongozi wa michezo wameshindwa kuziandaa timu zao mapema na badala yake wamekuwa wakilazimisha safari hata wakijua kuwa wachezaji wao hawajaandaliwa vizuri.

Hakuna mafanikio ya medali bila maandalizi ya uhakika, kwani tukumbuke kuwa huko nyuma tuliwekeza katika michezo na ndio maana tuliweza kufanya vizuri.