Tudumishe amani na umoja wa taifa

WAKRISTO wa Tanzania jana waliungana na wenzao duniani, kusherehekea sikukuu ya Pasaka, ambapo viongozi wa dini walihubiri na kutoa kauli na mafundisho mbalimbali kwa waumini na watanzania kwa ujumla.

Miongoni mwao ni Askofu Isack Amani wa Jimbo Katoliki la Moshi mkoa wa Kilimanjaro, Askofu Godfrey Sehaba wa Kanisa Anglikana Morogoro na Askofu Telesphor Mkude wa Kanisa Katoliki Jimbo la Morogoro.

Walitaja mfano wa matukio yanayochafua sifa ya taifa ni mauaji ya askari wanane, yaliyofanywa na majambazi mkoani Pwani wiki iliyopita.

Matukio mengine yanayoharibu sifa na hadhi ya taifa ni mauaji ya vikongwe na watu wenye ualbino, biashara haramu ya binadamu, ubakaji, ulawiti, utekaji, utesaji wa watu na upoteaji wa watoto.

Maaskofu hao wanasema waumini wanaungana na Watanzania wengine, kulaani matukio yanayoharibu sifa ya taifa, ikiwemo tukio hilo la mauaji ya polisi wiki iliyopita na mengine mara kadhaa yaliyotokea tangu mwaka jana.

Kwamba nchi yetu imekuwa kisiwa cha amani kwa muda mrefu, hivyo mauaji hayo, hayavumiliki na jamii ya Watanzania.

Tunaunga mkono kuwa hali si nzuri, kwani matukio ya uhalifu yanazidi kuongezeka mijini na vijijini kila siku na yapo katika sura mbalimbali, hivyo kuhatarisha amani na umoja.

Watanzania hatuna budi kutunza umoja na amani yetu, iliyodumu kwa kipindi chote cha zaidi ya miaka 50 tangu tupate Uhuru, kwani endapo itapotea itakuwa kazi kubwa kuirudisha.

Ipo mifano ya nchi kadhaa, ikiwemo jirani, ambazo baada ya amani kupotea, imekuwa kazi ngumu kuirejesha.

Jambo lingine ambalo viongozi wa dini, waliwaasa waumini jana ni kuacha ulevi; na pia kuacha kupoteza muda, kwani kwa sasa watu wengi hawajui thamani ya muda na hawana mipango wala malengo huku siku zikizidi kusonga mbele.

Pia viongozi wa dini walitaka waumini kuacha kutumia fedha katika mambo ya ovyo na yasiyo na msingi. Endapo fedha hizo, zingetumiwa kwenye masuala ya maendeleo, watu hao wangekuwa mbali katika masuala ya maendeleo.

Aidha, tunaunga mkono kauli za viongozi wa dini za kutaka Watanzania kufuata maelekezo ya serikali ya kukata bima ya afya, kwa kuwa bima ya afya ndio mkombozi wa watu wengi, hasa wenye kipato cha chini.

Kwa sasa matibabu yana gharama kubwa na watu wengi wamepoteza maisha kwa kukosa bima ya afya. Njia pekee ni kukata bima ya afya na kulipa kidogo kidogo, kisha kupata matibabu wakati wowote.

Kitu kingine walichosisitiza viongozi wa dini ni kuliombea taifa, liendelee kudumisha umoja na amani.

Madhehebu yote ya dini nchini, yanatakiwa kuliombea taifa kila siku bila kukoma ili liweze kusonga mbele kiuchumi na kijamii na kujiepusha na umwagaji damu usiokuwa wa lazima kwa wananchi wake.