Sasa madaktari wa Rais Magufuli chapeni kazi

TOLEO la jana la gazeti hili lilikuwa na habari kubwa iliyobeba kichwa cha habari: “JPM awashushia neema madaktari. Madaktari hao ni wale 258 waliokuwa waende kuajiriwa nchini Kenya.

Habari hiyo njema kwa watanzania ilitangazwa juzi mjini Dodoma na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu. Hatua hiyo ya Serikali inayopongezwa na wananchi kila kona kikiwamo Chama cha Madaktari Tanzania, imetokana na uungwana uliooneshwa na Tanzania kwa majirani zetu wa Kenya walioomba msaada wa madaktari 500 ili kuokoa maisha ya ndugu zao wa Kenya katika nyanja hiyo ya matibabu.

Kutokana na ombi hilo, Machi 18, mwaka huu Serikali ilitangaza nafasi za ajira kwa madaktari 500 wenye sifa na utayari kwenda kuwasaidia majirani hao. Jumla ya madaktari 498 walijitokeza na kati yao, 258 walikidhi vigezo vilivyotakiwa.

Waziri Ummy aliweka bayana kuwa uamuzi wa Rais Magufuli umetokana na madaktari hao kuwekewa pingamizi mahakamani nchini Kenya na madaktari wenzao waliopinga madaktari wa Tanzania, kwenda kufanyakazi nchini humo.

Licha ya utekelezaji wa mpango huu kulengwa kukamilika Aprili 6 na safari ya kwenda Kenya kupangwa iwe Aprili 6 -10, mwaka huu, Mahakama ya Kenya haijaondoa pingamizi lililowekwa na madaktari wa Kenya dhidi ya madaktari wa Tanzania.

Hatutaki kujikita katika sababu za Kenya kuomba msaada wa watanzania, bali tunaipongeza Serikali ya Tanzania kwa kuwa imeua ndege watatu kwa jiwe moja. Tunasema ndege watatu kwa sababu uamuzi wa Rais Magufuli kukubali kuwatoa madaktari nchini kwenda kuwahudumia majirani, umeouonesha ulimwengu kuwa uwezo wa Tanzania hauko katika ukarimu na nguvu za kijeshi pekee kiasi cha kwenda kulinda amani katika baadhi ya nchi za Afrika, bali pia kwamba Tanzania inao wataalamu wake wa ndani, tena wa kutosha.

Hii inaonesha kuwa, Serikali ilikuwa na mpango huo wa kuajiri madaktari hao kuwatumikia watanzania ndiyo maana imesema, itakuwa tayari wakati wowote kushughulikia ombi la Kenya la kupatiwa madaktari 500.

Tunasema hatua hiyo pia itasaidia kupunguza tatizo la ukosefu wa ajira na kuchochea uboreshaji wa huduma hizo nchini. Naye Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania, Dk Obadia Nyangole amesema hadi ifikapo Oktoba mwaka huu, Tanzania itakuwa na madaktari 2,883 ambao watakuwa hawajapata ajira.

Hakuna ubishi kwamba madaktari ni wachache na siyo hapa nchini tu bali karibu duniani kote. Ukweli huu unatokana na mambo mengi ikiwa ni pamoja na unyeti na ugumu wa masomo yake, gharama kubwa za mafunzo na muda mrefu wanaotumia wanafunzi hadi kufikia kuhitimu kuwa daktari kamili wa kutoa tiba kwa wagonjwa.

Tunaipongeza serikali kwa hatua hii ya kuwaajiri madaktari hao na bado kuna wengine ambao hawajapata ajira. Tunaamini kwamba wakati wowote tupatapo mwanya wa kuwaajiri basi wapewe nafasi hiyo.