Tanesco hongera kwa kuzinduka

TAARIFA ya kuwa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) limeanza kufanyia kazi maagizo ya Rais John Magufuli ya kulitaka kuachana na umeme wa majenereta ni taarifa muhimu ambayo kila mtanzania anayependa maendeleo ya taifa hili atajivunia.

Tunasema kila mtanzania atapenda kujivunia kwa kuwa bei ya umeme pamoja na kuyumbisha shirika la Tanesco pia linakuwa kama kidonda kibichi kinachotiwa chumvi kila mara hivyo kuleta ukakasi wa maisha.

Aidha ili kuwa na uhakika wa maendeleo suala la uwepo wa nishati inayoaminika na yenye bei nafuu ni muhimu sana. Siku chache zilizopita Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad katika ripoti yake alisema kwambaTanesco haiwezi kupata faida kwa vile inatumia gharama kubwa kununua umeme ukilinganisha na bei inayouza kwa wananchi.

CAG katika ripoti hiyo ya mwaka 2015/2016 aliyowasilisha kwa Rais Magufuli na baadaye Bungeni hivi karibuni, amesema Tanesco inanunua umeme kutoka kwa wazalishaji kwa wastani wa Sh 544.65 kwa uniti moja na kuuza kwa watumiaji kwa wastani wa Sh 279.35.

Katika hesabu hizi ni hakika hasara ya Sh 265 kwa kila uniti moja ya umeme inayouza ni changamoto kubwa katika kufanya maendeleo katika miradi ya kuweza kuitosheleza umeme nchi hii.

Kauli iliyotolewa na shirika hilo inaonesha kuzinduka na kuanza kuchukua hatua za kuanza kutegemea maji na gesi kama vyanzo muhimu vya kuzalishia umeme wa bei nafuu inatoa taswira nzuri ya hali ya baadae ya upatikanaji wa nishati nchini.

Ikumbukwe kwamba hakuna safari ya kuelekea uchumi wa kati kama taifa litakuwa na nishati ya kubahatisha tena yenye gharama kubwa. Hivyo tunapongeza Mkakati wa Tanesco kuamua kuivalia njuga kampeni iliyoasisiwa na Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan ya kuokoa mfumo wa ikolojia katika bonde la mto Ruaha Mkuu ambao ni tegemeo kwa mabwawa muhimu ya kuzalishia umeme ya Mtera na Kidatu.

Kauli ya kaimu Meneja wa Mawasiliano wa Tanesco, Leila Mhaji kuwa uongozi wa Tanesco umeamua kuitumia kampeni ya Makamu wa Rais ya kuokoa ikolojia ya Bonde la Mto Ruaha ili kuboresha mabwawa ya Mtera na Kidatu ni ya kutia matumaini makubwa.

Tumaini ushirika wao umelenga kuhakikisha kwamba wanashirikiana na wadau wote muhimu ili kuhakikisha kuwa mtiririko wa maji kuelekea mabwawa ya Mtera na Kidatu ambayo ni tegemeo kubwa kwa uzalishaji wa umeme unaimarika na kuwa bora ili kuondokana na tegemezi la umeme wa mafuta.

Ni tegemeo letu kwamba kamaTanesco wakizingatia maagizo yote yaliyotolewa kwao namna ya kuzalisha umeme rahisi kutatupa nafuu ambayo watanzania wote wanaitaka. Ni wazi kuwa pamoja na kampeni hiyo kusaidia katika uhifadhi wa mazingira lakini itasaidia kwa kiwango kikubwa kukabili tatizo la upungufu wa maji katika mabwawa ya Mtera na Kidatu ambalo kwa kiwango kikubwa linakwamisha uzalishaji wa umeme nafuu.

Ni kweli kama alivyosema, Profesa Assad kuna ulazima wa kufanya juhudi za makusudi kuinusuru Tanzania na bei ghali ya nishati ili uwekezaji uwe nafuu na Tnaesco yenyewe kupumuia ili kufikiria vyanzo zaidi vya nishati na hivyo kusonga mbele katika ndoto ya kuwa na Tanzania ya viwanda.