Tunaipongeza Takukuru kuokoa mabilioni

TAARIFA kwamba Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) imefanikiwa kuokoa zaidi Sh bilioni 12.3 mwaka huu wa fedha, huku Sh milioni 912 zikiokolewa kutoka katika mishahara hewa, haiwezi kupita bila kupongezwa kwa kuwa imetekeleza maagizo ya Rais John Magufuli kwa kiasi kikubwa.

Pia Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora), Angellah Kairuki alisema wakati akiwasilisha bajeti ya wizara yake juzi kuwa Takukuru imepanga kuendelea na kesi 409 zilizopo mahakamani, zikiwa ni sehemu ya kesi 706 zilizoendeshwa, zikiwamo mpya 227.

Zaidi ya mara mbili, Rais Magufuli amekuwa akizitaka taasisi nyeti, ikiwemo ya Mahakama, Polisi, Takukuru, TPA na TRA kufanya kazi kwa umakini kwa kuwa taasisi hizi zimebeba majukumu makubwa na mazito ambayo ni uti wa mgongo wa Taifa.

Pia Rais Magufuli amelivalia njuga suala la wafanyakazi hewa kiasi kwamba tangu mwaka jana, alilazimika kusitisha ajira serikalini ili kutoa nafasi kwa Wizara na taasisi zenye dhamana kushughulikia suala hilo kwa umakini.

Taarifa hiyo ya Takukuru ni moja ya ishara kwamba maagizo ya Rais Magufuli yanafanyiwa kazi kwa vitendo. Tumeona kazi inayofanyika TRA na TPA. Tumeshuhudia wafanyakazi hewa wakiendelea kubainishwa kila idara, wizara na taasisi nyeti za serikali.

Rais Magufuli akizungumza na majaji hivi karibuni aliwataka kuwa makini kwa kuwa kesi zinazopelekwa mahakamani, serikali imekuwa ndiyo inayopoteza kwa kuwa ama na ushahidi hafifu au kutokuwepo na ushahidi kabisa, hivyo kuifanya serikali mara kwa mara kulipa gharama za kesi hizo.

Ndio maana tunaipongeza Takukuru kwani katika taarifa hiyo ya bajeti ya Waziri, imesema kesi 264 ziliamuliwa mahakamani ambapo kati ya hizo, kesi 103 walipatikana na hatia na kuhukumiwa kifungo au kulipa faini. Ingawa zipo kesi 161 watuhumiwa wake waliachiwa huru na kesi 33 ziliondolewa mahakamani kutokana na sababu mbalimbali.

Waziri akasema fedha nyingine zilizookolewa na kurejeshewa serikalini ni Sh bilioni 8.003 zilizotokana na ukwepaji ushuru kupitia mfumo wa kielektroniki wa EFDs, Sh bilioni 2.6 kutokana na ubadhirifu. Kiasi cha Sh milioni 794.18 ziliokolewa katika maeneo mengine.

Hizi ni fedha nyingi ambazo zitaisaidia serikali katika baadhi ya maeneo muhimu. Tunaamini, kupatikana kwa fedha hizo kunaongeza hali pia kwa taasisi nyingine kuiga mfano. Kairuki akaongeza kwamba kutokana na kuimarika kwa kitengo cha ufuatiliaji na urejeshaji wa mali, Takukuru imefanikiwa kutaifisha nyumba sita na kutaifisha pia magari manne, mawili aina ya Toyota Chaser, jingine Toyota Land Cruiser na Mitsubishi Fuso yaliyopatikana kwa njia ya rushwa.

Takukuru haijaishia hapo, imefanya utafiti pia wenye lengo la kuimarisha mifumo ya udhibiti wa mianya ya rushwa katika sekta za uhamiaji na afya. Utafiti huo umehusisha uchambuzi wa mianya ya rushwa katika mfumo wa utoaji wa hati za kusafiria na tathimini ya uzingatiaji wa sheria na kanuni za uanzishaji na usimamizi wa maduka ya dawa muhimu.