Kwaresma na Pasaka ni maandalizi ya kuwajibika

WAUMINI wa Dini ya Kikristo ambao wamemaliza mfungo wa Kwaresma kwa kuadhimisha kuteswa, kufa na kufufuka kwa Yesu Kristo zaidi ya miaka 2000 iliyopita, wana kazi ya ziada ya kufanya kwa ajili ya usalama wa taifa la Tanzania, kazi ya kuenzi utaifa na kutekeleza maana ya mfungo na pasaka yenyewe.

Tunasema hivyo kwa kuwa maandiko ya dini hiyo yanatangaza upendo, utulivu na amani kama silaha ya imani na katika hilo kwa watu wenye upendo na amani hawatakuwa chachu ya matatizo katika nchi.

Maana halisi ya mfungo wa Kwaresma ilikuwa kujiandaa kubadilika na kuwa kielelezo chema kwa waumini na wasio waumini na wale wanaoabudu Mungu na wasioabudu . Leo wakati wakristo wanaadhimisha Pasaka tunapenda kuwakumbuisha madhila yanayotukuta ambayo ni matokeo ya kukosekana kwa uzalendo na upendo kwetu, ubinafsi na kwa taifa.

Kuwepo kwa vitendo vya kihalifu kwa watu wanaoamini uwapo wa Mungu, ni kwenda kinyume na amana ya kwaresma na Pasaka na hivyo wakati umefika kwa watu kuendelea kuwa na mwenendo mwema badala ya kuupoteza baada ya kumalizika kwa kwaresma na kufufuka kwa Kristo.

Kwa watu wanaojua maana ya Pasaka wakiitekeleza maana yake hakika Tanzania itakuwa ni mahali bora kabisa pa kuishi na kutekeleza maana ya uhai hapa duniani. Ndio maana si ajabu ujumbe unaotolewa kuanzia Ijumaa Kuu hadi leo Jumapili ya Pasaka ni kuhusu maana na matumizi ya mateso ya Yesu Kristu msalabani kama kielelezo cha kuishi vizuri na kupendana ufufuko wake ukionesha maana uya kuanza uopya katika maisha ya binadamu maisha yenye kumuogopa Mungu na kutekeleza maagizo yake.

Wakati tukiwatakia Wakristu Pasaka njema, tunawaomba pia kuwa na kiasi kwani kutangaza upendo wa Mungu una maana kubwa katika maisha ya sasa hapa duniani ya kutekeleza wajibu mbalimbali ambazo tumekabidhiwa na familia au nchi katika kutafuta ustawi wa binadamu.

Ni dhahiri kama watu watafuata maagizo na maelekezo ya viongozi wa dini kuhusiana na maadhimisho hayo ambayo yamelenga kuongeza maarifa kwa binadamu kwa kuwajaza upendo wenye tafsiri ya kuvumiliana na kusaidiana yataongezeka na ongezeko hili litawezesha utunzaji wa familia kwa umoja na hivyo kuhakikisha hakuna mhitaji atakayebaki akilalama kwa kukosa msaada.

Na upendo huu utaambukizwa katika kazi zetu na wajibu wetu kwa wenzetu na mamlaka, hivyo kuwezesha maisha kwenda katika hali inayostahili na kupaswa kuwa.

Na kama kila mtu atatekeleza wajibu wake, kitakachofuata ni ujenzi wa taifa hili ambalo linataka kuelekea katika ustawi wa watu wake wote; kwanza kwa kutambua msingi na maana ya kazi na huduma zinazostahili kutolewa na Mamlaka ambazo zinasimamiwa na watu wenyewe wengi wao wakiwa wanaoamini uwapo wa Mungu na upendo wake na pili kuacha kuchezea utu kwa kuingiza uhalifu ambao unaendelea kukandamiza ustawi wa jamii.

Tunaamini mafundisho ya Kwaresima na imani ya ufufuko wa Kristo baada ya mateso yatakuwa ni injini bora ya kuambukiza upendo katika jamii yetu ya Watanzania ili sote kwa pamoja tufikie ustawi wa kweli wenye haki ndani yake.